SERIKALI imekubaliana na mifuko ya hifadhi ya jamii kuanza utekelezaji wa ujenzi wa viwanda nchini ili kuhakikisha kuwa azma ya Tanzania ya kufikia uchumi wa viwanda inafanikiwa ifikapo mwaka 2020.
Utekelezaji huo unatokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli, aliyeitaka mifuko hiyo kuwekeza katika ujenzi wa viwanda nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema hayo juzi, baada ya kikao cha pamoja baina ya serikali na mifuko hiyo.
Jenista alisema serikali imekusudia kuhakikisha uanzishwaji wa viwanda unaanza haraka na kuongeza fursa za ajira nchini.
Alisema malighafi na nguvu kazi ya kutosha zipo nchini, hivyo hakuna sababu ya kuchelewa kuanza, ambapo serikali imepanga hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, utekelezaji wa azma hiyo uanze kuonekana machoni mwa Watanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka, alisema agizo hilo limekuja wakati muafaka kwa kuzingatia kwamba, mifuko hiyo imekusudia kutekeleza kwa vitendo azma ya serikali inayosisitiza kuijenga Tanzania kupitia uchumi wa viwanda.
Kwa mujibu wa Irene, kanuni na mifumo ya mifuko hiyo inaruhusu suala la uwekezaji katika viwanda ama kwa njia ya ubia, hati fungani au kutoa mikopo kwa wanaotaka kuwekeza katika viwanda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru, alisema uwekezaji katika viwanda ni suala, ambalo linawashirikisha wadau wengi, zikiwemo Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya malighafi za viwandani, elimu kwa ajili ya ujuzi wa watu wa kufanya kazi viwandani na Wizara ya Nishati na Madini kwa ajili ya nishati ya kuendesha viwanda.
“Kwa kuangalia raslimali tulizonazo, tumewaomba wadau waanze na viwanda, ambavyo vilikuwepo, lakini kwa sasa havifanyi kazi kama vile Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), General Tyre, NARCO na Kiwanda cha Viwadudu cha Kibaha,”alisema.
Pia, alisema malighafi za viwanda hivyo zinapatikana nchini.
No comments:
Post a Comment