UAMUZI wa serikali kuondoa msamaha wa kodi kwenye mafao ya wabunge wakati wa kupokea kiinua mgongo cha miaka mitano, umeonekana kuwa mwiba kwa wabunge, ambapo baadhi yao wameanza kuwa na mtazamo tofauti.
Akichangia bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema uamuzi wa serikali kuondoa msamaha wa kodi kwenye mafao ya wabunge ni jambo, ambalo haliko sawa kwa kuwa wabunge hawana pensheni,
wanategemea kiinua mgongo kujikimu baada ya utumishi wao.
Mbunge huyo alimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philp Mpango, kutocheza na maslahi yao, huku akiwasihi wabunge wenzake kutolikubali jambo hilo na walinde maslahi yao kwa kuwa hawana pensheni.
Alisema mshahara wa wabunge ni mdogo kuliko wa waziri, hivyo kutaka waondolewe kodi ni kucheza na maslahi yao.
Mbunge huyo alisema Dk. Mpango 'amewabeep' wabunge, nao watampigia kwa kuwa hawakubaliani na makato hayo.
Aidha, alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa juhudi zake za kutumbua majipu na kushughulikia mafisadi, ikiwemo uamuzi wake wa kutaka kuanzisha mahakama ya mafisadi.
Alisema juhudi za rais haziwezi kuzaa matunda bila kazi kubwa inayopaswa kufanywa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwenye jukumu la kukagua miradi na kubaini mafisadi huku ofisi yake ikiwa imetengewa kiasi kidogo cha fedha.
Lugola alisema kama CAG ataminywa fedha zaidi, itakuwa ngumu mafisadi kubainika na rais hatakuwa na kijipu uchungu wala kipele cha kutumbua kwa kuwa CAG atakuwa hajafanya kazi yake.
Kwa upande wake Mbunge wa Mkinga (CCM), Danstan Kitandula, alisema kamati ya bajeti imefanya kazi kubwa, huku akiwaasa wabunge wenzake kusoma sana hotuba ya kamati kwa kuwa imefanya kazi ya kizalendo.
Mbunge huyo alisema suala la wabunge kuondolewa msamaha wa kodi katika mapato yao si sahihi na ni sawa na kuwarudisha nyuma walikotoka.
Aliwataka wabunge wenzake wasikubali kukatwa posho hizo na kuongeza kuwa, anaunga mkono maoni yaliyotolewa na kamati.
Hata hivyo, Kitandula alisema kwa kuwa serikali ni sikivu, anaamini itakubali kufuta mpango huo.
“Kamati ya bajeti imesema tuweke tozo kwenye mafuta, mbona Kenya imeweka juzi, sisi tunashindwa nini? Tuweke ili tujenge zahanati. Ni aibu kuweka kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM bila kuifanyia utekelezaji,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mwanne Nchemba, alipendekeza kuongezwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya wanawake.
Akizungumzia sh. milioni 50 zitakazotolewa na serikali kwa kila kijiji,
alishauri zipelekwe ngazi kwa ngazi, kuanzia wilaya na mkoa ili watu wote wanufaike, kupitia wataalamu wa wizara ya fedha ili wasimamie ugawaji, badala ya kupitisha kwenye SACCOS.
Mbunge wa Ushetu (CCM), Elias Kuandikwa, alitaka Idara ya Takwimu iwezeshwe ili iweze kutoa takwimu zilizo sahihi.
Alisema bajeti hiyo ina maeneo muhimu kama uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na mengine mengi na pia inaonyesha dhamira ya serikali ya kutaka wategemee mapato ya ndani.
Awali, akisoma taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2015, mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2016/17, tathimini ya utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2015/16 na mapendekezo ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia, alisema kamati inashauri serikali kuondoa mpango wa kutoza kodi viinua mgongo vya wabunge, kwani kukata kodi kwenye fedha hizo ni ulipaji kodi mara mbili.
No comments:
Post a Comment