KAMISHNA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, Simon Sirro,
amewataka watu waliotajwa, wakihusishwa na biashara na utumiaji wa dawa za
kulevya, kujisalimisha kabla ya kutumika kwa nguvu ya dola.
Kamishna Sirro aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na
waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.
Alisema watu hao, ambao
hawajatii agizo hilo, wanatakiwa kuripoti haraka ili kufanyiwa mahojiano kwa ajili
ya kufahamu ukweli juu ya tuhuma zinazowakabili.
Kamanda Sirro aliongeza kuwa, watu hao ni wale ambao walitajwa
na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam, Paul Makonda.
“Bado kuna watu wachache, ambao walitajwa kwenye tuhuma za dawa za kulevya kwamba wanahitajika,
hivyo wajisalimishe wenyewe,”alisema
Kamanda huyo alisema, watu hao walipaswa kuitikia agizo hilo la
kujisalimisha kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano siku nyingi, badala yake
hawajitokezi, kitu ambacho kitalifanya jeshi hilo kutumia nguvu za dola
kuwakamata.
Alisema ni vyema watu hao wajisalimishe wenyewe kabla ya kutumia
nguvu kuwafuata na kwamba, sio jambo jema kutumia nguvu hizo.
“Waje wenyewe kuhojiwa na kitendo cha kukaa kimya kwa watu hao
ni ishara ya kupuuzia agizo hilo, ambalo limetolewa na kusisitizwa kwa lengo la
kufanyiwa mahojiano ili kubaini ukweli,”alisema.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 40,
kwa makosa ya dawa za kulevya, ambapo watu hao walipekuliwa na kuhojiwa kwa
kina.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwenye
oparesheni maalumu iliyoanza tangu Februari, mwaka huu, ambapo kati ya
watuhumiwa hao, 33 walifanyiwa vipimo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Katika vipimo hivyo, Mkemia Mkuu huyo wa serikali alibaini kuwa,
watuhumiwa hao ni watumiaji wa dawa za kulevya, ambapo hadi sasa 19, wamefikishwa
mahakamani, ”alisema.
Aliongeza kuwa tayari majalada matano yamekwishaandaliwa kwa
ajili ya kufikishwa mahakamani huku tisa yakiwa bado kwa mwanasheria mkuu wa
serikali kwa ajili ya uandaaji wa mashitaka.
Machi 4,mwaka huu, kikosi hicho cha oparesheni ya kupambana na
dawa za kulevya, kiliwakamata watu wawili eneo la Vikindu, wilaya ya Mkuranga, ambao
ni Khalid Mtumwa Jadi na Said Juma Khasam, wakiwa na dawa za kulevya aina ya Heroine
kete nane.
Aidha, Machi 9,mwaka huu, katika maeneo ya Mbagala Zakheem,
kikosi hicho kilimkamata Rafii Mohamed Nditi, akiwa na kete sita na gramu moja
za dawa za kulevye aina ya Heroine.
Kamanda Sirro alisema hadi sasa upelelezi wa majalada yote ya
watuhumiwa wa dawa za kulevya bado unaendelea kwa ajili ya kupelekwa katika
ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka.
Wakati huo huo, jeshi hilo linamshikilia Musuguri David
Sylvester, kwa mauaji ya mke wake, ambaye ni Samira Masoud (34), ambaye aliuwawa
kwa kuchinjwa na kisha mwili wake kuwekwa katika jaba la maji.
Kamanda Sirro alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 31,
mwaka huu, saa nne asubuhi katika eneo la Sinza Shekilango, baada ya
ufuatiliaji wa taarifa ya tukio hilo, ambalo lilitokea Machi 7, mwaka huu, huko
Kibamba.
Aidha, alisema katika mahojiano hayo, mtuhumiwa alikiri
kufanya mauaji ya mwanamke huyo na kueleza kuwa, sababu kubwa ilikuwa ni wivu wa
mapenzi baada ya kumfumania akiwa chumbani na mwanaume mwingine.
Alisema mtuhumiwa huyo aliwatumia ndugu wa marehemu ujumbe
mfupi wa maandishi kwa kutumia namba ya simu ya marehemu mke wake, ukieleza
kuwa “Nendeni mkachukue maiti ya ndugu yenu itaozea ndani”.
Mbali na hilo, Machi 8, mwaka huu, saa mbili usiku katika maeneo
ya Upanga, mtaa wa Charambe, raia watatu wa kigeni kutoka Afrika Kusini na
Serbia, walikamatwa wakiwa na pembe mbili za ndovu zenye uzito wa kilogramu 45.
Kamanda Sirro alisema watu hao walikamatwa baada ya raia wema
kutoa taarifa kwamba, kuna wafanyabiashara wawili wa Afrika Kusini huku mmoja
akitokea Serbia, wanahusika na dawa za kulevya.
Alisema baada ya kupewa
taarifa hizo na kufanyiwa upekuzi, hawakupatikana na dawa hizo, badala yake walipatikana
na pembe hizo za ndovu na kwamba, upelelezi kuhusu shauri hilo unaendelea.
No comments:
Post a Comment