Saturday, 11 June 2016
FILAMU YA WAPINZANI YAZIDI KUNOGA BUNGENI
HATIMAYE kambi ya upinzani bungeni imesalimu amri baada ya kusoma hotuba ya kambi hiyo wakati wa kikao cha bunge, kilichoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
Hotuba hiyo ilisomwa bungeni jana na Msemaji Mkuu wa kambi ya upinzani katika Wizara ya Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Momba (CHADEMA), David Silinde.
Silinde alisoma hotuba hiyo kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/17 na Mapendekezo ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Uamuzi wa kambi ya upinzani kusoma hotuba hiyo, umekuja siku chache baada ya Naibu Spika, Dk. Tulia kusema kuwa, wabunge wote waliokuwa wakisusia vikao vya bunge bila sababu za msingi, watakatwa posho.
Awali, wabunge hao waliapa kususia vikao vyote vya bunge vilivyoongozwa na Dk. Tulia, kwa madai kuwa amekuwa hawatendei haki, ikiwa ni pamoja na kutowapa nafasi ya kuomba miongozo.
Wabunge hao wa upinzani walikuwa na kawaida ya kutoka nje ya ukumbi wa bunge, kila Naibu Spika Dk. Tulia alipokuwa akiingia bungeni kuongoza vikao.
Lakini hali ilibadilika jana. Japokuwa wabunge hao walitoka nje ya ukumbi wakati wa kipindi cha maswali na majibu baada ya kumuona Naibu Spika akiingia ndani ya ukumbi wa bunge, Silinde alibaki ukumbini kwa ajili ya kuwasilisha hotuba hiyo.
Baada ya kumaliza kusoma maelezo ya awali kuhusu hotuba hiyo, Silinde naye alitoa nje ya ukumbi kabla ya kurejea tena bungeni, muda wa kuwasilisha hotuba hiyo ulipowadia.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia, aliwasilisha taarifa ya kamati ya bunge ya bajeti kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2015, mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2016/17, tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2015/16 na mapendekezo ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Baada ya mwenyekiti huyo kumaliza kuwasilisha taarifa hiyo, ilifika zamu ya kambi ya upinzani, ambapo Silinde, alisimama na kusoma hotuba ya kambi hiyo.
Kwa takriban wiki mbili sasa, wabunge hao wamekuwa wakipishana na Dk. Tulia, kila anapoingia ukumbini, kwa madai kuwa hawana imani naye na wameshawasilisha malalamiko yao katika ofisi ya spika.
Juni 8, mwaka huu, Naibu Spika alitangaza uamuzi wa ofisi ya bunge wa kuwakata posho wabunge wa kambi hiyo, kutokana na kutoshiriki ama kuhudhuria vikao vya bunge bila sababu za msingi.
Wabunge hao walianza kususia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika wakati wa sakata la wanafunzi wa mafunzo maalumu ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment