Sunday 1 November 2015

HUYU NDIYE WAZIRI MKUU WA DK. MAGUFULI





NA MUSSA YUSUPH
WAKATI Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akitarajiwa kuapishwa rasmi Alhamisi, wingu zito limetanda kuhusiana na nani atakuwa Waziri Mkuu wake.
Mbali na nafasi ya Waziri Mkuu, pia wingu hilo limetanda zaidi kuhusiana na Baraza la Mawaziri ambalo kiongozi huyo ataliteua kumsaidia kazi kubwa ya kuwatumikia Watanzania.
Mara kadhaa Dk. Magufuli amekuwa akiweka bayana sifa za mtu ambaye atamteua kushika nafasi ya Waziri Mkuu, ambaye kwa mujibu wa Katiba ndiye msimamizi wa shughuli za serikali.
Kwa sasa Watanzania wanasubiri kwa hamu kubwa uteuzi wa Dk. Magufuli, ambaye ameahidi kuwa atateua watendaji wachache na waadilifu na ambao watafunga mkataba wa kazi baada ya kukubali uteuzi wake.
Hata hivyo, tayari baadhi ya wanasiasa wakiwemo mawaziri na manaibu mawaziri waliopo kwenye Baraza la Rais Jakaya Kikwete, ambaye anamaliza muda wake rasmi Alhamisi, wameanza kutajwa.
Miongoni mwa mawaziri na manaibu wanaotajwa kuwa huenda wakachomoza kwenye nafasi hiyo ni Dk. Harrison Mwakyembe (Ushirikiano wa Afrika Mashariki), William Lukuvi (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wengine ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kuchomoza kwa majina ya wanasiasa hao kunatokana na utendaji kazi na ushiriki wa karibu kwenye kampeni za CCM, ambapo walionyesha uimara mkubwa na kuwa bega kwa bega na wanachama wengine katika kusaka ushindi.

WILLIUM LUKUVI
Ni mbunge mteule wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa, ambaye amefanikiwa kutetea nafasi yake kwa mara nyingine tena. Ni mwanasiasa mzoefu na mtendaji kazi mwenye msimamo usioyumba.
Ana uzoefu mkubwa katika utumishi serikali. Kabla ya kushika Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Lukuvi amepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge).
Ana uzoefu mkubwa na masuala ya uongozi wa Bunge na katika muda mfupi alihamishiwa Ardhi, ambako amefanya mageuzi makubwa, ikiwemo kusafisha watendaji wabovu waliokuwa wakishirikiana na matapeli kupora ardhi ya wanyonge.
Katika kipindi cha muda mrefu amesaidia Watanzania waliokuwa wakiumizwa kwa kudhulumiwa haki zao ndani ya wizara hiyo, kurejesha furaha kwa kutendewa haki waliyostahili.
Kwa kiasi kikubwa kero ya migogoro ya ardhi katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam, imepatiwa ufumbuzi na idadi kubwa ya wananchi wamerejeshewa ardhi waliyoporwa na wajanja wachache.
Lukuvi pia amepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na baadaye Dar es Salaam. Alizaliwa Agosti 15, mwaka 1955, ni mtaalamu wa masuala ya siasa, diplomasia na uongozi.

MWIGULU NCHEMBA
Mwanasiasa kijana aliyejizolea sifa nyingi katika kipindi kifupi. Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Iramba Mashariki mwaka 2010, ambapo muda mfupi baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara).
Akiendelea na shughuli za ubunge na kutumia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha, wakati Rais Kikwete alipofanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri.
Kwa sasa Mwigulu ni mbunge mteule wa jimbo hilo, baada ya kufanikiwa kulitetea kwa kura nyingi. Misimamo yake ndiyo inamfanya kuwa miongoni mwa wanaotajwa kushika wadhifa huo, ambapo alisimama kidete kuhakikisha watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliohusika kwenye kashfa ya Escrow wanawajibika.
Pia alisisima kidete kuhakikisha watuhumiwa wengine waliohusika kwenye kupata mgawo, wanakatwa kulipa kodi za serikali, jambo ambalo lilimpa sifa maradufu.
Mwigulu alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya CCM, ambapo alizunguka maeneo mbalimbali kufanya kampeni huku akiendeleza staili ya kupiga ‘push up’ ya Dk. Magufuli.
Alizaliwa Januari 7, mwaka 1975, ana Shahada ya Uzamili ya masuala ya fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Msimamo wake katika masuala ya utendaji kazi na kutofumbia macho uzembe ndio unamfanya kuwepo kwenye nafasi nzuri ya kushika nafasi hiyo.

JOB NDUGAI
Pamoja na kuwa kwenye nafasi nzuri ya kushika wadhifa huo, lakini pia Ndugai anabashiriwa huenda akabeba mikoba ya kuwa Spika wa Bunge iliyoachwa na Anne Makinda.
Uhodari, utulivu na misimamo isiyoyumba pindi anapokalia kiti cha Spika, umemjengea sifa ya pekee na umaarufu wa aina bungeni.
Pia, ameonyesha uwezo mkubwa wa kuliendesha bunge bila upendeleo kwa kutoa nafasi kwa kila mbunge kutoa au kuchagia hoja pamoja na kudhibiti nidhamu pindi ilipoonekana kutoweka kwenye chombo hicho muhimu cha kutunga sheria.
Mbunge huyo wa jimbo la Kongwa, alizaliwa Januari 21 mwaka 1960, ana elimu ya Shahada za Uzamili kutoka Chuo cha Maastricht cha Uholanzi na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Norway.

