Saturday 21 October 2017

WASOMI WASEMA HAKUNA KAMA MWALIMU NYERERE


WAKATI Watanzania wakiadhimisha miaka18, tangu  Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alipofariki dunia nchini Uingereza, baadhi ya wasomi nchini wamemuelezea kuwa ni mfano wa kuigwa na kizazi cha sasa katika mazingira yaliyopo.
Wakizungumza na Uhuru kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam wiki hii, kuhusu maisha na uongozi wa Mwalimu Nyerere, wasomi hao wamesema Watanzania wanapaswa kumuenzi kiongozi huyo kwa vitendo.
Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Benson Bana, anasema wananchi wanatakiwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufanya kazi bidii kama alivyofanya kipindi cha utawala wake.
Profesa Bana anamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa kukerwa na hali ya umaskini, hivyo kupambana nao kwa vitendo hatua kwa hatua, katika kipindi cha miaka 24 ya uongozi wake.
 “Tunapaswa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo. Mwalimu alikuwa mtu wa vitendo. Alichokisema alikifanya kwa vitendo na watu tulioishi katika utawala wake tuliona.
“Kama kuandika aliyofanya, ni mengi. Kama ni maneno ya kumsifia, tumesema mengi, lakini bila ya kuyatenda itakuwa kazi bure,”anasema.
Kwa mujibu wa Profesa Bana, Rais Dk. John Magufuli, ameonyesha njia ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo, hivyo taswira ya vitendo vyake iigwe na wananchi kwa wakati huu.
Anasema  viongozi wa serikali wa ngazi zote, washirikiane na wananchi katika shughuli za ujenzi wa taifa, badala ya kuwa waelekezaji pekee pasipo kufanya lolote.
“Tunataka viongozi wetu wamuige Mwalimu. Mathalani majengo yakijengwa, nao tuwaone katika miradi moja kwa moja wakishirikiana na wananchi, kama alivyokuwa anafanya Mwalimu. Hii ndiyo namna nzuri ya kumuenzi,”anasema.
Akizungumzia maadui watatu ujinga, maradhi na umasikini, ambao Mwalimu Nyerere aliamua kupambana nao kwa vitendo, anasema taifa kwa sasa  linatakiwa kutafakari njia muafaka za kuwatokomeza.
Mhadhiri huyo mwandamizi anasema, juhudi za serikali na watu binafsi zinahitajika katika kuhakikisha maadui hao hawaendelei kuwepo nchini.
Profesa Bana anasema kwa sasa uzalendo kwa nchi umeshuka kutokana na tofauti ya vyama vya siasa, hali inayosababisha baadhi ya watu kuihujumu nchi kwa sababu ya maslahi yao binafsi.
Anasema wananchi wanapaswa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha wanadumisha amani na umoja nchini, kwa ajili ya maendeleo ya nchi, badala ya kuendekeza tofauti za itikadi za  kisiasa.
Profesa Mohammed Bakari, Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa UDSM, anasema anamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa msingi mkubwa wa kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Profesa Bakari anasema, hali hiyo imeifanya nchi kuwa tulivu na wananchi kuishi bila ya ubaguzi, licha ya kutofautiana  sehemu wanazotoka.
“Kitu kikubwa kwangu ni kwamba, aliasisi umoja na kuulinda. Tunayo makabila mengi, lakini yote haya aliyaunganisha na kuishi pamoja bila ya kupigana.
“Hili ni jambo kubwa la kumpongeza. Wenzetu wa nchi  jirani mpaka leo bado masuala ya ukabilia yanawatatiza , lakini Mwalimu aliweza na sisi tunaendeleza aliyotuachia,”anasema.
Anashauri wananchi kumuenzi kwa kuhakikisha wanadumisha amani, badala ya kufanya vitendo vitakavyosababisha kuvurugika kwa umoja aliouacha.
Profesa Bakari anawaasa viongozi wa serikali, kuhakikisha wanalinda katiba ya nchi kwa kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere kwani ndiyo dira ya taifa.
“Aliheshimu katiba ya nchi ya mwaka 1977 na ile ya mwaka 1962. Alikuwa anaendesha nchi kwa utawala wa sheria, hakuwa dikteta katika maamuzi yake ingawa angeweza kufanya hivyo.
