Wednesday, 29 June 2016

TUNDU LISSU KIZIMBANI

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), amepanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kujibu tuhuma za kuchapisha chapisho la uchochezi lenye kichwa cha habari' Machafuko yaja Zanzibar'.

Lissu, alifika mahakamani hapo jana, saa tano asubuhi, kwa ajili ya kuitikia wito wa kumtaka kwenda kujibu tuhuma za uchochezi zinazomkabili baada ya washitakiwa wenzake wawili, akiwemo Mhariri wa Mawio, ambalo lilifungiwa kwa muda usiojulikana, Simon Mkina kusomewa mashitaka.

Mbunge huyo na washitakiwa wenzake, Mkina na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob, walipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi kwa kushirikiana na Salim Msemo, ulidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Jabir Idrisa, bado hawajampata na wamepata taarifa anaumwa.

Kadushi aliomba kumsomea mashitaka Lissu, ambapo alimsomea mashitaka matatu ya kula njama za kuchapisha chapisho la uchochezi, kuchapisha taarifa ya uchochezi na kosa la tano, ambalo ni mbadala wa kosa la pili la kutishia.

Wakili huyo alidai Lissu na wenzake, kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu,  Dar es Salaam, walikula njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio, lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Pia, Lissu na wenzake walidaiwa  Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi  kati ya wananchi na mamlaka halali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye uchochezi.

Aidha, Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka, waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya uchaguzi mkuu.

Lissu alikana mashitaka hayo, ambapo Hakimu Simba alisema Juni 14, mwaka huu, shauri lilipokuja kwa mara ya kwanza, upande wa utetezi ulileta pingamizi juu ya uhalali wa mashitaka wakiomba yafutwe.

Hakimu Simba alisema sasa ni wakati wa upande waJamhuri kuwasilisha majibu yao kuhusu hoja hizo za utetezi.

Akiwasilisha majibu, Wakili Kadushi alikubali kwamba kimsingi shitaka la kula njama kuchapisha chapisho la uchochezi na kutishia halikuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), hivyo aliiomba mahakama kuyaondosha.

Upande wa mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, Omary Msemo na Stanslaus Ishengoma, haukuwa na pingamizi juu ya ombi hilo, hivyo Hakimu Simba aliyatupilia mbali mashitaka hayo mawili.

Baada ya kuondolewa kwa mashitaka hayo mawili, Wakili Kadushi alidai hati iliyobaki itakuwa na mashitaka matatu, ambayo ni la pili, tatu na nne, ambayo yapo sahihi mahakamani hapo.

Kadushi alidai shitaka la nne, ambalo ni la kuchapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti, lipo wazi na kwamba hoja ya utetezi ya kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa sababu Sheria ya Magazeti haiko katika mambo ya Muungano, haina mashiko.

Alidai mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa makosa yote yamefanyika Dar es Salaam.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala alidai hati ya mashitaka ina upungufu ambao hauwezi kutibika, hivyo inapaswa kuondolewa. Pia alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa sababu hoja ni machafuko ambayo yangetokea Zanzibar.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo hadi Julai 11, mwaka huu, kwa uamuzi na Lissu aliachiwa kwa dhamana kutokana na kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaotia saini dhamana ya sh. milioni tano kila mmoja.

No comments:

Post a Comment