Tuesday 21 June 2016

MAAMUZI YA JPM NI SERA ZA CCM-MANGULA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM-Bara), Philip Mangula, amewashukia  wanasiasa na wanaharakati wanaomshutumu Rais Dk. John Magufuli katika utekelezaji wake wa dhana ya utumbuaji majipu kuwa, hayo si maamuzi yake binafsi, bali yapo ndani ya sera za Chama.

Aidha, amesema Chama kinaunga mkono kauli ya Rais Dk. Magufuli, aliyoitoa hivi karibuni kwamba, anakusudia kujaza vijana wengi zaidi katika serikali yake.

Mangula alisema hayo jijini Dar es Salaam, jana, wakati akizindua kitabu  kiitwacho 'Majipu ya Nchi Yetu: Tushirikiane kuyatumbua', kilichoandikwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Kampeni ya Vitabu na Midahalo (KVM) na Kada wa CCM, Amos Siyantemi.

Mangula alisema kitabu hicho kimekuja wakati mwafaka, ambapo serikali ya CCM, chini ya Rais Dk. Magufuli, imekuwa ikitekeleza sera  zake kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa, ufisadi, kusimamia dhama ya uwajibikaji na uzalendo.

“Dhama  hii si ya Rais Dk. Magufuli, bali ni ya CCM. Yeye ni mtekelezaji tu. Haya anayoyafanya Rais yapo katika Ilani yetu ya uchaguzi ya Chama na Chama kinayatekeleza kupitia kwa Rais Dk. Magufuli,”alisema.

Mangula alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. Magufuli na kuwataka wananchi kumuunga mkono.

“Ilani ya CCM inaeleza wazi kwamba, tutapambana na rushwa na ufisadi  kwa nguvu zaidi. Hivyo  Rais anachokifanya sasa ni kutekeleza kwa vitendo.

“Tofauti ya walionacho na wasionacho ilikuwa ni kubwa. Wapo watu walikuwa wanapokea mishahara hadi  sh. milioni 40. Rais amelisemea hili kwa sababu ni kitu, ambacho hakiwezekani. Kwa kweli amefanya kazi kubwa,”alisema Mangula.

Akizungumza  tuhuma kwamba, serikali ya awamu ya tano inabana uhuru wa wananchi, Mangula alipinga fikra hizo na kueleza kwamba, mjadala wa bunge kuonyeshwa moja kwa moja  (live) katika runinga, hauna tija kwa sababu si kila kinachozungumzwa bungeni ni habari ambayo wananchi wanatakiwa kuipata.

“Hakuna mtu anayekaa siku nzima katika runinga au kusikiliza redio. Pia si kila kitu kinachozungumzwa ni habari, hivyo sioni kama kuna suala la kuminywa kwa uhuru wa  kujieleza,”alisema Mangula.

Mangula alimpongeza mwandishi wa kitabu cha 'Majipu ya Nchi Yetu; Tushirikiane Kuyatumbua', Siyantemi kwamba, kimegusa kwa mapana mapambano ya ujenzi wa taifa  na Afrika mpya.

"Nimekisoma kitabu hiki, maudhui yake yanachochea moyo wa uzalendo na uwajibikaji kwa watendaji, viongozi na Watanzania wote. Kitabu hiki kimetoa wito maalumu kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dk. Magufuli za utumbuaji majipu pamoja na kuitekeleza kwa vitendo falsafa yake ya hapa kazi tu,”alisema.

Mangula alisema kazi anayoifanya Siyantemi kuandika vitabu pamoja na uendeshaji wa kampeni ya usomaji na uandishi wa vitabu ni ya kimapinduzi na ni ushahidi kwamba, nchi yetu ina hazina kubwa ya viongozi na kwamba, wakipewa majukumu ya uongozi wataifanyia makubwa Tanzania na Afrika.

“Mwandishi wa kitabu hiki ameainisha vikwazo na changamoto mahususi za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi, zinazoikabili nchi yetu na vilevile amefanikiwa kutoa masuluhisho yake,” alisema Mangula.

Aliongeza:”Pia ametumia ujuzi wa hali ya juu wa kisanaa wa kuvipa vikwazo na changamoto hizo jina la majipu.  Hii ni kwa vile dhana ya jipu inaeleweka kirahisi kwa watanzania wote kutokana na falsafa ya utumbuaji majipu inayoendelea hapa nchini dhidi ya baadhi ya watendaji wazembe kwenye sekta ya umma.”

Alisema kutokana na uzito wa maudhui yaliyomo katika kitabu hicho, atapeleka nakala  moja ya kitabu kwa Rais Dk. Magufuli, marais wastaafu pamoja na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete ili wakisome.

Kwa upande wake, Siyantemi alisema maudhui ya kitabu hicho yanachochea moyo wa uzalendo na uwajibikaji kwa watendaji, viongozi na wananchi kwa ujumla.

“Kupitia kitabu hiki, nimetoa wito maalumu kwa watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kwa kuitekeleza kwa vitendo falsafa yake ya  hapa kazu tu,” alisema.

"Nimeamua kukipa kitabu changu jina hilo kwa sababu neno jipu linatumika  sana katika zama za sasa za serikali hii ya awamu ya tano na kwa mantiki hiyo, itakuwa rahisi kuwahamasisha watanzania kushiriki kwenye mapambano ya kujenga Tanzania mpya, pamoja na kushirikiana na serikali katika kuwadhibiti watendaji na viongozi wazembe,"alisema.

No comments:

Post a Comment