Tuesday 21 June 2016

BAJETI YAPITA KWA KISHINDO


BUNGE jana lilipitisha bajeti kuu ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/17 kwa kishindo, baada ya wabunge 251 kati ya 252 waliokuwepo bungeni kuipigia kura ya ndio.

Upigaji huo wa kura ulifanyika kwa mujibu wa kanuni za bunge, baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuhitimisha mjadala kuhusu bajeti hiyo na kujibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wabunge.

Dk. Mpango aliwasilisha bajeti hiyo ya serikali Juni 9, mwaka huu, ambapo wabunge waliijadili kwa siku sita kabla ya kuhitimishwa kwa hoja hiyo jana.

Akisoma idadi ya wabunge waliopo bungeni, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema idadi kamili ya wabunge kwa sasa ni 389, lakini iwapo uteuzi wa rais utakamilika, idadi yao itakuwa 393.

Dk. Tulia alisema idadi ya wabunge wanaopaswa kupitisha bajeti ni 185 na kwamba waliokuwepo bungeni wakati wa kupiga kura walikuwa 252 na wasiokuwepo walikuwa 137.

Alisema katika upigaji huo wa kura, wabunge 251 walipiga kura ya ndio, hakukuwa na kura ya hapana wakati kura moja ilishindwa kuamua.

Akijibu michango ya wabunge, Dk. Mpango alisema serikali imeyakataa mapendekezo ya wabunge ya kutaka asilimia tano ya malipo ya kiinua mgongo cha wabunge kila baada ya miaka mitano yafutwe.

Dk. Mpango alisema serikali haiwezi kuondoa tozo ya kodi katika kiinua mgongo cha wabunge, badala yake inachokifanya ni kila kiongozi wa kisiasa kuanza kukatwa kodi hiyo, akiwemo rais.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, mbali na rais wa nchi, viongozi wengine watakaokatwa kodi hiyo ni makamu wa rais, waziri mkuu, spika wa bunge na naibu spika, wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

Alisema uamuzi huo wa serikali umelenga kuonyesha dhamira ya ukusanyaji kodi kwa watanzania wote.

“Hatua hiyo ni kuweka msingi na haki katika kukatwa kodi kwa kuwa watu wengine kwenye sekta binafsi na utumishi wa umma wanatozwa kodi kwenye mafao yao,"alisema.

Aidha, Dk. Mpango alisema serikali haijaongeza fungu la fedha katika bajeti ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa sababu fedha zilizotengwa zinatosha.

Wakati wa kuchangia bajeti hiyo, wabunge wengi walilalamikia fedha zilizotengwa kwa ajili ya ofisi ya CAG kwa madai kuwa ni kidogo na hazitamwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Dk. KIJAJI
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, akijibu hoja za wabunge, aloisema serikali imeendelea kufanyia kazi ripoti ya Chenge One kwa kila jambo, ambalo wanalifanya.

Dk. Ashatu alisema ripoti hiyo ilionyesha uhitaji wa serikali kupata mapato kupitia kampuni za simu nchini, ambapo kwa kuanzia ni kupata asilimia 10 ya makusanyo kutoka kwa kampuni hizo.

“Utaratibu wa kupata asilimia 10 hautahusu watumia simu na itakuwa ni katika kile ambacho kinakatwa na kampuni hizo ambazo zilikuwa hazilipi,” alisema.

Aidha, alisema serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekuwa ikitumia taarifa za hesabu za Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMA) kama nyenzo muhimu ya ukaguzi na ugunduzi wa maeneo hatarishi.

Akizungumzia kuchelewa kulipwa kwa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Dk. Ashatu alisema ni kutokana na mchakato wa uhakiki kwani hadi Mei, mwaka huu, uhakiki wa PSPF ulikuwa umekamilika, ambapo deni sahihi ni sh. trilioni 2.04 kutoka sh. trilioni 2.67, hivyo kulikuwa na madeni hewa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, akizungumzia sh. bilioni 59 zilizotengwa kwa ajili ya kuvipatia vijiji sh. milioni 5 kila kijiji, alisema serikali imeunda jopo la wataalamu, ambao wanatengeneza utaratibu madhubuti utakaozingatia uzoefu wa miaka ya nyuma wa mifuko mbalimbali, lengo likiwa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Walemavu, Jenista Mhagama akizungumzia suala la wageni kufanyakazi nchini bila kuwa na vibali, alisema kuanzia sasa serikali itakuwa ikipambana na waajiri wanaokiuka sheria.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema dhamira ya serikali ni kuongeza tozo kwenye mitumba inayoingia nchini ili kulinda  viwanda vya kuzalisha nguo.

Aliwaondoa hofu wenye viwanda vya kuzalisha nguo hapa nchini na kuwataka kuvuta subira wakati wakiendelea na uzalishaji na kuahidi baada ya miaka mitatu, utakapokuwa mzuri, mitumba itapigwa marufuku.

Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, serikali iliomba kuidhinishiwa shilingi trilioni 29.5 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.

No comments:

Post a Comment