NA MWANDISHI WETU
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeamua
kurudiwa kwa mchakato wa kura za maoni katika jimbo la Handeni mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisi Ndogo za
Chama, Lumumba mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye, alisema uchaguzi huo, unarudiwa leo, chini ya
wasimamizi Maua Abeid Daftari, Dk. Emmanuel Nchimbi na Abdalla Bulembo.
Nape alisema uamuzi huo ulitolewa jana na kikao cha
Kamati Kuu, chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kikao hicho kilikuwa maalumu kwa ajenda maalumu,
ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili majimbo ambayo hayakufanya uchaguzi
kwa sababu mbalimbali.
Nape alisema mchakato wa kumpata mgombea katika jimbo la
Handeni, ulikamilika lakini hakuna mgombea aliyepata kura za kuridhisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati Kuu, imeamua
uchaguzi wa kura za maoni urudiwe na kwamba wagombea wawili ndio watapigiwa
kura katika uchaguzi huo.
Nape aliwataja wagombea hao kuwa ni pamoja na Omari
Kigoda na Khamis Mnondwa, ambao walipata kura za juu.
Hata hivyo, alisema kuwa mtoto wa kiongozi si hoja ya
kukosa sifa ya kugombea kwani, nafasi ya ubunge inatangazwa hivyo kila
Mtanzania mwenye sifa anayo haki ya kugombea.
Uchaguzi wa Jimbo la Handeni, unarudiwa kufuatia kifo
cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Abdalah Kigoda, kilichotokea nchini
India, alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Dk. Kigoda ambaye pia alikuwa Waziri wa Viwanda na
Biashara, alifariki dunia Oktoba 12, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment