Monday 23 January 2017

SERIKALI YALIPA DENI BIL. 29 KWA WATUMISHI WA UMMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imelipa sh. bilioni 29, kwa watumishi mbalimbali wa umma, wakiwemo walimu ikiwa ni sehemu ya madeni yao.

Alitoa kauli hiyo juzi, wakati akizindua vyumba vitatu vya kisasa vya madarasa katika shule ya sekondari Iwawa, iliyoko wilayani Makete.

Waziri Mkuu alisema serikali imedhamiria kumaliza madeni ya watumishi hao, ambapo hadi Novemba mwaka jana, sh. bilioni 29, zililipwa kwa watumishi 31,000.

Alisema kwa sasa serikali imejipanga kuhakikisha hakuna madeni mapya yanayozalishwa, hivyo aliwataka watumishi wa umma na wananchi kuendelea kuiunga mkono.

Hata hivyo, alisema serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

“Tumeanza mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu katika halmashauri nchini. Hapa Makete tumeleta sh. milioni 557, kwa ajili ya ujenzi huo,”alisema.

Alisema nyumba hizo za walimu zinazojengwa katika maeneo mbalimbali, hususan ya vijijini, ni za kisasa ambazo zinalenga kuwaondolea changamoto ya makazi.

Waziri Mkuu alisema serikali inafanya jitihada za dhati za kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu kwa kuwa elimu ni kichocheo cha maendeleo ya jamii.

Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Novatus Msivala, aliishukuru serikali kwa kugharamia ujenzi wa vyumba hivyo vitatu vya madarasa na matundu 10 ya vyoo pamoja na uingizaji wa maji kwenye vyoo na utengenezaji wa madawati 46.

Alisema ujenzi huo umegharimu sh. milioni 95 na kwamba, utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi. Alisema kwa sasa serikali na wananchi wanaendelea kukamilisha ujenzi wa vyumba vingine viwili vya madarasa na ofisi ya walimu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu jana, alitimiza ahadi yake ya kumpatia laptop mwanafunzi Ally Alijai wa Chuo Kikuu cha SAUT tawi la Songea mkoani Ruvuma.

Ahadi hiyo aliitoa mwanzoni mwa mwezi huu, alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma, lengo likiwa ni kuendeleza kipaji cha utunzi wa vitabu kwa mwanafunzi huyo.

No comments:

Post a Comment