Friday 13 October 2017

SERIKALI YAITAKA TUCTA IACHE SIASA



SERIKALI imesema madai yaliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), kuhusu serikali kushindwa kutekeleza ahadi ya kupandisha mishahara ya watumishi wa umma, hayana ukweli wowote na ni ya kupuuzwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, alisema Rais Dk. John Magufuli hakuwahi kuzungumzia kukataa kutekeleza ongezeko la mwaka la mishahara ya watumishi wa umma.

Dk. Abbas alisema alichozungumza Rais Magufuli wakati akifungua mkutano mkuu wa ALAT, ni kujibu hoja mahsusi ya posho za madiwani, ambao walitaka kuongezwa posho kutoka sh. 350,00 hadi sh. 80,000, sawa na ongezeko la asilimia 150.

"Ni hatari kwa chama cha wafanyakazi chenye hadhi ya TUCTA, kufanyiakazi uongo unaoenezwa mitandaoni na vyama vya siasa visivyo na ajenda yoyote yenye maslahi kwa umma na kuifanya kuwa yao.

"TUCTA wanazijua taratibu stahiki za kupata uhakika wa jambo lolote kutoka serikalini. Wamechagua kutozifuata taratibu hizo na zaidi kutoamini hata ushahidi wa serikali, lakini wanawaamini CHADEMA," alisema Dk. Abbas.

Tamko hilo limekuja baada ya TUCTA kuilaani serikali, kutokana na kile ilichodai kutotekelezwa ahadi za Rais Magufuli, alizozitoa wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi, mwaka huu.

Katika madai yao hayo, TUCTA pia imelalamikia baadhi ya wafanyakazi wenye elimu ya darasa la saba, kuondolewa kinyume na waraka wa mwaka 2004. Pia, walizungumzia kuwaonea huruma walioghushi vyeti kwa madai kuwa, wamefukuzwa kama mbwa.

"Dai hili nalo halina msingi kwa sababu msimamo wa serikali wa kwa nini walioghushi vyeti hawakuwa na sifa za kuendelea kuwepo katika utumishi wa umma, ulishaelezwa na sote tulizielewa. Kama kuna mtu alionewa nafasi ya rufaa ilikuwepo na wapo walioitumia vizuri,"alisema Dk. Abbas.

Aliongeza: "Tunasisitiza tena ni vyema chama hiki kikajitathmini mwenendo wake. Rais aliahidi Mei, mwaka huu, mbele yao kuwa asingepandisha wakati ule kwa kuwa uhakiki wa wafanyakazi ulikuwa unaendelea na akaahidi utakapomalizika tu wote wenye haki yao wataipata."

Dk. Abbas alisema Rais Magufuli aliisimamia ahadi yake hiyo na kuhakikisha zimetengwa sh. bilioni 487.7, kwa ajili ya wale watakaopanda madaraja mwaka huu wa fedha baada ya uhakiki kumalizika.

Aidha, alisema serikali imetenga sh. bilioni 35.2, ambazo ni malimbikizo ya nyuma ya mishahara.

"Katika robo hii ya kwanza, tayari serikali imekwishalipa sh. milioni 531.4, ikiwemo waliopanda ngazi kwa namna mbalimbali na pia sh. milioni 739.3, zimelipwa kwa wastaafu 108, ikiwa ni sehemu ya malimbikizo yao ya nyuma ya kupanda madaraja,"alisema Dk. Abbas. 

"Masuala haya yote yameingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu kama tulivyoainisha hapo awali na ndio kwanza tumeanza kuitekeleza na mawaziri wa sekta husika walishasema hadharani, kisekta, madai gani na gani yametengewa fedha.

"Tayari serikali imeshaanza kulipa madai haya, tofauti na kauli ya TUCTA. Kiasi cha sh. bilioni 70.4, kimeshalipwa kwa ajili ya madai ya wafanyakazi, sehemu kubwa ikiwa ni madai yasiyo ya mishahara kwa mwaka 2016/2017. Katika robo hii ya kwanza tu, yaani Julai-Septemba, 2017, sh. bilioni 37.4 zimeshalipwa.

"Kwa takwimu hizi, madai ya TUCTA yanaanguka. Tunatumia fursa hii kuwaonya wale wote ambao wanadhani hizi ni nyakati za kufanya propaganda katika masuala ya msingi kitaifa kwamba, wajitafakari upya.

"Serikali itaanza kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale watakaoendeleza mtindo wa kutoa taarifa za uongo zinazoihusu Serikali kwa lengo la kupotosha umma, kuzua taharuki au kuifanya Serikali ichukiwe na wananchi wake bila sababu.

"Serikali yetu imetunga sheria kadhaa kuwahakikishia wananchi, ikiwemo TUCTA, haki na mifumo rasmi ya kupata habari sahihi na taarifa za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, 2016 na Sheria ya Kupata Taarifa, 2015. Watumie mifumo hiyo kuliko kuokoteza hoja," alisema Dk. Abbas.

No comments:

Post a Comment