Saturday 30 July 2016

JPM: SIJARIBIWI


NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

RAIS Dk. John Magufuli amesema yeye si mtu wa kujaribiwa, hivyo atawashughulikia wale wote wanaojaribu kufanya vurugu au kuwahamasisha watu wafanye vurugu.

Amesema hataki nchi iwe ya vurugu kwa kuwa Watanzania wengi wana shida na huu ndio wakati wao wa kutumikiwa ili wapate maendeleo kwa kasi kubwa.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani hapa wakati wa ziara ya siku moja huku akiwataka Watanzania wafanye kazi kwa bidii.

“Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma, na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa,’’alisema.

Rais Dk. Magufuli aliongeza kuwa: “Wananchi hawa wana shida na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate dawa.”

Akizungumzia maandamano ya wapinzani ya Septemba Mosi, Rais Dk. Magufuli alisema amewaonya kuacha kumjaribu kwa sababu hawataamini kitakachowakuta.

ìHao wanaochochea maandamano watangulie wao, wasiwatangulize watoto wa masikini kwa kuwapa viroba huku wao wakibaki hotelini wakisikilizia. Wananchi wametuchagua ili tuwaletee maendeleo sio maandamano, hivyo sitaki mtu yeyote anicheleweshe,î alisema.

“Wasinijaribu kwa kulazimisha maandamano siku ya tarehe moja Septemba…. atakayethubutu kufanya hivyo kitakachompata mmmh, hatasahau kamwe. Mimi ni tofauti sana, wasije wakanijaribu,” alionya Rais Dk. Magufuli huku akishangiliwa na umati mkubwa uliohudhuria.

Aidha, alisema ni ruksa kwa wanasiasa kufanya mikutano ya kuhimiza maendeleo kwenye maeneo yao.  ìKama wewe ni mbunge wa Jimbo la Hai, zunguka kwenye jimbo lako hadi uchoke si unaacha kwako unaenda Shinyanga kushawishi watu waandamane. Mimi sijazuia shughuli za wachaguliwa kwenye maeneo yao bali nimekataa mtu kuondoka jimboni kwake na kwenda kufanya fujo mahali pengine,î alisisitiza.

Hivyo, aliwasihi wananchi waendelee kumuunga mkono na kumwombea hasa wakati huu anapoendelea kukabiliana na ufisadi nchini kwa kuwa anaowatumikia ni wananchi wa kawaida ambao hali zao za maisha ni duni.

Kauli ya Rais Dk. Magufuli inaendana na msimamo uliotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa operesheni inayotajwa kutaka kufanywa na CHADEMA imefadhiliwa na wakwepa kodi na wahujumu uchumi waliobanwa na mianya yao.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. Magufuli ni kubwa na wapinzani wamekosa agenda na ndio maana wanakuja na operesheni zisizokuwa na faida kwa taifa huku wakiwa wanawatetea wahujumu uchumi na wakwepa kodi.

“Wapinzani wanataka kutunga uongo ili waendelee kupata wafuasi huku wakijua fika serikali haijazuia mikutano ya kisiasa kwani wabunge wapo huru kufanya mikutano kwenye majimbo yao yote, lakini tunajua wanataka kuwatetea wahujumu uchumi na wakwepa kodi,’’alisema Sendeka.

Sendeka aliwataka Watanzania waelezwe ukweli kuwa hoja za wapinzani si za kweli na wanapaswa kujiuliza udikteta wa Rais Dk. Magufuli ni kuzuia na kuwashughulikia watumishi hewa? kuwabana wakwepa kodi?, kupunguza na kudhibiti safari za nje? au kubana matumizi ya serikali?.

Alisema CCM inaamini Watanzania wengi wanaunga mkono juhudi za Rais Dk. Magufuli na hawatakuwa tayari kuona damu za watanzania zikimwagika kutokana na uongozi wa watu wachache wanaotaka kutumia siasa kumwaga damu za Watanzania wasiokuwa na hatia.

“CCM inapenda kuwaasa Watanzania wajiulize kabla ya kushiriki ni vizuri watafakari na kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kuamua kushiriki au kuruhusu watoto wetu kuwa mbuzi wa kafara,’’alisema Sendeka.

Katika hatua nyingine, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ameituhumu CHADEMA kwa kutoa kauli zilizojaa uchochezi.

Jaji Mutungi amesema kauli za chama hicho cha upinzani ni kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa na kauli zao zina lengo la uchochezi na kuleta vurugu kwa Watanzania.

No comments:

Post a Comment