Friday, 13 October 2017
CCM YASHUSHA RUNGU ZITO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kugongelea msumari wa moto kwa kusema kuwa, hakitakuwa na msamaha kwa watendaji na vikao vilivyokiuka kanuni na waraka uliozuia watumishi wa serikali kuwania uongozi ndani ya Chama.
Kimesema hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa taarifa za vikao vya uteuzi vya ngazi za wilaya na mikoa, kuteua watumishi wa serikali kugombea uongozi ndani ya Chama, kinyume na utaratibu ulioelekezwa na waraka uliotolewa hivi karibuni.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, alisema hayo jana, Dar es Salaam, alipozungumza na Uhuru, kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Chama na jumuiya kwa ngazi za wilaya, uliofanyika hivi karibuni katika maeneo mbali mbali nchini.
Alisema taarifa za awali zinaonyesha kuna wilaya na mikoa iliyokiuka waraka huo na baadhi wamekuwa wakifafanua kwamba, nafasi zilizozuiliwa ni zile za muda wote, jambo ambalo ni upotoshaji wa makusudi.
“Waraka umeelekeza bayana kwamba, watumishi wa serikali hawaruhusiwi kuwania uongozi ndani ya Chama. Lakini baadhi ya watendaji kwa kushirikiana na wajumbe wengine wa vikao vya uteuzi,wamewapitisha na wengine wameshinda nafasi mbalimbali.
"Ni vema watumishi wa serikali waliochaguliwa kwenye nafasi mbalimbali, waamue kuchagua siasa ama ajira serikalini,vinginevyo wanapaswa kujiondoa kwenye nafasi hizo na watendaji wa CCM wasimamie suala hilo kabla hatua hazijachukuliwa,”alisema.
Alisema ukiukwaji huo wa kanuni na maelekezo ya Chama ni uvunjaji wa kanuni za maadili na uongozi, hivyo watendaji wanapaswa kuhakikisha wanachukua hatua mapema, badala ya kusubiri kuchukuliwa hatua na vikao vya juu.
Mangula alisema kanuni za uongozi na maadili zinaeleza bayana vikao vina wajibu wa kusimamia na kufuatilia mwenendo wa wanachama na viongozi na kufanya uamuzi sahihi.
Kwa mujibu wa kifungu cha 5 (iii):”Kikao chenye wajibu wa kikatiba wa kusimamia tabia na mwenendo wa wanachama na viongozi endapo kinachelea kuwachukulia hatua, kitakuwa kimefanya kosa la kimaadili.”
Mangula alisema msingi wa waraka huo ni mpana mno na unalenga maslahi mapana ya Chama, hivyo hakuna mjadala, kinachotakiwa ni utekelezwe na pale ambapo kuna ukiukwaji, walioshinda wataenguliwa kama hawatajiengua wenyewe.
Katika hatua nyingine, Mangula alisema taarifa za uchaguzi wa ngazi za wilaya, zinaonyesha kwamba, yapo maeneo ambako vitendo vya rushwa viliendelea kufanyika licha ya makatazo yote yaliyotolewa katika nyakati mbalimbali.
Alisema kutokana na hali hiyo, Chama kitalazimika kufuta matokeo ya uchaguzi katika baadhi ya wilaya baada ya kujiridhisha kwamba, kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni kwa kuwa suala la rushwa ni kinyume na maadili ya viongozi wa CCM.
“Walidhani kwamba, maagizo ya Mwenyekiti na Rais Dk. John Magufuli juu ya rushwa ni utani. Watashuhudia matokeo yakifutwa na baadhi yao kuondolewa kwenye orodha ya wagombea wa nafasi husika. Tunaposema mageuzi ndani ya CCM, tunamaanisha hivyo, wanachama wabadilike,” alisema Mangula.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema, mwanachama akijihusisha na rushwa, anavunja kanuni za maadili ya uongozi na maana nyingine anazuia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo, imeweka msimamo mkali katika eneo hilo.
Katika Ibara ya 12, CCM imeahidi kwamba: 'Itazielekeza serikali zake kuendeleza mapambano dhidi ya adui rushwa kwa nguvu zake zote na kuendelea kuziba mianya ya rushwa katika taasisi za umma na kuchukua hatua kali na za haraka kwa wale wote watakaobainika kuendeleza rushwa.'
Alisema katika ibara ya 13 ya Ilani CCM, inasisitiza kwamba, pamoja na kupambana na tatizo la rushwa, serikali pia zitatakiwa kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka, ukiukwaji wa maadili ya uongozi na utumishji wa umma.
Mangula alisema kutokana na ahadi hizo, CCM haitafanya mzaha kwa mwanachama ama kiongozi anayendekeza vitendo vya rushwa kwa makusudi.
Mkakati wa CCM kudhibiti rushwa, ulianza katika uchaguzi wa mashina na wakati wa uchaguzi wa ngazi ya kata, ambapo CCM ilifuta matokeo katika kata zaidi ya 40 na kutangaza upya uchaguzi ili kukomesha vitendo hivyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment