SERIKALI baada ya kupata mafanikio makubwa katika
uhakiki wa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi, sasa inahamia kwa wale
waliodanganya umri wa kuzaliwa ili wasistaafu mapema.
Imesema watumishi wa umma 40,000 nchini, wamedanganya
umri wa kuzaliwa kwa kutoa taarifa tofauti kwa mwajiri na kwenye Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Kubainika kwa watumishi hao, kunafuatiwa na tamko
la Rais Dk.John Magufuli, alilolitoa Mei Mosi, mwaka huu, wakati wa maadhimisho
ya siku ya wafanyakazi duniani, yaliyofanyika mkoani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Dk. Magufuli, alisema baada ya kukamilika kwa
uhakiki wa wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki, kuwa kwa sasa wamejipanga
kufanya uhakiki wa wafanyakazi waliobadilisha umri wao.
Alisema, kuna watu ambao ni wazee kwenye ofisi za
umma, lakini hawataki kustaafu.
Alisema, mtu wa namna hiyo, hana tofauti na
mfanyakazi hewa kwa sababu hataki kutoka kazini ili wengine nao waajiriwe.
Rais alisema, hao ambao hawataki kuachia ofisi,
lakini ni wazee dawa yao inachunguzwa.
Akizungumzia kuhusu watumishi waliodanyanga umri
baada ya kuulizwa wakati wa makabidhiano ya wizara kati yake mtangulizi wake,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angella Kairuki na Waziri mpya, George Mkuchika.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema kuna watumishi
ambao walighushi umri wakati wanaajiriwa na walivyokwenda kwa ajili ya kupatiwa
vitambulisho vya NIDA, walitaja umri mwingine tofauti na waliotaja serikalini.
“Sijui wamebadilisha kwenda kwenye umri halali au
kwa kughushi, takribani watumishi wa umma 40,000 ambao taarifa zao katika mfumo
wanaonekana umri wao wameubadilisha, katika miaka ya hivi karibuni,” alisema.
Alisema, serikani walijaza umri ambao sio sahihi
ambapo NIDA walijaza umri sahihi,”alisema.
Dk. Ndumbaro, alisema walipokwenda NIDA
kulinganisha taarifa zao ambao zipo kwenye mfumo, walibaini kuna baadhi yao
wana umri wa aina mbili tofauti.
Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, wanaendelea kusoma
taarifa zao na ni wengi waliobadilisha umri.
Alisema taarifa hizo wanazo na wanazifanyia kazi
kadiri muda itakavyokwenda ili watumishi hao waweze kurekebisha umri wao na
kubakia na ule ambao ni halali.
Kwa upande wake, Angellah ambaye ni Waziri wa
Madini, alisema katika wizara hiyo alikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo
uhakiki wa vyeti ambapo kazi yake haikuwa nyepesi.
Waziri huyo alisema kuna maofisa utumishi wengine
hawakuwa waaminifu katika mchakato huo, walidiriki kuwasaidia watu kuficha sifa
zao.
“Naamini kama wapo masalia na kwa timu iliyopo
itafanyiwa kazi na wataondolewa,”alisema.
Kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, Angellah
alisema kuna idadi kubwa ikilinganishwa na mapato yanayopatikana
serikali.
Alisema katika mwaka wa fedha, zimetengwa fedha kwa
ajili ya kuwapandisha watumishi 193,666 katika madaraja na kinachosubiriwa ni
utekelezaji wake.
Naye, Mkuchika alimpongeza waziri mwenzake kwa kazi
kubwa aliyoifanya katika wizara hiyo na kusema huo ni mtaji na amemrahisishia
sehemu ya kuanza na kupita.
“Umeeleza kulikuwa na operesheni ya kuwaondoa
watumishi hewa na umefanya kazi kubwa ya kujua idadi hasa ya watumishi waliopo.
“Nafikiri ni busara ya Rais, kabla ya kuwapandisha
watu vyeo na mishahara, je watu hao wapo na ni watumishi halali, kazi hiyo wewe
umeifanya.
“Sasa ni muda muafaka tutakaka na kuangalia jambo
hilo, baada ya kujiridhisha, msingi tayari umewekwa na kufanikiwa kuwaondoa na
kurejesha nidhamu ya watumishi na mambo mengine,”alisema.
Mkuchika alisema zamani watu walikuwa na heshima
ukiambiwa kuwa wewe ni mtumishi wa serikali kuliko mtumishi mwingine katika
taasisi binafsi na walitambulika kutokana na nidhamu waliyokuwa nayo.
Waziri huyo alisema wataendeleza pale alipoishia na
zaidi ni kuongeza kasi ya kufanya kazi kwa maadili ya utumishi wa umma na
mapambano dhidhi ya rushwa.
Pia, Mkuchika aliiagiza sehemu zitazokuwa
zinafanya makongamano na semina,
wataalamu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana (TAKUKURU), waalikwe kwa ajili ya
kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala
ya rushwa.
“Ukienda katika nchi zilizofanikiwa katika rushwa,
Norway na Sweden, wananchi wanafahamu rushwa ni adui wa haki, hata muombaji wa
rushwa anaogopa kwa sababu wanajua.
“Watanzania wangapi wanajua ni wachache, mtu
anaombwa rushwa, sijui hospitalini, anatafuta vipimo, ukitaka vipimo vyake viende
haraka lete kiasi fulani, anatoa masikini yule hana anaumia,”alisema.
No comments:
Post a Comment