Tuesday 3 November 2015

MAFURIKO YATIKISA MWANZA, WAWILI WAPOTEZA MAISHA





Na waandishi wetu, Mwanza
MTU mmoja amekufa na mwanafunzi wa kidato cha nne Zainab Shaban (18), hajulikani alipo huku wanafunzi wengine wanne wa kidato hicho wakinusurika kifo, baada ya kusombwa na mafuriko ya maji yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jijini hapa.
Mbali na kifo hicho, mvua hiyo iliyonyesha kwa zaidi ya saa tano, kutoka saa 12 alfajiri hadi saa 5:20 adhuhuri, pia imesabisha uwanja wa ndege wa Mwanza kufungwa kwa saa tano kutokana na kujaa maji.
Habari zilizopatikana kutoka katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo zimesema baadhi ya nyumba katika maeneo ya Kiseke na Mabatini, zimeanguka huku miti iking’olewa na kusombwa na maji na kusababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali, ikiwemo barabara, madaraja na mabomba ya maji.
Akitoa taarifa ya madhara yaliyosabishwa na mvua hiyo jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Charles Mkumbo, alisema mwanafunzi huyo wa kidato cha nne aliyekuwa akisoma katika Sekondari ya Nyamanoro, alisombwa na maji wakati akivuka mfereji uliojaa maji, maeneo ya Nyamanoro na wenzake wawili ambao walinusurika.
“Aliyethibitika kufariki kwa kusombwa na mafuriko ya mvua hiyo ni dereva wa bodaboda mmoja, ambaye jina lake halijapatikana, aliyekuwa akiendesha pikipiki yenye namba za usajiri MC. 861 AHA,” alisema Kamanda Mkumbo na kufafanua:
“Dereva huyo wa bodaboda alikuwa amebeba wanafunzi wawili waliokuwa wakienda kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, lakini wao walinusurika.”
Alieleza kuwa mwili wa dereva huyo umekutwa katika maeneo ya Villa Park, Kirumba na jitihada za kusaka mwili wa mwanafunzi Zainabu, anayehofiwa kufa, zinaendelea hivyo mwananchi atakayeuona mwili huo atoe taarifa.
Habari kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza zimesema kuwa, ulijaa maji na kulazimika kufungwa kutoka saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 na kusababisha ndege kushindwa kutua na kuruka.
“Ni kweli mvua hii imesabisha mafuriko na uwanja wetu kujaa maji, hali ambayo isingekuwa salama kwa kutua na kuruka kwa ndege, hivyo tumefunga uwanja toka saa 3:00 asubuhi hadi hali itakapokuwa nzuri,” alisema Meneja wa uwanja huo, Ester Madale, wakati uwanja huo ukiwa umefungwa.
Madale alisema uwanja ulifunguliwa saa 8:00 mchana jana na ndege ya kwanza ilianza kuruka saa 6.45 mchana.
Habari kutoka katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza zimesema madhara mengine yametokea katika maeneo ya Mabatini, Mtaa wa Nyerere ‘B’ wilayani Nyamagana na Kiseke, wilayani Ilemela, ambapo baadhi ya nyumba zinadaiwa kuanguka kutokana na kujaa maji huku vyombo mbalimbali vikisombwa na mafuriko hayo.
Mbali na uharibifu huo, miundombinu ya barabara, madaraja na mabomba pia vimedaiwa kuharibiwa na maji na kusabisha barabara za Mkuyuni, Voil, Tanesco, Mabatini, Kona ya Bwiru, Pasiansi na Kiseke zisipitike kwa urahisi na kusababisha msongamano wa magari.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji Mkoani Mwanza, Andrew Mbate, alisema jana kuwa kituo cha kulelea watoto cha Pasiansi wilayani Ilemela, kilikumbwa na mafuriko na jeshi lake kulazimika kupiga kambi katika kituo hicho na kufanikiwa kuokoa watoto wote ambao hakutaja idadi yao.

Hali ya Hewa yatoa tahadhari
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wadau wa hali ya hewa kuchukua tahadhari kwa namna mbalimbali wakati huu, ambao mvua za vuli kwenye maeneo mbalimbali ya nchi zinaendelea kunyesha.
Imesema kama ilivyoeleza awali kwenye utabiri wake wa msimu, mvua za vuli za mwaka huu zina viashiria vingi vya kuwepo kwa El Nino, kutokana na kuongezeka kwa joto kwenye maeneo ya bahari ya Pasifiki ambayo ni chanzo cha mvua hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, alitoa tahadhari hiyo Dar es Salaam jana, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, ambapo aliwashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wakiwemo wakulima na wafugaji kuwa makini kuzifuatilia.
Vilevile ilizitaja Mamlaka za Maji na Afya na wananchi kwa ujumla kuwa ni wadau ambao wanapaswa kuendelea kufuatilia taarifa za mamlaka hiyo ili kuepuka maafa ambayo yanaweza kutokea kutokana na mvua hizo.
Kupitia taarifa hiyo, alisema wananchi na wadau wengine wanatakiwa kuendelea kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika katika jitihada zao za kutekeleza mipango inayoweza kuathiriwa na mwelekeo wa hali ya hewa iliyotabiriwa.
Pia, alieleza kuwa maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria, Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani katika kipindi cha kuanzia mwezi huu hadi Disemba, pamoja na vipindi vifupi vya mvua kubwa.
Aidha, kwenye taarifa hiyo, TMA ilisema mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, tofauti na ilivyotarajiwa awali, itakuwa na vipindi virefu vya upungufu wa mvua katika msimu huu kutokana na mwitikio hasi wa mfumo ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi.
Maeneo mengine ya nchi yametabiriwa kuwa na vipindi vya mvua za wastani mpaka juu ya wastani katika msimu huu, kuanzia mwezi huu na mwanzoni mwa Desemba.

No comments:

Post a Comment