Saturday 21 October 2017

MAMBO YALIYOMPA WAKATI MGUMU MWALIMU NYERERE KATIKA UONGOZI WAKE






 Na Pius  Msekwa                                                        

HUU ni mwaka wa 18 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipomaliza muda wa  maisha yake ya hapa Duniani. Kama ilivyo kawaida, maadhimisho haya huwa yanatupatia fursa ya kujikumbusha juu ya uongozi wake, ikiwa ni njia mojawapo ya kumuenzi na kuendeleza mafunzo mazuri yanayotokana na uadilifu wa uongozi wake kwa manufaa ya vizazi vipya vya viongozi wa nchi yetu. 

Katika Makala hii, nitajikita zaidi katika kueleza baadhi ya mambo, ambayo yalimpa Mwalimu Nyerere wakati mgumu sana katika kuyafanyia maamuzi wakati wa uongozi na utawala wake.   
                                                                                                                                                                  Ni vizuri pia izingatiwe kwamba, ugumu aliokuwa akiupata, ulikuwa unasababishwa na imani yake  ilivyokuwa  ya dhati  kuhusu mambo husika, kama nitakavyoeleza.
Wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alisifiwa na wengi kwa kuwa ni mtu anayefuata misingi katika maamuzi yake na katika vitendo vyake.  Kwa sababu hiyo, alijulikana kama ‘a man of principles’, kwa lugha ya Kingereza.
Misingi, ambayo aliiiamini kwa dhati. Alikuwa ameiweka katika maandishi  rasmi, tangu na hata kabla hajashika uongozi wa nchi, hususan wakati alipoanza kupigania Uhuru wa nchi yetu mwaka 1954, akitaka kuujulisha ulimwengu kwamba, endapo atafanikiwa kuwa kiongozi wa nchi huru, uongozi wake utajikita katika misingi hiyo.
Misingi yenyewe aliiandika kwanza katika Katiba ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), wakati kilipoundwa Julai, 1954, kwa madhumuni ya kudai na kupigania upatikanaji wa Uhuru wa Tanganyika; kama ifuatavyo:  
IMANI YA TANU.
TANU inaamini :-
(a) Kwamba binadamu wote ni sawa.                                                                                                                                  (b) Kwamba kila mtu anastahili heshima. 
(c) Kwamba kila raia ni sehemu ya Taifa na anayo haki ya kushiriki sawa na wengine katika shughuli za serikali yake.                                                                                                                                                                             (d) Kwamba kila raia anayo haki na uhuru wa kutoa mawazo yake, ya kwenda popote anapotaka, kuamini dini anayotaka na kukutana na watu wengine, ili mradi havunji sharia.
(e) Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata kutoka katika jamii, hifadhi ya maisha yake na ya mali aliyo nayo kwa mujibu wa sheria.                                                                                                                                       (f) Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata malipo ya haki kutokana na kazi yake.
(g) Kwamba raia wote kwa pamoja wanamiliki utajiri wa asili wa nchi hii, ukiwa kama dhamana kwa vizazi vyao.
(h) Kwamba ili kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakwenda sawa, serikali lazima iwe na mamlaka kamili juu ya njia kuu za kukuza uchumi.                                                                                                                   (i) Kwamba ni wajibu wa serikali, ambayo ni watu wenyewe, kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi  ya Taifa, ili kuhakikisha ustawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine, au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine, na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa.

Maamuzi na vitendo vya Mwalimu Nyerere vilijikita katika misingi hii
Kwa hakika,  kama tutakavyojitahidi kuonyesha katika makala hii, maamuzi  mengi ya Mwalimu Nyerere alipokuwa madarakani, pamoja na matendo yake mengi, kwa jumla yalijikita katika kutekeleza imani yake katika mojawapo, au zaidi ya  misingi hiyo.                                                                                                             Mifano michache ifuatayo ni ushahidi tosha wa kuthibitisha jambo hilo:-
(i)          Suala la kuingiza wanawake katika nafasi za uongozi
Mwalimu Nyerere aliamua mapema sana baada ya kushika uongozi kama Rais wa Tanzania, kuanza kutekeleza suala la kuingiza wanawake katika nafasi za uongozi wa nchi. Uamuzi wake huu ulitokana na imani yake kuhusu msingi  kwamba ‘kila raia ni sehemu ya Taifa na anayo haki ya kushiriki sawa na wengine katika shughuli za serikali’. 
Mfano ninaoutoa hapa ni wa mwanamke mmoja akiitwa Bernadeta Kunambi, aliyekuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kushika nafasi ya Mkuu wa Wilaya. Nafikiri  ilikuwa mwaka 1968.
Mteuliwa huyo  akapangiwa kituo chake cha kazi kuwa ni Wilaya ya Morogoro. Wakati wa uteuzi huo, mama huyo alikuwa akiishi Dar es Salaam pamoja na  mume wake, Chifu Patrick Kunambi.  Mama Kunambi alikubali uteuzi huo kwa furaha kabisa na akaondoka kwenda zake Morogoro kufanyakazi. Lakini Bwana Kunambi alikataa katakata  kuhamia Morogoro kumfuata mke wake, kwa jeuri tu kwamba mwanamke aliyeolewa ndiye humfuata mume wake popote anapokwenda kuishi na siyo mume kumfuata mke. 
Baada ya muda, ilibidi Mama Kunambi aeleze shida yake kwa Mwalimu Nyerere, kwamba  kazi hiyo ilikuwa imemletea mgogoro mkubwa wa kifamilia, wa kutenganishwa na mume wake.Hapo ndipo Mwalimu Nyerere alipopata wakati mgumu sana wa kufanya mamuzi katika mazingira ya hali hiyo.
Ni dhahiri kwamba asingependa familia ya Mama Kunambi ipate mgogoro kwa sababu tu ya uteuzi wake huo.  Lakini pia asingependa wanawake walioolewa wakose nafasi ya kuteuliwa kushika madaraka serikalini, kwa sababu tu ya misimamo kama hiyo ya waume zao.
Hatimaye, Mwalimu Nyerere aliamua kwamba, Bernadeta Kunambi ahamishiwe katika Wilaya za Dar es Salaam, ili aweze kuwa karibu na mume mume wake. Tumetoka mbali. Lakinni  siku hizi tatizo la aina hiyo halipo tena.
(II)  Suala la  kulinda heshima ya kila mtu.
Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika,  Mwalimu Nyerere alilazimika kufanya maamuzi ya kutekeleza msingi unaosema ‘kila mtu anastahili heshima’, katika kudhihirisha azma yake ya  kutaka kutekeleza msingi huo kwa vitendo. 
Ilikuwa mapema Januari, 1962, ndani ya mwezi mmoja baada ya kupatikana Uhuru.  Wakati huo, Sheikh Amri Abedi alikuwa ndiyo ametoka kuchaguliwa kuwa Meya wa kwanza Mwafrika wa Jiji la Dar es Salaam. Siku moja, Meya Amri Abedi, akifuatana na kiongozi mwenzake, Jacob Namfua, ambaye naye alikuwa ametoka kuteuliwa kuwa Waziri Mdogo, (ndilo lilikuwa jina la cheo hicho wakati huo. Hivi sasa wanaitwa Naibu Waziri), walikwenda kwenye Hoteli inayoitwa Palm Beach, iliyoko maeneo ya Upanga, Dar es Salaam.  
Kabla ya Uhuru,  Waafrika walikuwa hawaruhusiwi kuingia kupata huduma zozote katika hoteli hiyo. Ilikuwa ni hoteli kwa ajili ya wazungu pekee.  Kwa kudhani kwamba mambo yatakuwa yamebadilika baada ya Uhuru,  Mstahiki Meya na mwenzake wakaenda kupata viburudisho kwenye hoteli hiyo.  Walipofika, walifukuzwa kwa kuambiwa  kwamba, Waafrika walikuwa hawaruhusiwi kuingia hapo. 
Pamoja na Mheshimiwa Amri Abedi kujitambulisha kuwa yeye ndiye Mstahiki Meya wa Dar es Salaam, na kwamba mwenzake ni waziri, bado waliamriwa waondoke hapo.
Habari hizo zilipomfikia Waziri Mkuu Nyerere (kama alivyokuwa wakati huo), alitoa amri ya kuwafukuza nchini wazungu waliokuwa wakiendesha hoteli hiyo na kutakiwa wawe wameondoke ndani ya saa 48. Ulikuwa uamuzi mgumu, lakini Mwalimu Nyerere hakusita hata kidogo kuufanya, ili kulinda  msingi wa ‘kila mtu anastahili heshima;,  ambao aliuamini kwa dhati.  
Kuhusu tukio hilo,  Mwalimu alisema hivi: “Tumepigania Uhuru kwa lengo la kuleta heshima kwa kila mtu anayeishi hapa nchini. Hatuwezi tena kuvumilia ubaguzi na udhalilishaji wa wananchi kama walivyofanyiwa viongozi wetu hawa”.

