Sunday 1 November 2015

IKULU YAMKANA MAALIM SEIF




NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema haijapokea maombi yoyote kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kutaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete, kujadili hali ya kisiasa ya Zanzibar baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu visiwani humo.
Imesema madai yaliyotolewa na Maalim Seif kuwa, serikali imepuuza maombi hayo hayana ukweli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, Ikulu ilisema maombi yaliyotumwa na CUF yalikuwa ni malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi na maombi ya kutaka kufanya mazungumzo kati ya Maalim Seif na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange.
Baada ya kutolewa kwa maombi hayo, Rais Kikwete amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, kuchunguza malalamiko hayo ya CUF kisha kutoa taarifa kamili.
Pia, Rais Kikwete ametoa maagizo kwa ofisi yake kusimamia mazungumzo kati ya viongozi wa CUF na Jenerali Mwamunyange.
Jitihada hizo za Rais Kikwete, zimeonyesha dhamira thabiti ya namna anavyotilia mkazo hali ya kisiasa Zanzibar, kwa kufanyakazi usiku na mchana ili kutafuta suluhu ya kisiasa kwa amani.
Licha ya hatma ya uchaguzi wa Zanzibar kuwa mikononi mwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), taarifa hiyo imeeleza kuwa, Rais Kikwete yuko tayari kufanikisha suluhu hiyo.
Uchaguzi wa Zanzibar ulitangazwa kufutwa Oktoba 28, mwaka huu na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha, baada ya kubainika kasoro kadhaa, ikiwemo idadi ya wapigakura kuzidi na ile iliyoandikishwa kwenye daftari la wapiga kura.
Kasoro nyingine ni kupigwa kwa mawakala wa vyama vya siasa kwenye vyumba vya kupigia kura pamoja na wajumbe wa ZEC kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Profesa Lipumba amuomba JK
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ameibuka na kumuomba Rais Kikwete, kumaliza mgogoro wa Zanzibar kabla ya kuapishwa kwa Dk. John Magufuli.
Alisema ni vyema kuelewa kuwa  endapo yatatokea machafuko kisiwani Zanzibar, Dar es Salaam haitabaki salama hivyo ni muhimu mgogoro huo ukamalizwa kistaarabu .
Akizungumza jana Makao Makuu ya CUF jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema ni wazi hatua iliyofikia Zanzibar, wananchi wake hawako tayari kurudia uchaguzi na ili kuzuia machafuko busara za Rais Kikwete zinahitajika.
Alisema ameona ipo haja ya kutoa mawazo yake akiwa  Mtanzania mzalendo na si kwa shinikizo la mtu  bali kwa maslahi ya taifa.
“Niliposikia Dk. Magufuli ataapishwa Alhamisi na kuanzia siku hiyo atakuwa Amiri Jeshi Mkuu, nimeona ipo haja jambo hili la Zanzibar kumalizwa kwanza na Rais Kikwete ambaye ni mwanasiasa,” alisema.
Alisema Rais Kikwete kutolimaliza suala hilo na kumuachia Dk. Magufuli ni kumuongezea mzigo wa kuanza kushughulikia migogoro.
“Na kwa Zanzibar Katiba iko wazi kabisa, chama chochote kitakachoweza kupata zaidi ya asilimia tano za kura wataingia kwenye serikali ya umoja wa kitaifa, kwenye uchaguzi huu CUF wana viti 27, CCM 26 na jimbo moja halijapiga kura hivyo wamelingana,” alisema.
Alisema kutokana na hali iliyopo, usikivu wa serikali unahitajika na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutumia busara ili visiwa hivyo visirudi kwenye machafuko.

No comments:

Post a Comment