Sunday, 31 July 2016

DOVUTWA: ISINGEKUWA BUSARA ZA CCM, TAIFA LINGEANGAMIA

MWENYEKITI wa Chama cha UPDP na aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania, Fahmi Dovutwa, amesema kama si busara za CCM, kumteua Rais Dk. John Magufuli, kuwania nafasi hiyo ya uongozi, taifa lingekuwa kwenye hali ya hatari zaidi kwa kutawaliwa na genge la wala rushwa.

Amesisitiza kuwa, genge hilo la wala rushwa na wakwepa kodi, liliamua kuingilia uchaguzi kwa kumpanga kiongozi wamtakaye mwenye kusimamia maslahi yao.

Aidha, amesema ushindi wa kishindo alioupata Dk. Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kipimo tosha kwa wana-CCM na Watanzania kuwa, wanamwamini kutokana na uongozi wake kulinda maslahi ya umma.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, ambapo alisema endapo genge hilo la wabadhirifu lingefanikiwa, kura ya maoni kwenye vyama ya kuwapata wagombea ingekuwa utaratibu usiokuwa na maana.

Alisema badala yake, wabadhirifu hao wa mali za umma, wangepanga kila nafasi iongozwe na mtu wanayemtaka na sio kujali matakwa ya wapiga kura.

“Kama si busara za CCM, hali ya nchi ingekuwa mbaya kwa sababu genge la wala rushwa, wakwepa kodi na majangili waliamua kuingilia uchaguzi na kupanga ni nani awe kiongozi,” Dovutwa alisisitiza.

Mwenyekiti huyo pia alipongeza utaratibu wa CCM wa kuachiana madaraka na kutaka iungwe mkono na vyama vingine.

“Kuna vyama vya siasa ambavyo viongozi wake wanakabidhiana madaraka barabarani, hivyo naipongeza CCM na Mwenyekiti mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, kwa kuendeleza utamaduni wa kuachiana madaraka kwa nderemo na vifijo huku kada zote za chama zikishuhudia,” aliongeza.

Alimwomba Mwenyekiti mpya wa CCM, Dk. Magufuli, kufuata katiba, kanuni na kalenda za vikao kwani akizingatia hayo, kazi ya uenyekiti itakuwa rahisi zaidi kwa kiongozi huyo ili kuepuka kupewa angalizo kutoka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

Dk. Magufuli alikabidhiwa uenyekiti wa CCM, Jumamosi wiki iliyopita, baada ya wajumbe wa mkutano mkuu kumchagua kwa kura zote 2,398, na kuweka rekodi ya kuwa mwenyekiti wa kwanza kuchaguliwa kwa kura zote.

Kukabidhiwa nafasi hiyo ni utamaduni wa Chama kwa kila rais kushika wadhifa huo baada ya kuingia madarakani.

Rais Magufuli ameandika historia ya kuwa mwenyekiti wa tano wa CCM, akitanguliwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Ali Hassani Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete.

No comments:

Post a Comment