MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha (AFD), Said Soud Said, akifafanua jambo kwa wandishi wa habari wakati wa mkutano huo. |
NA WILLIAM SHECHAMBO
VIONGOZI na wawakilishi wa vyama vya siasa hapa nchini,
wamezitaka nchi wadau wa maendeleo kuacha kuliingilia suala la kurudiwa kwa
uchaguzi mkuu wa Rais na wawakilishi visiwani Zanzibar.
Wamesema ni ukweli usiopingika kuwa kuna uzembe mkubwa
uliofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), katika kusimamia uchaguzi huo,
uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, hivyo kusababisha kutokuwa huru na haki.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na UHURU, Dar es Salaam,
jana, wanasiasa hao waliokuwa kwenye maandalizi ya hafla itakayofanyika leo ya
kumuaga Rais Jakaya Kikwete, walisema hali iliyoko Zanzibar itatulizwa na
Watanzania wenyewe.
Walisema Rais Kikwete ana uwezo mkubwa wa busara ambayo
awali ilisaidia kuleta amani visiwani humo kwa kuwaleta pamoja viongozi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CUF ili washirikiane kuongoza dola.
“Hakuna haja na mtu mwingine kuingilia suala hili, Rais
Kikwete ana busara sana, tunaamini ataweza kulitatua kwa falsafa na busara
aliyoitumia kipindi kile cha kuwapatanisha Maalim Seif na Aman Karume. Kitendo
cha hawa wenzetu kuleta maneno mengi kutavuruga zaidi mambo,” alisema Juma Ali
Hatib.
Hatib, ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya
ADA-TADEA na Makamu wa Rais wa chama hicho Taifa, alisema kuwa hali iliyoko
Zanzibar inazidi kuwa mbaya kwa maisha ya watu kutokana na kupanda kwa gharama
za maisha.
“Wiki mbili zilizopita, gunia la viazi mbatata Zanzibar
lilikuwa sh. 100,000, leo hii nazungumza na wewe ni sh. 250,000 na hii ni kwa
sababu boti kutoka bara zinaenda mbili tu kwa siku wakiogopa usalama,” alisema.
Alisema jinsi siku zinavyozidi kwenda, ndivyo mambo
yanavyozidi kuwa magumu kwa wananchi, hivyo umefika wakati wa Rais Kikwete
kulivalia njuga suala hilo ili uchaguzi huo ufanyike tena kwa uangalifu tofauti
na awali.
Said Sudi Said, ambaye ni Mwenyekiti wa AFP Taifa,
alisema hakuna sababu ya nchi wahisani kuingilia suala la Zanzibar kwa kuwa
siku chache zijazo mambo yatarudi kama yalivyokuwa awali.
Alisema kinachotakiwa kufanyika ni kuundwa kwa serikali
ya mpito, ambayo itasubiri kurudiwa kwa uchaguzi mkuu ambao utamruhusu rais
kupewa madaraka yake kikatiba.
“Tunajua katiba haisemi kuwepo kwa serikali ya mpito,
ila ninashauri wakubaliane iwepo kwa siku hizo za kusubiri uchaguzi ufanyike
tena ili kuepusha zogo la kisiasa,” alisema.
Aidha, alimshauri mgombea urais wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad, kupunguza jazba na kusubiri uchaguzi urudiwe ili haki itendeke
kwa anayestahili.
No comments:
Post a Comment