UPANDE wa jamhuri katika kesi inayowakabili vigogo
wa Kampuni ya IPTL, umeieleza mahakama kwamba, imetekeleza amri zake, ambapo
mshitakiwa Harbinder Sethi, amepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na
kufanyiwa vipimo.
Umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa
mshitakiwa Sethi alipelekwa Muhimbili, juzi, ambapo kafanyiwa vipimo na
wanasubiri ripoti itakayotolewa wiki ijayo.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), Leonard Swai, alieleza hayo jana, mahakamani hapo, mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati shauri hilo, linalomkabili Sethi na James
Rugemarila, lilipopelekwa kwa kutajwa.
Swai alidai upelelezi wa shauri hilo unaendelea na
kwamba, wametekeleza amri ya mahakama, ambapo Sethi alipelekwa Muhimbili juzi,
ambako alifanyiwa vipimo na ripoti itatoka wiki ijayo.
Kwa upande wa Wakili wa Rugemarila, Respicius Didas
alidai kuna suala la ucheleweshaji wa
upelelezi kwani washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, mwaka huu,
kwa mashitaka ambayo yanadaiwa kutendeka mwaka 2013.
Alidai washitakiwa wapo mahabusu na upande wa
jamhuri kila kesi ikitajwa, wanaeleza upelelezi haujakamilika wakati wateja wao
kwa kuendelea kukaa ndani kuna athari.
Akijibu hoja hizo, Wakili Swai alidai kuchelewa kwa
upelelezi kunatokana na makosa ya kughushi, ambayo upelelezi wake huchukua muda
mrefu, ambapo aliahidi kukamilisha.
Sethi na Rugemarila
wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ikiwa na mashitaka 12, yakiwemo
ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa
nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kutakatisha
fedha na kuisababisha hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60 na sh.
309,461,300,158.27.
No comments:
Post a Comment