Tuesday, 21 June 2016
WAPINZANI WAONYESHA VIOJA BUNGENI
WABUNGE wa kambi ya upinzani bungeni jana, waliendeleza viioja na vitimbi baada ya kuingia bungeni na kutoka huku wakiwa wameziba midomo yao kwa karatasi nyeupe zenye gundi.
Huo ni mwendelezo wa mgomo wa wabunge hao, kuhudhuria vikao vya bunge vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kwa madai ya kutokuwa na imani naye.
Kwa takribani mwezi sasa, wabunge hao wamekuwa wakisusia kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za bunge, ikiwemo kuchangia mijadala ya bajeti, ikiwemo bajeti kuu, ambayo ilihitimishwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phili Mpango.
Mara baada ya kuwasili ukumbini jana, wabung hao wa upinzani walianza kugawana vipande vya makaratasi na gundi kwa lengo la kuziba midomo yao endapo kikao hicho kingeendeshwa na Dk. Tulia.
Baada ya Naibu Spika, Dk. Tulia kuongoza dua ya kuliombea bunge na kuwaamuru wabunge kuketi, wabunge hao wa upinzani walijiziba midomo yao kwa makaratasi na kutoka nje ya ukumbi.
NJE YA UKUMBI
Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa bunge, baadhi ya wabunge hao walidai kuwa wamebuni mtindo huo mpya
kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii kwamba, hawatachangia mjadala wa bajeti na mambo mengine yote hadi hapo watakapopata majibu ya kuwaridhisha kuhusiana na malalamiko yao ya kutokuwa na imani na Dk. Tulia.
Pia, walisema wataendeleza utaratibu wa kutoka bungeni na kutoshiriki shughuli za bunge endapo kiongozi huyo atakalia kiti.
Walisema hawawezi kupiga kura ya kupitisha bajeti, ambayo hawakushiriki kuijadili kwa kile walichodai kuwa wamefungwa mdomo na Naibu Spika.
Aidha walisema wanajiandaa kwenda mitaani kuishtaki serikali kupitia mikutano ya hadhara kwa madai kuwa hiyo ni haki yao ya kikatiba na kwamba hakuna mwenye mamlaka ya kuwazuia.
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, (NCCR-Mageuzi), alidai wamelazimika kufunga mdomo ili kuionyesha jamii vitendo ambavyo vinafanywa na serikali na Naibu Spika katika Bunge hilo.
"Kimsingi hatuna haki ya kupigia kura bajeti kwa sababu hatukuijadili lakini tumekuwa tukihitaji suluhu ila Naibu Spika ameonyesha kuwa na kiburi na dharau, ambazo haziwezi kukubalika kwa watu ambao wanajitambua," alisema.
MAWAZIRI WAMPA MOYO DK. TULIA
Baadhi ya mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, walimpongeza Dk. Tulia kutokana na msimamo wake, ambao unasimamia misingi, kanuni na taratibu zilizopo kisheria.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, aliwapongeza wabunge wa CCM kwa kutumia vyema nafasi yao ya uwakilishi bungeni.
Alisema wakati wapinzani wamegomea shughuli za vikao vya bunge zinazoendelea kutokana na kupagawa na msimamo mahili wa naibu spika, wao wametumia nafasi hiyo bila kuachia mwanya.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philipo Mpango, alimpongeza Naibu Spika kwa umahiri wa hali ya juu katika kusimamia kanuni wakati akiendesha shughuli za vikao vya bunge.
Dk. Mpango alisema viwango vyake ni vya kimataifa ndio mana wapinzani wamekimbia kwa kuwa walizoea ubabaishaji.
“Ningekuwa bado niko chuoni, ningempatia alama mia kwa mia kama walivyofanya maprofesa wako wa sheria pale chuo kikuu cha Dar es Salaam,” alisema.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema, watu wamekwisha ingia kwenye gari moshi (treni), hivyo ni lazima iondoke, hakuna namna.
“Watu wakubali wakatae, lazima treni iondoke na ndivyo itakavyokuwa kwa serikali hii ya awamu ya tano, ambayo ni serikali ya viwanda,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, akichangia mjadala huo, alimpongeza Dk. Tulia kwa kutoyumba katika kiti chake wakati wa kuendesha vikao vya bunge.
Alisema amekuwa akisimamia bila kulegalega utekelezaji wa kanuni za kudumu za bunge, jambo ambalo ndio sahihi katika uendeshaji bora wa shughuli za bunge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment