Saturday, 11 June 2016
NAIBU SPIKA AAGIZA SUGU ACHUNGUZWE, ADAIWA KUTOA ISHARA YA MATUSI BUNGENI
NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kufanya uchunguzi kuhusu kitendo, ambacho kina tafsiri ya matusi na ni kinyume cha maadili ya bunge cha kuonyesha alama ya kidole wakati wa kutoka nje, kinachodaiwa kufanywa na Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi 'Sugu'.
Dk. Tulia alitoa kauli hiyo bungeni mjini hapa jana, wakati akijibu muongozo ulioombwa na Jaquline Msongozi, kuhusu kitendo cha
Mbilinyi kulidhalilisha bunge na kudharau mamlaka ya Spika kwa kuonyesha alama ya kidole, kitendo ambacho amedai ni matusi.
Muongozo huo uliombwa Juni 6, mwaka huu, katika kikao cha 37 cha mkutano wa tatu wa bunge, ambapo mbunge huyo alitumia
kanuni ya 68, fasiri ya saba ya kanuni za kudumu za bunge.
Mbunge huyo alieleza kuwa, kitendo hicho kilifanyika wakati Mbilinyi akitoka nje ya ukumbi wa bunge, baada ya kuwasilisha maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu azimio la bunge, kuridhia mkataba wa kimataifa wa uthibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.
Katika kujenga hoja juu ya muongozo huo, mbunge huyo alisema wakati Mbilinyi alipokuwa anaondoka, baada ya kuwasilisha hoja zake, alionyesha alama ya kidole, ambayo ni matusi makubwa sana, kitendo ambacho alidai ni kulidharirisha bunge, lakini pia kukidharilisha kiti cha Spika.
Aidha, Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM, Sixtus Mapunga, naye alisimama sambamba na Jaquline, kuashiria kuomba muongozo na alipopewa nafasi, alieleza kuwa muongozo aliotaka kuomba ilikuwa ni hoja iliyowasilishwa na mbunge aliyepewa nafasi kabla yake.
Akijibu muongozo huo, Dk. Tulia alisema binafsi hakumuona Mbilinyi iwapo alionyesha ishara iliyolalamikiwa kuwa ni mbaya na ni matusi na kuongeza kuwa, ameiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kufanya uchunguzi.
Alisema amefikia uamuzi huo kwa sababu jambo linaloombewa muongozo linahusu maadili ya bunge na muongozo huo unatokana na kitendo cha mbunge kuonyesha kitendo ambacho kina tafsiri ya matusi.
Naibu Spika alisema endapo itadhibitika kuwa kitendo hicho kimefanyika, itakuwa ni kinyume na masharti ya kanuni ya 74 ya kanuni za kudumu za bunge.
Alisema kwa mujibu wa nyongeza ya nane kifungu cha nne, fasiri ya kwanza ya kanuni za kudumu za bunge, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya bunge, pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya wabunge.
“Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya bunge, itashughulikia mambo yanayohusu maadili ya wabunge, yatakayopelekwa na spika,” alisema Naibu Spika, akinukuu kanuni za bunge.
Alisema kamati hiyo itafanya uchunguzi wa tuhuma hizo kwa mujibu wa kanuni za bunge na kuchukua hatua stahiki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment