Saturday, 11 June 2016

TCU SASA KUHAKIKI WANAFUNZI VYUONI

FAGIO la chuma limeanza kutua katika vyuo vikuu hapa nchini, baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kuanza mchakato wa kuwahakiki wanafunzi walioko vyuoni.

TCU imesema hatua ya kuhakiki wanafunzi hao ni jambo linalofanywa kila mwaka kwa ajili ya kutambua wanafunzi halali walioko vyuoni.

Akizungumza na Uhuru, mjini Dar es Saalam, jana,Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku, alisema mchakato huo wa kuwahakiki wanafunzi hao ni mwendelezo, kwani hufanyika mara kwa mara.

Mkaku alisema maofisa hao wa TCU wanafanya ukaguzi huo katika kila chuo, ambapo wanafunzi watatakiwa kuwasilisha vyeti vya kidato cha nne, sita na stashahada ili viweze kuhakikiwa.

Katika ukaguzi huo, TCU itapitia tarifa za wanafunzi wote kuanzia vigezo zilivyotumika kudahiliwa chuoni na kwamba, ikishindikana kufanya hivyo, itasababisha wanafunzi hao kuondolewa vyuoni mara moja.

Hata hivyo, utaratibu huo wa TCU umelalamikiwa na baadhi ya wanafunzi kwa madai kuwa, baadhi ya wanafunzi huviacha vyeti vyao nyumbani au shuleni.

Solomoni Makombe, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini cha Makumira kilichoko Arusha, alisema pamoja na hatua hiyo ya ukaguzi kuwa nzuri, lakini ni vema TCU ikajenga utaratibu wa kutoa taarifa mapema kwani baadhi yao huviacha vyeti vyao nyumbani au shuleni.

"Wanafunzi wengi wameviacha vyeti vyao nyumbani na mashuleni walikomalizia, hususan kwa upande wa shule za sekondari na kwamba mchakato huo ni hatua nzuri ya kuwaondoa wanafunzi feki waliogushi vyeti," alisema

Alisema ni vyema TCU ikatoa taarifa za ukaguzi mapema na sio kufanya hivyo kwa kushtukiza.

No comments:

Post a Comment