Saturday 30 July 2016

SERIKALI KUPIGA MNADA MAJENGO YAKE YALIYOKO DAR



NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

RAIS Dk. John Pombe Magufuli amesema mchakato wa kuhamia makao makuu ya nchi Dodoma utakapokamilika, atapiga mnada majengo ya serikali yaliyopo Dar es Salaam ili yageuzwe hoteli au mambo mengine.

Pia, amesema mtumishi yeyote wa serikali atayekataa kuhamia Dodoma, atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe na hatapata mshahara kutoka serikalini.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana katika ziara yake ya siku nne kwenye mikoa minne ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita ikiwa sehemu ya kuwashukuru kwa ajili ya kumchagua katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Alisema azma ya serikali yake kuhamia Dodoma haraka iwezekanavyo ipo pale pale huku akiwaonya wale watakaong’ang’ania kubaki Dar es Salaam kuwa watakuwa wamejifukuzisha kazi wenyewe.

“Nitahakikisha baada ya kuhamia Dodoma napiga mnada majengo yote ya wizara na atakayeng’ang’ania kubaki huko ajue hana kazi wala mshahara.’’alisema Rais Dk. Magufuli.

Aliongeza kuwa: “Hatuwezi kuendelea kukaa miaka 50 tunaimba tu kuhamia Dodoma wakati hatutekelezi maamuzi yetu hadi wengine wameshatangulia mbele za haki.”

Akizungumzia hatua alizochukua toka alipokabidhiwa madaraka, alisema serikali yake tangu iingie madarakani amechukua hatua kadhaa ikiwemo kufuta ada kwa shule za msingi na sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya 100,000 .

Alisema amefanikiwa kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika bajeti ya serikali kutoka asilimia 26 ya mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 40 katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017.

“Tumeondoa wafanyakazi hewa 12,500 katika orodha ya waliokuwa wanalipwa mshahara na serikali, kudhibiti upotevu wa mapato serikalini, kutenga sh. trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa yaani standard gauge,’’alisema.

Hivyo, alisema ataendelea kuchukua hatua dhidi ya wala rushwa na wanaojihusisha na ufisadi kwa kuunda mahakama ya mafisadi huku akiapa kuwa katika kipindi chake hakuna fisadi atakayeendelea kutamba

 

No comments:

Post a Comment