CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kauli za Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad anazoendelea kuzitoa sehemu mbalimbali ni uongo na uchochezi.
CCM imezitaka imezitaka serikali mbili na vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kuvifumbia macho vitendo vinavyoendelea kufanywa na kiongozi huyo wa upinzani, kwani athari zake baadae zinaweza kuwa kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Pia, imevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya watu wanaopatikana na hatia kuhusiana na matukio ya uvunjifu wa amani ikiwemo uchochezi katika taifa.
Taarifa ya CCM iliyotiwa saini na Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi (Zanzibar), Waride Jabu, ilisema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa marudio wa Zanzibar, kumekuwa kukishuhudiwa matukio ya hujuma ambazo chanzo chake ni kauli za uchochezi, uongo na upotoshaji zilizotolewa hadharani na Maalim Seif anapofanya ziara kwenye maeneo tofauti Unguja, Pemba na nje ya Zanzibar.
"Wana-CCM, viongozi na wananchi wa Zanzibar wameshuhudia kuchomwa kwa mashamba ya mikarafuu, kuharibiwa mazao ya wakulima, watu hasa wanachama na wafuasi wa CCM kuchomewa nyumba, kuitishwa migomo, wananchi kushawishiwa kutoitambua serikali halali iliyoko madarakani na matukio mbalimbali yenye kuashiria uvunjifu wa amani na uhujumu wa uchumi wa nchi,"ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema juzi Maalim Seif kupitia televisheni ya “Voice of America” (VOA), alionekana hadharani akishutumu serikali za Tanzania na viongozi wake waliopo na walioondoka madarakani kwa madai tofauti ya uongo ikiwemo kile alichodai kukosa uwajibikaji na ukiukwaji wa makusudi wa misingi ya utawala wa sheria.
Ilisema kwa maoni yake CCM Zanzibar, jitihada za Maalim Seif hazina lengo la kutaka kurejewa uchaguzi wa Zanzibar ambao umefanywa kwa mujibu wa sheria za nchi, bali zinalenga kujitafutia umaarufu alioupoteza kutokana na ubinafsi wake wa kuwakataza wafuasi wake kushiriki uchaguzi wa marudio, jambo ambalo limewanyima fursa muhimu kisiasa ikiwa ni pamoja na kutoa hoja za kisheria kupitia chombo rasmi cha kutunga sheria Baraza la Wawakilishi.
CCM Zanzibar inajivunia amani na utulivu uliotawala nchini tangu kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015, hadi kumalizika kwa uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu ambao ulikamilisha ushindi wa CCM kwa pande zote mbili za Tanzania.
"Tunapongeza uteuzi wa viongozi waliounda serikali pamoja na juhudi za serikali kuzitafutia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili wananchi kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015 – 2020. Kadhalika tunapongeza hoja mbalimbali zinazotolewa na wajumbe wa CCM kwenye kikao kinachoendelea cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi.
"CCM inawaomba wananchi kutobabaishwa na kauli za uchochezi na uasi zinazotolewa na Maalim Seif ambaye dalili zinazonesha kuwa yeye na chama chake wamepoteza mwelekeo wa kisiasa badala yake wanatafuta mwelekeo mwengine ambao kamwe haukubaliki hapa nchini ambako hakuna historia ya vita wala matukio ya uasi,"alisema.
Chama kilisisitiza kwamba hakuna uchaguzi mwingine utakaofanyika kabla ya mwaka 2020 na hakuna serikali nyengine itakayokuwa madarakani kwa kile kinachodaiwa kumaliza mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment