KESI ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Dk.
John Magufuli, inayomkabili mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee (CHADEMA),
imepangwa kuanza kusikilizwa, Novemba 8, mwaka huu.
Hatua hiyo inatokana na upande wa jamhuri katika
kesi hiyo iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilimsomea maelezo ya
awali.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali, Leonard Chalo akishirikiana na Wakili wa Serikali,
Janeth Magoho, walimsomea Halima maelezo ya awali.
Kabla ya kusomewa maelezo, Halima alikubushwa
shitaka linalomkabili ambalo alikana kulitenda.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Halima anadaiwa
Julai 3, mwaka huu, makao makuu ya CHADEMA, yaliyoko maeneo ya Ufipa, wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam, alitoa lugha ya matusi dhidi ya Rais Magufuli.
Halima anadaiwa kutamka nanukuu; 'anaongea hovyo
hovyo anatakiwa afunge breki,' jambo ambalo lingesababisha uvunjifu wa amani.
Akimsomea maelezo ya awali, Janeth alidai Halima
(39), mbunge na mkazi wa Makongo, Kinondoni, Dar es Salaam.
Alidai Julai 3, mwaka huu, mshitakiwa alikuwa
maeneo ya ofisi za CHADEMA, zilizoko
Ufipa, Dar es Salaam, ambapo akiwa hapo alitoa maneno hayo ya kejeli kwa
Rais Magufuli.
Janeth alidai kutokana na maneno hayo, Julai 4,
mwaka huu, mshitakiwa alikamatwa Kibamba, wilayani Kinondoni, na kuhojiwa
ambapo alikubali kusema maneno hayo na baada ya utaratibu wa polisi kukamilika
alipelekwa mahakamani.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, mshitakiwa huyo
ambaye anatetewa na wakili Hekima Mwesigwa, alikubali taarifa zake binafsi,
Julai 3, mwaka huu alikuwa makao makuu ya CHADEMA na kukamatwa kwake huku
akikana maelezo mengine.
Hakimu Victoria aliahirisha shauri hilo hadi
Novemba 8, mwaka huu, kwa kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa jamhuri
na dhamana ya mshitakiwa inaendelea.
No comments:
Post a Comment