BAADHI ya Wasomi na Wanasiasa nchini, wamemwelezea
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba alikuwa kiongozi
aliyeasisi uzalendo, misingi ya uongozi bora na uadilifu
Wamesema misingi hiyo, haijawahi kutekelezwa
kikamilifu kwa vitendo na yeyote, isipokuwa Rais Dk. John Magufuli.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
William Ole Nasha, akifungua kongamano la maadhimisho ya Kumbukizi ya Mwalimu
Nyerere, Dar es Salaam, jana, alisema kumekuwa na mmomonyoko wa maadili kwenye
jamii.
“Rais Magufuli amerejesha kwa kiasi kikubwa nidhamu
katika misingi aliyoiweka Mwalimu Nyerere, hivyo ni wajibu wa kila mmoja katika
nafasi yake, kumuunga mkono,” alisema.
Maadhimisho hayo, yalifanyika katika Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni, naibu waziri huyo alikipongeza chuo
hicho kwa kurejesha mitaala ya mafunzo ya uongozi, maadili na utawala bora.
“Chuo kinayo nafasi nzuri ya kutoa viongozi wengi
waadilifu katika misingi aliyoiasisi Mwalimu Nyerere, hivyo endeleeni kutoa
mafunzo kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, watakaosimamia uzalendo,”
alisema.
Vile vile, aliitaka jamii kuhakikisha inawaokoa watoto
kutoka katika wimbi la mitandao ya kijamii ambamo wanajifunza mambo yasiyofaa,
badala yake watafiti, kusoma na kufuata misingi ya Baba wa Taifa.
Alisema, anaamini ikiwekwa mikakati imara, vijana
watapata malezi na makuzi ya kimaadili, baadaye kushika uongozi katika ngazi za
juu.
Alihimiza kuunga mkono sera ya kukuza uchumi wa
viwanda kwa kuwa Mwalimu Nyerere alihimiza kuendeleza viwanda vya ndani ikiwa
ni njia ya kujinasua na mabepari.
Akitoa mada, Mzee Samuel Kasori, alisema
Mwalimu Nyerere alihimiza matumizi mazuri ya raslimali, masoko ikiwemo
kutumia wataalamu kuondoa umasikini.
“Lakini baada ya kuondoka, watu wanafanya mambo ya
hovyo kila mtu anavyojisikia ili kujinufaisha, leo nawatia moyo Watanzania
watekeleze nia ya rais Magufuli kwani ndiye anayeendeleza misingi hiyo,”
alisema.
Alisema, inapaswa kuwekwa sera nzuri ya ardhi, kwa
kuwa mwaka 1958, kabla ya Uhuruardhi isichezewe kwa kuwa ni mali ya Watanzania
wote.
“Uzalendo, uadilifu na utaifa si kuvaa nembo au
kupamba bendera ofisini kwenye magari na nyumbani huku mnafanya uozo, dhuluma
na hujuma kwa Watanzania wenzenu, bali ni kutekeleza kwa vitendo,” alisema.
Mzee Kasori alinukuu kauli iliyosemwa na Mwalimu
Nyerere mwaka 1959 kuwa Afrika inaonewa kwa kufanywa bara la kuuzwa nje,
kutokana na kunyonywa.
Msajili wa Hazina, Dk. Oswald Mashindano, akitoa
mada alisema Rais Magufuli anatekeleza ajenda ya uchumi wa viwanda iliyoasisiwa
na Mwalimu Nyerere, dhamira ilikuwa kulifanya taifa lijitegemee kiuchumi.
Alisisitiza kuchunguza changamoto zilizoangusha
viwanda vya awali, ili kuziepuka na taifa kusonga mbele.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Profesa Mark
Mwandosya, alisema wanayo kazi kubwa ya kuhakikisha wanarudisha misingi
iliyowekwa na Baba awa Taifa, kwa kuwa misingi yake ina umuhimu hususan kipindi
hiki cha awamu ya tano.
Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda, alisema
ukweli utabaki pale pale kuwa misingi aliyoiweka Baba wa Taifa inafaa na
kuopaswa kurithishwa kwa vizazi vyote.
Anasema Nyerere alikuwa kama mtabiri kwani yote
aliyoyasema ndiyo tunayohangaika nayo hivi sasa, hivyo si ya kupuuzwa.
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Shedrack anasema
watahakikishja wanapika viongozi watakaowafikisha Watanzania wanapopataka.
No comments:
Post a Comment