NA
WAANDISHI WETU
SIKU
chache baada ya aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, kushindwa
na mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, CHADEMA
wameanza mikakati ya kuvuruga amani ya nchi.
Katika
uchaguzi huo ambao ulikamilika kwa amani na utulivu huku waangalizi wa ndani na
nje ya nchi wakithibitisha kuwa ulifanyika kwa amani, utulivu na bila
kuingiliwa, mgombea wa CHADEMA alilalamika kuonewa kwa madai kuwa ameibiwa
kura.
Katika
madai hayo aliyoyatoa kwa vyombo vya habari kabla na baada ya kukamilika kwa
mchakato wa kuhesabu kura, alisema yeye ndiye alistahili kuwa mshindi wa
uchaguzi huo na kwamba hatakubali matokeo hayo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC).
Kauli
hiyo ya Lowassa ilionyesha dalili za kutaka kuharibu amani ya nchi kwa kuwa
mamlaka husika kwenye kutangaza matokeo hayo (NEC), ilikiri kuwa matokeo
yalikuwa halali yasiyokuwa na kasoro hivyo kila mgombea aridhike nayo.
Hata
hivyo, CHADEMA walionekana kuendelea na mikakati ya chini kwa chini kama moja
ya njia za kupinga matokeo hayo, wakianzia na kutokuhudhuria kwenye vikao
muhimu vya NEC vilivyowajumuisha wagombea wote kwa lengo la kutia saini hati ya
ushiriki wao.
Jana,
viongozi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali ya nchi, waliendeleza mkakati
wao kwa kuwasilisha kwa jeshi la polisi barua za maombi ya kufanya maandamano
waliyoyaita ya amani, yasiyo na kikomo, ombi ambalo jeshi la polisi limekataa
na kusema endapo yatafanyika ni batili.
Kutoka
Kanda ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake jana, alisema walipokea barua ya CHADEMA saa 7.30 mchana ambapo
iliwataka watoe kibali cha maandamano hayo.
Alisema
barua hiyo ilikiuka sheria za nchi kwa kuwasilishwa kwa kuchelewa na kwamba
maandamano yasiyo na kikomo hayajawahi kutokea hapa nchini na hata katika nchi
zilizowahi kuyapata kwa sasa hazina amani.
Alisema
barua hiyo yenye namba ya kumbukumbu CDM/PW/GEN/042/2015, ilionyesha kuwa
imeandikwa Oktoba 31, mwaka huu, ikieleza azma yao ya kufanya maandamano maeneo
yote ya jiji la Dar es Salaam, bila kikomo kwa madai ya kupinga kubakwa kwa
demokrasia.
Kova
alisema baada ya kuipokea barua hiyo waliisoma kwa makini pamoja na kupata
tafsiri za kisheria na kubaini kuwa imekiuka sheria ya polisi sura ya 322, k/f
43 (1) ya mwaka 2002, inayotaka barua ya aina hiyo kuwasilishwa saa 48 kabla ya
kufanyika kwa maandamano.
Pia,
alisema katika barua hiyo, CHADEMA walimtaja Edward Lowassa, kuwa mshindi wa urais
katika uchaguzi mkuu, jambo ambalo ni
kinyume cha sheria ya nchi ibara ya 41 (7), iliyoko kwenye katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, inayotoa mamlaka kwa NEC pekee kumtangaza rais.
Kamishna
Kova alinukuu sheria hiyo kuwa: ”iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi
kwamba amechaguliwa kuwa rais kwa mujibu wa ibara hii, hakuna mahakama yoyote
itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”
Aidha,
ibara ya 74 (11), imeeleza wazi kuwa katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu
wa masharti ya katiba hii, Tume ya Uchaguzi haitalazimika kufuata amri au
maagizo ya mtu yeyote au idara yoyoyte ya serikali au maoni ya chama chochote
cha siasa.
Kova
alisema maandamano yasiyo na kikomo hayawezekani kwa kuwa yatasababisha
usumbufu kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kushindwa
kufanya shughuli zao.
Alisema
pia hayakubaliki na kwamba jeshi la polisi linapiga marufuku maandamano hayo
yanayotarajiwa kufanyika leo, kwa kuwa yana vishiria vya kutaka kuvuruga amani
ya nchi.
Aliwataka
wananchi kutokujihusisha na maandamano hayo kama walivyokataa agizo la baadhi
ya viongozi wa vyama vya siasa waliowataka kusimama mita 200 kulinda kura
Oktoba 25, mwaka huu.
Mwanza
Akizungumza na waandishi wa habari jana, ofisini
kwake, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Charles Mkumbo, alisema jeshi lake
limepiga marufuku maandamano ya CHADEMA yaliyoombwa kufanyika leo wilayani
Misungwi, kupinga ushindi wa Rais Mteule Dk. John Magufuli.
Kamanda huyo alisema wakati huu wa maandalizi ya kuapishwa kwa Rais
Mteule, kitendo cha kuandamana kitakuwa ni kukiuka sheria na kusababisha
uvunjifu wa amani, hivyo watu wakatae na waendelee na shughuli zao.
“Uchaguzi umepita, tufanye kazi za maendeleo na siyo suala la kupinga
kura za kiongozi fulani, maana kumchagua mtu ni utashi wa mtu baada ya kuridhika
na sera zake na kumuamini kuwa ndiye atakayewaletea maendeleo na ndiyo
demokrasia,” alieleza Kamanda Mkumbo.
“Kama hujaridhishwa na matokeo vipo vyombo vya sheria, siyo maandamano
maana ni uvunjifu wa sheria. Nachukua fursa hii kuwatangazia wale wote
waliokuwa wanataka kuandamana kesho (leo), maandamano ni marufuku mkoa wa
Mwanza, atakaye kiuka tutamchukulia hatua maana amevunja sheria,” alisisitiza
Mkumbo.
Singida
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Thobias Sedoyeka, alisema jeshi
lake lilipokea barua ya CHADEMA kuomba kufanya maandamano hayo, lakini
hawayaruhusu.
Alifafanua
kuwa pamoja na kupinga matokeo hayo yaliyotangazwa, CHADEMA na vyama
vinavyounda UKAWA, vinaitaka pia mamlaka husika (NEC) kumtangaza mgombea wao,
Edward Lowassa wakiamini kuwa ndiye mshindi wa kiti cha urais.
Alisema
uchunguzi unaonyesha kuwa maandamano hayo yatashirikisha makundi mbalimbali ya
watu, hususan vijana zaidi na kupita sehemu mbalimbali za mji kabla ya
kuhitimisha katika ofisi walizolenga.
Mwenyekiti
wa CHADEMA mkoa huo, Shabani Limu alikiri kupokea maagizo kutoka ngazi za juu
za chama hicho na kuongeza kuwa, mpaka sasa bado hakuna mafanikio ya kufanyika
kwa maandamano hayo kutokana na makamanda wa polisi wa wilaya zote kutoyaruhusu
kwa kuhofia uvunjifu wa amani.
“Ni
kweli tumepokea taarifa kutoka kamati kuu ya chama kwamba maamuzi ya kamati kuu
ni kufanya maandamano nchi nzima kupinga matokeo ya urais ambayo yametangazwa
na Tume ya Uchaguzi.
“Nimesambaza
taarifa zote kwa viongozi wangu wa wilaya, wakawa wamepekela taarifa hizi kwa
maofisa wa polisi wa wilaya zao, lakini mpaka leo (jana) na mpaka sasa wakati
nikiendelea kuzungumza na nyie, maofisa wa polisi wa wilaya wamekataa maandamano
haya kwa kudai kuwa hayatakuwa ya amani,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment