WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Mzee John Malecela, amesema bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, iliyotangazwa Jumatano, wiki hii, haijawahi kutokea.
Malecela, alisema hayo nyumbani kwake mjini Dodoma, jana, alipokuwa akizungumza na Uhuru, ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kusoma bajeti hiyo bungeni mjini Dodoma.
Alisema bajeti ya mwaka huu, imeelekezwa katika kutekeleza ahadi alizozitoa Rais John Magufuli, wakati alipokuwa akiwaomba kura Watanzania kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliofanytika Oktoba 25, mwaka jana.
"Kwa kweli bajeti ya mwaka huu ni nzuri sana. Naamini yale ambayo yaliahidiwa katika kampeni za Dk. Magufuli, sasa yanakwenda kutekelezwa bila tatizo,"alisema.
Alisema bajeti hiyo inaipeleka Tanzania kwenye siasa na kujitegemea, hivyo Watanzania wana kila sababu ya kumuunga mkono Rais Magufuli.
Malecela alisema vipo vegezo vinavyomsukuma kuiona bajeti hiyo kuwa ni nzuri, ikiwa ni pamoja na aina ya matumizi yaliyopangwa, ambayo yamewagusa wananchi moja kwa moja huku ikilenga kuimarisha udhibiti katika ukusanyaji mapato ya nchi.
Aidha, alisema ili bajeti hiyo iweze kutekelezeka, ni lazima kila Mtanzania afanyekazi na kuachana na maisha ya mazoea ya kuendelea kupiga kelele na kuinyooshea kidole serikali kwamba haifanyi lolote la maana kwa wananchi.
"Kila Mtanzania kwa nafasi yake, lazima ajiulize ameifanyia nini nchi kuanzia asubuhi anapoamka hadi jioni na kama hakuna mchango alioutoa, basi atambue kwamba yeye ni miongoni mwa wanaoikandamiza Tanzania na hana haja ya kulalamika,"alisema.
Kwa mujibu wa Mzee Malecela, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu, ni vema kila Mtanzania akatoa mchango kwa taifa ili kuliongezea mapato yatakayowezesha kutekelezwa yale yalioahidiwa na serikali.
Pia, Mzee Malecela ametoa wito kwa watumishi wa serikali, kuhakikisha wanamsaidia Rais Magufuli kwa vitendo na si kumhujumu ili aonekane hafanyikazi.
"Nawaomba wananchi iwapo wanaona kuna mambo hayaendi sawa, wapige kelele ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa watumishi, ambao hawatimizi wajibu wao. Tumeona hatua zimeshaanza kuchukuliwa kwa watendaji wa aina hiyo,"alisema.
Kuhusu suala la kutengwa fedha kwa ajili ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi, Malecela alipongeza uamuzi huo kwa kuwa utatenda haki kwa wale, ambao wamekuwa wakiibia serikali, lakini mahakama za kawaida zinashindwa kuwatia hatiani.
"Nakumbuka miaka ya nyuma, mahakama kama hizi zilikuwepo na zilisaidia kuwatia hatiani na kuwachukulia hatua wahusika,"alisema.
No comments:
Post a Comment