Tuesday 3 November 2015

MAALIM SEIF AMELIKOROGA, SASA ALINYWE




Alifanya kosa la kihaini kujitangaza mshindi

Anawezaje kuipa serikali saa 48 imkabidhi nchi?

Jumuia za kimataifa hazipaswi kutoa shinikizo

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

WAZANZIBAR wamekuwa katika hali ya sintofahamu tangu yalipofutwa
matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita.

Katika uchaguzi huo ulioshirikisha vyama 14, ushindani zaidi ulikuwa
baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichomsimamisha Dk. Ali Mohammed Shein, kupeperusha bendera katika urais na CUF kama kawaida yake, kilimuidhinisha Maalim Seif Sharrif Hamad.

Vyama vyote vilifanya kampeni kuanzia Septemba 13, mwaka huu na
kuhitimisha shughuli hiyo Oktoba 25, mwaka huu, kwa wananchi kupiga kura.
Kwa taratibu za Zanzibar,wananchi hupewa siku moja ya kupumzika ili kuhakikisha zilipo kadi zao za kupigia kura na kutafakari ahadi za wagombea na siku ya pili inakuwa kazi kwao kuamua wa kuwachagua.

Uchaguzi wa Zanzibar, inayoundwa na visiwa viwili vikubwa vya Unguja na
Pemba, unahusisha nafasi tano ambazo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Kisiasa Wazanzibar wamepevuka kwa uelewa na wana mwamko mzuri pengine kuliko watu wa mataifa mengi Afrika, kwani wake kwa waume, vijana na wazee, wote hawachezei nafasi adimu ya kupigakura kama ilivyokuwa Oktoba 25, mwaka huu.

Tangu saa 12 asubuhi wananchi waliojitokeza kupigakura, walijipanga
mistari mirefu, wakiwa na shauku ya kutumia haki yao hiyo kikatiba.
Hakuna aliyetaka kutopiga kura kwa makusudi.

Kwa mtu asiyetafakari vizuri anaweza kudhani kujitokeza kwao kwa wingi
kunatokana na uchache wao, mfano wapigakura walioandikishwa na Tume
ya Uchaguzi (ZEC), jumla ni 503,860, lakini ufinyu huo si kigezo cha
kuwafanya wachangamkie kupigakura, bali inatokana na mwamko mkubwa walionao tangu zama za utawala wa sultani na hatimaye ilipoundwa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ).

Viongozi wa vyama vya siasa wapo vizuri katika kujenga hoja na wanajua
hasa kurushiana vijembe, ambavyo mtu mgeni anaweza kubaki anashangaa na kujiuliza maswali kwamba nini kitajiri baada ya uchaguzi kwa kuwa kuna maisha mengine baadaye, lakini wenyewe wameshazoea miaka mingi hali hiyo.

Pia, wakati wa kwenda au kutoka kwenye viwanja vya kampeni, huwa
hapakosekani matukio ya kuvamiana baina ya wafuasi wa vyama na
kujeruhiana hapa na pale, ingawa katika kampeni za mwaka huu, uhasama
haukuwepo kabisa au ulipungua.

Hatua hiyo inatokana na kuwepo muafaka uliounda serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK), uliovishirikisha vyama vya CCM na CUF, hivyo kutokuwa ajabu wafuasi wa vyama hivyo  kupeana mikono njiani walipokutana wakiwa kwenye magari.

Wapenzi wa vyama vyote walisafiri kwa magari ya aina mbalimbali pamoja
na pikipiki kwenda kwenye maeneo zilikofanywa kampeni za wagombea
urais au nafasi za chini ya hiyo.

HALI YA UCHAGUZI ILIVYOKUWA

Kwa ushuhuda mdogo katika vituo vya Unguja, ambako Dk. Shein alipiga
kura katika Shule ya Msingi Bungi na Maalim Seif, Mtoni Kidatu, hali
ilikuwa shwari na wananchi walionekana na nia ya dhati ya kutaka
kumaliza shughuli hiyo ili warejee majumbani kusubiri kusikiliza
hatima ya mshindi.

Hata hivyo, baadaye zikasambaa taarifa za CCM kuchezewa 'faulo kali'
katika Mkoa wa Mjini Magharibi, wenye watu wengi zaidi katika kisiwa cha
Unguja.

Malalamiko ya CCM yalitokana na mawakala wao kutolewa katika vyumba
vya uchaguzi kutokana na kutokuwa na vitambulisho vya ZEC, ambavyo
haikueleweka sababu hasa ya kutopewa.

Mawakala hao hawakuruhusiwa kuingia katika vyumba vya uchaguzi hadi
ilipofika saa nne asubuhi, ndipo walipatiwa vitambulisho wakaingia,
lakini wakati huo mchakato wa upigaji kura ulikuwa umeshaanza zaidi ya
saa nne nyuma.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alilalamikia faulo hiyo ambayo amedai ilifanywa makusudi na maofisa wasio waaminifu wa ZEC kwa lengo la kuibeba CUF katika uchaguzi huo.

"Siku moja kabla ya uchaguzi vitambulisho vya mawakala wetu tuliviona
ZEC, lakini ilipofika siku ya uchaguzi, havikuonekana na hatujui
vilichukuliwa na nani," alisema Vuai akiilalamikia ZEC

Inawezekana kwa asilimia 99, ZEC walicheza mchezo huo kwa kuwa mpaka
matokeo ya uchaguzi yalipofutwa na Mwenyekiti Jecha Salim Jecha,
Jumatano iliyopita, tume ilikuwa haijatoa ufafanuzi wowote rasmi
kuhusu madai hayo au yaliyohusu jimbo la Chonga, lililoko Chakechake,
Pemba kuhusu wakala kukamatwa na kura tano bandia.

Maeneo hayo mawili na mengine ambayo huenda ZEC iliyabaini yenyewe,
ndiyo yaliyomshawishi Jecha kwa mamlaka aliyonayo, kufuta matokeo yote
na kupanga uchaguzi urudiwe kwa kuwa haukuwa huru na haki.

Alisema uchaguzi huo ulikuwa na jumla ya dosari tisa, ambazo
zimemridhisha achukue hatua hiyo. Hivyo, vyama havina budi kusubiri
uchaguzi mwingine, ingawa Maalim Seif hatambui uamuzi huo wa ZEC na
kushinikiza atangazwe mshindi wa urais.

Kauli ya mgombea huyo wa CUF ilikuja wakati alijitangazia ameshinda
kwa asilimia 52.87, akidai amepata kura 200,077, dhidi ya 178,363 za
CCM, ambazo sawa na asilimia 47.13. Kwa hesabu hizo za Maalim Seif, ni kwamba vyama vingine havikupata kura?

Hatua hiyo ya Maalim Seif kutangaza ameshinda kufuatia kuwa na matokeo
yote kutoka kwa mawakala wake si kwamba ilikuwa inaiweka Zanzibar
katika hali tete, bali binafsi alipaswa kutiwa mbaroni kwa agizo la
ZEC ili akajibu mashitaka.

Kwa mujibu wa sheria, tume pekee ndiyo yenye mamlaka ya kumtangaza mshindi wa urais, ndio sababu hata CCM ilipotoa tamko lake juzi, ilieleza kushangazwa kuona mgombea huyo yuko huru mpaka sasa licha ya kutenda kosa kikatiba.

KAULI ZA JUMUIA YA KIMATAIFA

Saa chache baada ya ZEC kutamka imefuta matokeo ya uchaguzi, yakaibuka matamko kama 'mvua' kutoka jumuia za kimataifa, yakiongozwa na nchi za Marekani na Uingereza, kutaka kura ziendelee kuhesabiwa mpaka mwisho na mshindi atangazwe.

Hatua hiyo iliongeza fukuto kati ya CUF na tume, pamoja na CCM ambacho
kimesimama imara kwamba uchaguzi haukuwa huru, huku Seif ambaye ni
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, akitoa matamshi ya kutishia kuvunja amani,  waliyoitafuta kwa nguvu hadi kuipata baada ya kutoweka tangu ulipoanza uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995.

Moja ya tamko lake ambalo limeanza kuamsha vurugu kufuatia watu
wanaoaminika kuwa ni wafuasi wake, ambao baadhi waliandamana na kukutwa na bomu, ambalo liliteguliwa eneo la Mkunazini siku nne zilizopita na mengine mawili kulipuka Michenzani bila kudhuru watu, ni kuipa
serikali saa 48 imkabidhi nchi.

Alikwenda mbali kwa kusema kwamba hilo lisipotendeka, yeye na viongozi wenzake wataondoa mikono yao kwa wananchi ili kuwaacha waamue cha kufanya. Hii si kauli nzuri kwa kiongozi mkubwa na mwanasiasa mwandamizi kama Maalim Seif.

Kwa nafasi yake katika serikali, anatakiwa kuwa wa kwanza kuhubiri
amani na kupinga umwagaji wa damu kwa watu wasio na hatia, kwani
yanapozuka mapigano, raia wa kawaida ndio wanaoathirika. Maalim Seif
anatambua hilo.

Kama hiyo haitoshi, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), ubalozi wa Marekani
na nchi ya Uingereza kwa ujumla hazipaswi kuwa mstari wa mbele
kushinikiza mchakato wa uchaguzi uendelee, ilihali tume yenye mamlaka
ya kufanya kazi hiyo imeshasema kulikuwa na kasoro.

Nchi hizo na jumuia zinazotaka uhesabuji wa kura uendelee, zisidhani
jambo hilo ni jepesi. Waangalizi wa kimataifa wanapata wapi ujasiri wa
kusema uchaguzi ulikuwa huru na haki wakati hawajui hata kidogo
mazingira ya rafu za uchaguzi wa nchi za Kiafrika?

Msimamo walionao una ajenda ya siri. Kwanini waegemee CUF pekee na
kukipuuza CCM, ambacho mawakala wake walitolewa katika vyumba vya
kupigia kura zaidi ya saa nne na kuwaacha mawakala wa vyama vingine
wakitamba na kufanya watakavyo?

Kuna siri iliyojificha katika mioyo ya waangalizi hao ambao, huenda
wanalazimisha kukitoa madarakani chama wasichokipenda na kukipa nchi
kile wanachopenda hata kwa kuingilia mlango wa nyuma.

Jambo la kusikitisha zaidi ni pale jumuia hizo zinaposhikilia kauli
za kutaka kura zihesabiwe na kusahau au kupuuza kwa makusudi kwamba,
vyama zaidi ya vinne vinalia na kasoro za uchaguzi huo.

Chama cha ADC na AFP vyote kwa nyakati tofauti, viongozi wake
wamenukuliwa katika matamko yao kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kwa kuwa walipandikiziwa chuki kwa wananchi wa Pemba, ili wasipate kura pamoja  na kuwepo ubaguzi mwingi kama wa kutishia kuwatimua Watanzania Bara wanaoishi Zanzibar.

Mbali ya maneno hayo yaliyosemwa na Hamad Rashid, ambaye ni mbunge wa zamani wa jimbo la Wawi, Wete, Pemba, Mwenyekiti wa AFP, Said Soud amekiri kuwa uchaguzi ulikuwa na kasoro nyingi, ikiwemo masanduku ya kura kuhamishwa kutoka kituo namba nne kupelekwa namba sita bila sababu za msingi.

Anasema uamuzi huo ulizua mzozo kuanzia saa moja usiku hadi saa tano usiku na ulikosekana uamuzi, huku maofisa waandamizi wa ZEC walioko Pemba wakishindwa kuchukua hatua na kubariki baadhi ya vitendo visivyofaa.

Soud, ambaye alishuhudia ujanja mwingi ukifanywa Pemba kwa sababu alipita katika baadhi ya vituo kufuatilia mchakato wa uchaguzi mwenyewe,
alihoji: "Hao waangalizi wanadhani uchaguzi kuwa huru maana yake watu
kupigakura bila ya kugombana na kupanga mistari?"

Anasema rafu za uchaguzi Afrika wanazijua wenyewe kama alivyobaini
katika chumba kilichopelekwa masanduku,  alikuwemo mtu ambaye alikaa
kuanzia asubuhi hadi usiku akiwa hafahamiki majukumu yake.
Je, hilo au kutumbukizwa kura nyingi za bandia katika masanduku na kufanya zivuke idadi ya watu walioandikishwa Pemba, wamechunguza na kujiridhisha hakukuwa na ubabaishaji kwenye mchakato huo?

Waangalizi watafakari kauli wanazotoa kuwa zinalenga kuwasaidia watu
wa Zanzibar au kuwaharibia maisha na kuwaacha katika historia isiyofaa
kuisoma au kusikiliza.

Siku zote vurugu zinagharimu maisha ya watu kwa kuwaacha na vilema,
vizuka, wagane na watu wengi kupoteza maisha na bila ya kupindisha
ukweli, matamko hayo hayaitazami Zanzibar kwa macho mawili, isipokuwa
jumuia hizo zinataka mapenzi yao yatimizwe.

Wazanzibar wamechoka mahubiri au matamko ya shari kwa nia ya kuamsha hasira, wanachopenda ni amani iliyopo.

Hivyo, jumuia za kimataifa ziache kupaza sauti zitakazokuwa chanzo cha kuzuka kwa ghasia na zibebe jukumu la kuzikutanisha pande zinazosuguana kisha kuipa tume fursa ya kuita uchaguzi mkuu mwingine wa viongozi halali.

No comments:

Post a Comment