MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula, amesema Chama na wana-CCM wote wanamuunga mkono Rais Dk. John Magufuli na kuwaonya wanaoeneza uchochezi kwamba Chama kinampinga na kumpiga vita.
Amesema kasi na kazi inayofanywa na Rais Magufuli ndilo lililokuwa lengo la CCM na kwamba Chama kinatambua na kupongeza juhudi zake.
"Hata Kamati Kuu ilipokutana mara ya mwisho ilitoa tamko la kumpongeza na kumtaka aendelee na kasi ya kuwatumikia wananchi," alisema Mangula.
Aidha, aliwataka Watanzania na wapenda maendeleo wote kuondoa hofu na dhana kwamba wapo watu wanaompinga ndani ya Chama kuwa hizo ni propaganda zinazosambazwa na wachache wasiopenda maendeleo ya Tanzania.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mangula alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, kwenye ufungaji wa kongamano lililodumu kwa siku tatu la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
"Kama kauli mbiu yake inavyosema 'Hapa Kazi Tu', tumethibitisha kweli Magufuli ni mtu wa kazi...kiongozi anapaswa kutenda anayotamka na si kutamka na kutenda tofauti," alisema.
Mangula aliwataka Watanzania kutopumbazwa na maneno ya wachache kuwa Rais Magufuli hakubaliki na kusema huo ni uchochezi usio na tija unaofanywa na watu wachache.
"Watu wengine wamekuwa na hisia tu pengine hakubaliki ingawa kuna uchochezi usio na maana wa watu wachache wenye lengo la kurudisha nyuma maendeleo. Kiukweli anakubalika na wengi,"alisisitiza Mangula.
Aliongeza kuwa kimsingi rais hajapigwa vita popote hususani kwenye Chama kama inavyozungumzwa, kwa kuwa hata mkutano uliofanywa mara ya mwisho wa Kamati Kuu ya CCM, ulitoa tamko la kumpongeza Rais Dk. Magufuli kwa utendaji wake mzuri.
Mangula alisema kila anachofanya Rais Magufuli kinaonekana na kukubalika, hivyo aliwaasa wanaofanya uchochezi kuacha kwa kuwa ni kurudisha nyuma jitihada zake na taifa kwa ujumla,"alisema.
Badala yake aliwataka Watanzania kumuunga mkono katika kukomesha rushwa na maovu, ikiwemo kuliletea taifa maendeleo.
Vile vile, alisema siasa zinazofanywa sasa na baadhi ya wanasiasa za kujibizana mitaani zinapaswa kuachwa kwa kuwa hazina tija katika ujenzi wa taifa.
Hata hivyo, Mangula alisema bado anaamini katika sera za Mwalimu Nyerere kuwa binadamu wote ni sawa, kila mtu anastahili heshima, kuthaminiwa na kutambuliwa utu wake.
Aliasa juu ya kuchanganya siasa na rushwa na kusema suala hilo linafanya siasa kugeuka kuwa biashara, jambo ambalo si sawa na kutolea mfano kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambapo wanachama 42 walichukua fomu za kuwania urais ndani ya CCM.
"Kwa yale tuliyofanya ndani ya Chama, ikiwemo uchujaji uliozingatia vigezo ni wazi bado tunafuata misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere," alisema Mangula.
Alitoa kauli hiyo, kufuatia michango ya baadhi ya washiriki wa kongamano hilo kudai kuwa misingi ya Mwalimu Nyerere ikiwemo kupinga rushwa, utu, usawa wa binadamu na mengine kuwa hayafuatwi.
Alisema mila na desturi nyingi zimefanywa kwa muda mrefu ikiwemo zinazoonekana hazifai hususani ukandamizwaji kwa wanawake vijijini na wanawake kuozwa kwa mahari, hivyo ni lazima igharimu muda tena kuzibadili.
Profesa Bertha Koda ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi UDSM, akichangia mada juu ya msimamo wa Mwalimu Nyerere na masuala ya kijinsia, alisema anaunga mkono mtazamo wa kuachwa kwa baadhi ya mila na desturi zinazorudisha nyumba maendeleo ya taifa.
"Mfano mila za mahari zinazofanya mwanamke kufananishwa na thamani ya vitu ikiwemo fedha, ng'ombe na mbuzi ni udhalilishaji na uvunjaji wa heshima yake kama binadamu, wanaume kuoa mitala, kupigwa na kutumikishwa," alisema.
Profesa Ruth Mukama, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, aliwataka Watanzania kusimamia kitabu cha Mwalimu alichotafsiri yeye, kiitwacho 'Usawa kwa Wanawake Katika Jamii', kwa kuwa kinayo mafundisho muhimu ya kupinga ukandanizwaji, rushwa na umasikini.
Alitaja baadhi ya mambo muhimu aliyoandika Mwalimu kuwa wanawake wanapaswa kupewa uhuru juu ya kuchagua wanaume wa kuwaoa, uamuzi wa kuolewa ama la, badala ya kulazimishwa, kuheshimu haki za binadamu katika maisha ya kila siku na kuondoa dhana potofu kuwa nguvu ya mtu ni kuwa na pesa.
Wakati huo huo, CCM imesema Kamati Kuu ya CCM itakutana kesho mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, kikao hicho ni cha kawaida.
No comments:
Post a Comment