(ii)          Njama za maadui wa Muungano zilivyompa mfadhaiko
Mwaka 1965, Mwalimu Nyerere alipata wakati mgumu sana wa kufanya uamuzi  katika mazingira yaliyojengwa kwa njama za maadui wa  Muungano wetu. Ilikuwa hivi: 
Siku moja, mawaziri wawili, ambao ni  Oscar Kambona na Kassim Hanga, walikwenda kumwambia Mwalimu Nyerere kwamba, ‘Rais Karume wa Zanzibar amewafukuza watumishi wa kutoka upande wa Tanzania Bara, waliokuwa  wamepelekwa Zanzibar kufanya kazi za Muungano’. Mawaziri hao waliendelea kukoleza taarifa yao hiyo kwa kusema kwamba, ‘hii inadhihirisha kwamba Karume hataki Muungano’.
Taarfa hiyo ilimfadhaisha sana Mwalimu Nyerere, hadi kufikia uamuzi wa kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri, ili kuwaarifu kwamba ‘kwa kuwa Rais Karume hataki Muungano, basi yeye hawezi  kumlazimisha, kwa hiyo amewaita ili kuwajulisha kwamba atalazimika kutangaza kuvunjika kwa Muungano huu”.
Huo ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Mwalimu Nyerere na pia kwa Baraza lake la Mawaziri. Ilikuwa ni bahati njema tu  kwamba, baadhi ya mawaziri walitia shaka kama  Rais Karume kweli alifanya hivyo, na hata kama alifanya hivyo, kama ni sahihi kutafsiri kitendo hicho kwamba ‘Karume hataki Muungano’.  Je,  kama alikuwa na sababu nyingine ?
 Hatimaye, waziri mmoja akatoa wazo kwamba, alikuwa na habari kwamba Mzee Sheikh Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa Afro-Shirazi Party,  alikuwa mjini Dar es Salaam siku hiyo na akapendekeza kwamba mzee aitwe mbele ya kikao hicho, aulizwe kama anazo habari hizo.  Ushauri huo ulikubaliwa, Sheikh Thabit Kombo akaitwa na ndiye aliyeokoa jahazi.
Sheikh Thabiti Komba alisema kwamba,  alikuwa hana habari hizo na kwamba kwa maoni yake, haziwezi kuwa za kweli.Kwa hiyo akaomba apewe mjumbe mmoja wa baraza hilo, wafuatane kwenda Zanzibar kumuuliza Rais Karume juu ya jambo hilo. Mzee Rashid Kawawa aliteuliwa, na baraza likaahirishwa kusubiri majibu ya ujumbe huo. 
Majibu yalikuwa ni kwamba, Rais Karume alikanusha kabisa habari hizo na  kuomba ujumbe huo umhakikishie Mwalimu Nyerere kwamba Karume  ni muumini wa Muungano, na wazo la kuvunja Muungano kamwe haliwezi kutoka kwake.  Hivyo ndivyo shauri hilo gumu  lilivyomalizika kwa usalama.

(iii)        Juhudi za kupambana na dhuluma
Neno  ‘dhuluma’ maana yake ni uonevu, yaani vitendo vinavyokwenda kinyume cha  haki  na usawa wa binadamu, ambayo ni miongoni mwa misingi Mwalimu Nyerere aliyoiamini kwa dhati. Kwa hiyo matukio ya aina hiyo yalipotokea,  yalimpa wakati mgumu na kusababisha pia afanye maamuzi magumu.
Mfano mmoja ni tukio lililotokea katika kituo cha Ilemela, karibu na mji wa Mwanza, wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa amekwishashika madaraka ya kuongoza serikali ya mpito iliyoitwa  serikali ya ‘madaraka ya ndani’ katika kipindi cha kabla ya Uhuru.
Kilichotokea ni kwamba, wakati huo kulikuwa na kodi inayoitwa ‘poll tax’ au ‘kodi ya kichwa’ kwa Kiswahili.  Mamlaka ya Serikali za Mitaa ya eneo hilo ilikuwa imewakamata watu wengi kwa kosa la kutokulipa kodi hiyo na kuwaweka mahabusu katika kituo hicho cha Ilemela.
Kumbe chumba walichowekwa mahabusu hao kilikuwa  kidogo mno kuweza kuhifadhi idadi kubwa ya watu waliofungiwa humo, hasa kwa kuwa walifungiwa kwa kipindi  kirefu cha siku kadhaa, bila kuwajulia hali, uzembe  ambao ulisababisha baadhi yao kufariki kwa kukosa hewa safi ya kutosha.  Hiyo ilikuwa ni dhuluma ya kutisha dhidi ya watu hao.
Taarifa hizo zilipomfikia Mwalimu Nyerere, mara moja alifanya uamuzi mgumu, siyo tu wa  kuamuru  kukamatwa kwa maafisa wote waliohusika katika kufanya uzembe ambao ulisababisha maafa hayo kutokea, bali pia aliamuru kufutwa kabisa kwa kodi hiyo ya kichwa, ili isiendelee kuwa chanzo cha kusababisha maafa kama hyo kutokea tena.
(iv)       Suala la vita dhidi ya majeshi ya Iddi Amin wa Uganda.

Katika nusu ya pili ya mwaka 1978, majeshi ya Iddi Amin, aliyekuwa Rais wa Uganda wakati huo, yalivamia nchi yetu kwa upande wa mkoa wa Kagera (wakati huo ukiitwa Mkoa wa Ziwa Magharibi). Majeshi hayo yalifanya uharibifu mkubwa, pamoja  na wizi wa mali za watu. Pia waliua watu wengi raia wa kawaida katika mkoa huo.  Halafu, Rais Iddi Amin akatangaza kwa jeuri kwamba, sehemu yote hiyo iliyovamiwa na majeshi yake, ‘sasa imemegwa kutoka Tanzania na kwamba   imekuwa sehemu ya nchi ya Uganda’.
Wakati hayo yanatokea, Mwalimu Nyerere alikuwa katika ziara ya mkoa wa Ruvuma. Taarifa za uvamizi huo zilipomfikia, zilimfadhaisha sana. Ilibidi akatishe ziara yake na kurejee Dar es Salaam mara moja,  ili kujipanga vizuri kupambana na udhalimu huo.
Baada ya kutoa maelekeo stahiki kwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alihutubia Taifa  kupitia kikao cha Wazee wa Dar es Salaam, kilichofanyika Diamond Jubilee Hall; ambapo  aliwatangazia  Watanzania uamuzi wake kuhusu sala hilo. Kwa sauti kubwa na muonekano wa kujiamini kabisa, Mwalimu Nyerere alitangaza  uamuzi wake wa kusudio la kumuadhibu vikali Iddi Amin, kwa kutumia maneno  mazito yafuatayo:-  ”Uwezo wa kumpiga tuno, sababu ya kumpiga tunayo, na nia ya kumpiga tunayo. Tunataka dunia ituelewe hivyo.’
 Jeshi letu liliingia kazini mara moja na baada ya muda usiokuwa mrefu, lilifanikiwa kuwafukuza wanajeshi wa Iddi Amin kutoka katika ardhi ya Tanzania na kuwarudisha nchini  kwao.

(v)        Uamuzi mgumu wa kuruhusu jeshi letu kuingia Uganda.

