Friday 13 October 2017

MAPATO SEKTA YA UTALII KUFIKIA DOLA BILIONI 16 MWAKA 2025


Na. Fatma Salum-MAELEZO

Sekta ya utalii nchini inakadiriwa kuongeza mapato kufikia dola bilioni 16 ifikapo mwaka 2025 iwapo itawekewa mikakati madhubuti ya kuboresha sekta hiyo ikiwemo miundombinu itakayorahisisha watalii kufika kwenye vivutio.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan aliyasema hayo leo wakati akifungua Maonesho ya 3 ya Kimataifa ya Utalii (Swahili International Tourism Expo) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
“Kwa mujibu wa ripoti ya 6 ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania imeonesha kuwa ifikapo mwaka 2025 mapato kutokana na sekta ya utalii yataongezeka kufikia dola za kimarekani bilioni 16, hivyo tunajitahidi kuboresha sekta hiyo ili tuweze kufikia makadirio hayo,” alisema Mh.Samia.
Alieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vivutio vingi duniani na idadi ya watalii inaendelea kuongezeka ambapo kwa mwaka 2016 ilifika zaidi ya watalii 1,284,279 ambao walifika nchini kujionea vivutio mbalimbali na waliingiza nchini takriban dola bilioni 2.1.
Alisema kuwa Serikali inatambua mchango wa sekta ya utalii katika kukuza uchumi hivyo maonesho hayo ni muhimu kwa wadau wa sekta hiyo kujadili fursa na changamoto zilizopo pamoja na kubadilishana uzoefu ili kuboresha kwenye maeneo yao.
“Tutumie maonesho haya kujitangaza kote duniani ili tuweze kuongeza idadi ya watalii na kukuza uchumi wa Tanzania na bara letu la Afrika kwa ujumla,” alibainisha Makamu wa rais.
Pia alisema kuwa kati ya mwaka 2007 na 2017 utalii wa ndani ya Afrika umekua kutoka asilimia 34 hadi asilimia 44 ya watalii wote wa kiafrika wanaotembelea nchi za ndani ya bara hili.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Hamisi Kigwangalla aliwapongeza waandaaji wa maonesho hayo wakiongozwa na Bodi ya Utalii Tanzania na kuwataka kutumia fursa hiyo kujitangaza zaidi.
Maonesho hayo ya Kimataifa ya Utalii yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo wafanyabiashara na watoa huduma kutoka nchi za Afrika Kusini, Nigeria, Morocco, Kenya, Uganda, Rwanda na Mauritius.

No comments:

Post a Comment