“Alikuwa mtu wa watu, hakujikweza na kujiona kuwa ni bora kuliko wananchi wake, hivyo viongozi wa sasa wanatakiwa kujifunza kwake,”anasema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Hisabati ya Chuo cha UDSM, Dk. Sylvester Rugeihyamu, anasema viongozi wa sasa wanaweza kumuenzi kwa kutoa huduma  za jamii, bila ya malipo kama alivyofanya katika utawala wake.
Kwa mujibu wa Dk. Rugeihyamu, enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, huduma za shule na hospitali zilitolewa bila malipo, ingawa uchumi wa nchi ulikuwa wa chini.
“Viongozi wetu wa sasa waangalie, ikiwa Mwalimu Nyerere aliweza kutoa dawa bure kwa wananchi, wanafunzi kusoma bure kwa uchumi mdogo, sasa wajiulize wao wanashindwaje wakati uchumi wa sasa umepanda,”anasema.
Anaeleza kuwa viongozi wa sasa wanatakiwa kuchukua mawazo yake na kuyaoanisha na mazingira yaliyoko, hali ambayo itasaidia nchi kupata maendeleo.
Anamuelezea Mwalimu Nyerere kuwa ni kiongozi aliyependa nchi kujitegemea katika kufanya mambo yake, badala ya kutegemea kila kitu kutoka kwa nchi nyingine.
Kwa mtazamo wake, anasema nchi inatakiwa kujifunza teknolojia kutoka nchi zilizoendelea na kuwafundisha watu wake wafanye wenyewe.
Anatoa mfano wa shughuli za ujenzi wa majengo makubwa ya vyuo vya elimu ya juu kwamba, kandarasi zake wanapewa watu wa nje, badala ya wazawa wenye uwezo huo.
“Katika uchumi wetu, kuna mambo tunatakiwa tufanye wenyewe ili kupunguza matumizi ya pesa za serikali, kama Mwalimu Nyerere alivyofanya, ndiyo maana alisisitiza elimu ya ujamaa na kujitegemea,”anasema.
Anaongeza kuwa nchi ni lazima igeukie kilimo kama Mwalimu alivyokuwa akikithamini na kukiita kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi.
Anasisitiza kuwa, kilimo na viwanda vikienda pamoja, nchi itakuwa imeenzi jitihada za Baba wa Taifa kwani ni vitu ambavyo vinategemeana.
“Kuna maeneo mengi unaweza kuanzisha kilimo, mfano mkoa wa Morogoro. Unaweza kuanzisha kilimo cha mpunga, unawekeza ukiwa na malengo, halafu mazao mapya yaangaliwe masoko kwani kwa sasa ni mengi, tofauti na enzi hizo,”anasema.
Akizungumzia uhusiano wa falsafa za Mwalimu Nyerere na  Rais Dk. John Magufuli,  anasema rais wa sasa anajitahidi kufuata falsafa hizo katika baadhi ya mambo.
Anasema Rais Magufuli anarudisha mfumo wa serikali ya awamu ya kwanza katika utoaji wa elimu bure na usawa katika umiliki wa mali za umma.
Anasema mipango na mikakati ya serikali ya awamu ya tano, iko katika mwelekeo wa kuenzi alichokiasisi Mwalimu Nyerere, hivyo ipewe muda katika utekelezaji wake.
Kuhusu ulinzi wa viwanda vya ndani, amempongeza Rais Magufuli kwa kuweka sera ya kuvilinda viwanda hivyo visiathiriwe na bidhaa za nje.
Mhadhiri wa zamani wa UDSM katika masomo ya Saikolojia na Mitaala, Dk. Alfred Mdima, anasema Watanzania na Waafrika wanapaswa kumuenzi kwa Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha umoja unadumishwa.
Dk.  Mdima anasema, Mwalimu Nyerere na waasisi wenzake wakati wa kupigania uhuru, walikuwa na ndoto ya Bara la Afrika kuwa moja, hivyo wananchi wamuenzi kwa kuendeleza ndoto hizo.
“Ili tumuenzi Baba Taifa, inatubidi kupigania sana umoja wa Watanzania wote na waafrika kwa ujumla, mpaka siku moja Afrika iwe nchi moja kubwa yenye nguvu na sauti duniani,”anasema.
Dk. Mdima, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mitihani wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), anasema njia nyingine ya kumuenzi ni kuzingatia elimu ili kupata maarifa ya kushindana na mataifa mengine.
Hata hivyo, anasema wananchi wanatakiwa kuondoa chuki ya mtu mmoja na mwingine, pamoja na makundi, kwani Mwalimu Nyerere alipinga vitendo vya namna hiyo.
                                                                                                                                                   

No comments:

Post a Comment