Lakini uamuzi uliokuwa mgumu zaidi kwa Mwalimu Nyerere,  na ambao kwa hakika ulisumbua sana  akili yake katika kuufikia, ni ule wa kuruhusu Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuvuka mpaka na kuingia Uganda,  kwa lengo la ‘kwenda kumpa Iddi Amin kipigo cha mwisho’. Ugumu wa uamuzi wa kufanya hivyo ulitokana na ushauri wa aina mbili unaopingana, aliokuwa akipewa na Ma-Rais wenzake wa Afrika kwa upande mmoja na ushauri wa JWTZ kwa upande mwingine. 
Kwa upande wao, Ma-Rais wa Afrika walikuwa wakimshauri Mwalimu Nyerere kwamba, asiruhusu jeshi lake kuvuka mpaka na kuingia Uganda, kwani akifanya hivyo, walimwambia, na yeye ‘atakuwa amefanya kosa lile lile la  kuwa mvamizi wa nchi jirani  ya Uganda’. Yaani atakuwa amefanya kosa kama lile la Iddi Amin la kuvamia Tanzania. Ma-Rais wenzake hao  walimshauri kwamba ‘kwa kuwa alikuwa tayari ameyafukuza majeshi ya Uganda kutoka katika ardhi ya Tanzania,  huo uwe ndio mwisho wa mapambano hayo’.
Lakini JWTZ kwa upande wake, walimshauri Mwalimu Nyerere kwamba, kuishia mpakani haliwezi kuwa suluhisho la kudumu la mapambano na Iddi Amin. Walisema, ‘Itabidi jeshi likae hapo mpakani kwa  muda mrefu usiojulikana, kwa ajili ya kuzuia majeshi ya Uganda yasiingie tena nchini’.
Kwa hiyo, JWTZ wakamshauri Mwalimu Nyerere kwamba, ‘turuhusu sisi twende huko Kampala kwake,  tukampe Iddi Amin kipigo cha mwisho’. Sisi tuliokuwa karibu na Rais Nyerere, tunakumbuka jinsi aliyoteseka mno kimawazo, katika kufikia uamuzi kuhusu akubali ushauri upi.
Mateso  aliyopata yanadhihirishwa na jinsi siku moja alivyoamua kukubaliana na ushauri wa Ma-Rais wenzake wa Afrika kwamba, asiruhusu majeshi yake kuvuka mpaka na kuingia Uganda. Lakini kesho yake akabadili uamuzi huo, akaamua kuruhusu JWTZ wavuke mpaka na kwenda kumuadhibu Iddi Amin ndani ya nchi yake.  Mambo yenyewe yalikuwa hivi:
 Ilikuwa ni siku moja ya Jumamosi (sikumbuki tarehe), ndipo  Mwalimu Nyerere alipofanya uamuzi wa kukubaliana na Ma-Rais wenzake wa Afrika, wa kuzuia JWTZ wasivuke mpaka kwenda Uganda, na papo hapo akamtuma Makamu wa Rais,  Aboud Jumbe, kwenda kuwatangazia wanajeshi uamuzi huo. 
Makamu wa Rais  huyo kweli akaondoka asubuhi ya kesho yake Jumapili, kwenda Bukoba kuwasilisha ujumbe huo. Lakini kumbe huku nyuma, Mwalimu Nyerere  akagundua kwamba, alikuwa amefanya uamuzi usiofaa kwa manufaa ya nchi.  Kwa hiyo akatuma taarifa haraka ya kumzuia Makamu wa Rais,  asiwaambie  wanajeshi yale maneno aliyokuwa amemtuma kuwaambia.
Badala yake aliondoka yeye mwenyewe kwenda Bukoba, mpakani walikokuwa wanajeshi wetu, kuwapatia idhini rasmi ya kuvuka mpaka na kuingia Uganda, kazi ambayo waliifanya kuanzia usiku wa siku hiyo hiyo.Matokeo yake  sote  tunayajua. Iddi Amin alilazimika kuikimbia nchi yake na kwenda Arabuni kuishi kama mkimbizi, hadi mwisho wa maisha yake.                                                                                                 Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya mrehemu Mwalimu Nyerere mahali pema.

                                                                     

No comments:

Post a Comment