Wednesday, 30 March 2016

KORTINI KWA KUTUMIA JINA LA WAZIRI MKUU KUTAPELI
WATU wanne, wakiwemo mwanafunzi na mwandishi wa habari, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kujitambulisha kwa kutumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Pia, washitakiwa hao wanadaiwa kughushi barua zisizo na tarehe kuonyesha zimetoka Ofisi ya Rais, Ikulu, zikielekeza kampuni mbalimbali kuingiza sh. milioni 25, katika akaunti zilizopewa ili ziweze kupata punguzo la kodi.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni mwanafunzi Issa Awadh au Charles Mwamunyange au Trah Rio Mwenge (29), mtengeneza mihuri, Nicolaus Obado (32), mtangazaji, mwandishi wa habari na mfanyabiashara, Hamis Tembo (37) na mfanyabiashara Wakati Mungi (51).
Obado, Tembo na Wakati walipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ambapo Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pamela Shinyambala, waliwasomea mashitaka.
Kabla ya kuanza kusomewa mashitaka kwa washitakiwa hao watatu, Wakili Nchimbi alidai mshitakiwa Awadh, amelazwa  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hivyo aliomba mahakama kuhamia hospitalini hapo kwa ajili ya kumsomea mashitaka yanayomkabili.
Akiwasomea mashitaka washitakiwa waliokuwepo mahakamani hapo, Pamela alidai washitakiwa wote wanne kwa pamoja tarehe isiyofahamika, kati Machi 10 na 17, mwaka huu, sehemu tofauti wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam, walikula njama kutenda makosa ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Awadh, Obado, Tembo na Wakati wanadaiwa katika kipindi hicho, sehemu tofauti mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walijitambulisha wao ni Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu huku wakijua si kweli.
Kuanzia shitaka la tatu hadi la 11, washitakiwa hao wanadaiwa katika kipindi hicho, mkoani humo, walighushi barua mbalimbali zisizo na tarehe, kuonyesha ni halali, zimetoka ofisi ya Rais, Ikulu zikiwaelekeza wakurugenzi wa kampuni kuingiza sh. milioni 25 kila mmoja katika benki ya ABC, kwenye akaunti namba 1801833619, yenye jina la TRA. HR. MWENGE ili kupata punguzo la kodi, wakati wakijua si kweli.
Washitakiwa hao wanadaiwa kughushi barua hizo kuzielekeza kwa wakurugenzi wa kampuni za Usangu Logistics, Bakhresa and Company Limited, IPP Media, Oil Com, GAPCO Limited, Lake Oil CO Tanzania Limited na PUMA Company Limited.
Shitaka la 11, linamkabili Awadh, ambaye anadaiwa Machi 17, mwaka huu, katika ofisi za kampuni ya Usangu Logistics, aliwasilisha kwa  mtu wa mapokezi nyaraka za uongo, ambazo ni barua isiyokuwa na tarehe, kuonyesha kwamba ofisi ya Rais, ikimuelekeza mkurugenzi wa kampuni hiyo, kuingiza fedha hizo katika akaunti hiyo ili aweze kupata punguzo la kodi kwa kampuni hiyo.
Awadh na Tembo wanadaiwa Machi 10, mwaka huu, katika ofisi ya TSN Foundation, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, kwa pamoja kwa nia ya udanganyifu, walijipatia Dola za Marekani 1,000, kutoka kwa Farough Ahmad au Bagozah, baada ya kudanganya kwamba fedha hizo ni kwa ajili ya kudhamini masomo ya Awadh huko Marekani.
Tembo, Wakati  na Obado walikana mashitaka, ambapo Nchimbi alidai upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba shauri kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa, na mahakama izuie dhamana za washitakiwa hao kwa muda kwa madai ya kwamba, iwapo watakuwa nje, kuna hatari ya kuingilia upelelezi kwa namna unavyofanywa.
Kwa upande wao, washitakiwa waliomba mahakama iwapatie dhamana. Hata hivyo, Hakimu Simba alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na kusema maombi yao yana msingi kwa kipindi hiki cha upelelezi, hivyo washitakiwa watabaki rumande hadi hapo upelelezi utakapokamilika.
Hakimu Simba alitoa rai kwa upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi haraka na kuahirisha shauri hilo hadi Aprili 11, mwaka huu, kwa kutajwa.
Baada ya kuwasomea washitakiwa hao mashitaka, mahakama hiyo ilihamia Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa ajili kumsomea mashitaka Awadh.
Awadh alikana mashitaka, ambapo upande wa Jamhuri uliomba anyimwe dhamana kama wenzake. Hakimu alikubaliana na ombi hilo.

No comments:

Post a Comment