JANUARI MAKAMBA
Mmoja wa wanasiasa vijana wanaokuja kwa kasi kubwa. Amekuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Dk. Magufuli, akishika eneo muhimu la kupashana habari. Alikuwa mmoja wa wajimbe 32 wa Kamati ya Ushindi ya CCM, lakini akiwajibika kikamilifu na kwa karibu zaidi kila wakati.
Ni mbunge mteule wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, ikiwa ni kipindi chake cha pili baada ya kuingia kwa mara ya kwanza mwaka 2015, alipofanikiwa kumuangusha kwenye kura za maoni mwanasiasa mkongwe, William Shelukindo.
Kwa sasa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, nafasi ambayo ameimudu vyema na kufanya mageuzi makubwa ndani ya wizara hiyo, akishirikiana na Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.
Pamoja na mambo mengine, ana sifa ya kuwa mtendaji kazi mwenye kufanya maamuzi kwa haraka na mwenye msimamo usioyumba.
January alianza kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje kama Ofisa wa Mambo ya Nje Daraja la Pili.
Alipata nafasi ya kufanya kazi na Rais Kikwete, wakati huo akiwa waziri kwenye wizara hiyo katika harakati za kutafuta suluhu ya amani kwenye nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wakati Rais Kikwete alipoingia kwenye mbio za urais mwaka 2005, January ndiye alikuwa mwandishi wa maandiko mbalimbali huku akiwa muanzilishi wa kampeni za televisheni na mabango makubwa kwenye barabara kwa mara ya kwanza nchini.
Pia, kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa miongoni mwa wasaidizi wa Rais Kikwete, Ikulu. Alizaliwa Januari 28, 1974, mkoani Tanga.
Alihitimu elimu ya msingi shule ya msingi Masiwani, kisha kujiunga na kidato cha kwanza Handeni Sekondari na baadae kuhitimu kidato cha nne Galanos Sekondari.
Alihitimu kidato cha sita, Shule ya Sekondari Forest Hill, ambako kwa sasa ana Shahada ya Uzamili ya Diplomasia na usuluhishi wa migogoro kutoka chuo Kikuu cha George Mason, Marekani.

PROFESA SOSPETER MUHONGO
Wakati anajiuzulu wadhifa wa Waziri wa Nishati na Madini, wapenda maendeleo nchini walihuzunika na kusikitishwa kutokana na utendaji kazi makini. Katika kipindi cha muda mfupi alichoongoza wizara hiyo, amefanya mageuzi makubwa na kurejesha matumaini mapya hususan kwenye sekta ya nishati na madini.
Ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya Jiolojia, ambaye aliachia ngazi kwa kuhusishwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Anarejea tena bungeni akiwa mbunge wa Musoma Vijijini, ambapo awamu iliyopita alikuwa mbunge wa kuteuliwa. Utendaji kazi na sifa yake ya kusema ukweli hata kama unaoumiza, imekuwa kivutio kwa Watanzania wengi wapenda maendeleo.
Amedumu kwa miaka mitatu, lakini alikuwa kichocheo katika ujenzi wa mradi mkubwa wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Pia, amewezesha wachimbaji madini wadogo wadogo, kupatiwa maeneo maalumu ya uchimbaji, elimu pamoja na vifaa vya utafiti na uchimbaji madini.
Profesa Muhongo ni mwandishi wa makala za kisanyansi za Jiolojia zaidi ya 150. Alizaliwa June 25, 1954 na kutunikiwa hadhi ya Profesa na Chuo Kikuu cha Petrolia mwaka 2006.
Mwaka 2009, aliteuliwa na serikali kuwania nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la Sanyansi Duniani (UNESCO).
LAZARO NYALANDU
Mmoja wa mawaziri vijana na makini katika serikali ya Rais Kikwete, ambaye anatajwa kuimudu kikamilifu Wizara ya Maliasili na Utalii. Ni Mbunge mteule wa Jimbo la Singida Kaskazini, ambaye analitumikia kwa miaka 20 mfululizo sasa.
Kabla ya kuwa Waziri wa Maliasili, alikuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo na ile ya Viwanda na Biashara, ambako alisimamia kwa uwazi maslahi ya wafanyabiashara wazawa dhidi ya wageni waliokuwa wameshamiri kwenye mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Nyalandu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutuliza wizara hiyo na taasisi zake tofauti na miaka ya nyuma. Pia ameshiriki kikamilifu vita dhidi ya ujangili kwa kuziwezesha taasisi husika kuwa na uwezo wa kutosha kukabiliana na mtandao wa ujangili ndani na nje ya nchi.
Kwa sasa Serikali ya China imetangaza kupiga marufuku biashara ya bidhaa zinazotokana na pembe za ndovu, ikiwa ni hatua kubwa ya kukabiliana na biashara hiyo.
Alifuta vibali vya uwindaji vya kampuni zenye historia mbaya za uwindaji kwa kujihusisha na ujangili na kuweka mazingira mazuri kwa watalii nchini.
Alizaliwa Agosti 18, 1970. Aliwahi kuwa Mshauri wa Masuala ya Kimataifa na Maendeleo wa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote (EOTEF), uliokuwa chini ya Mama Anna Mkapa, ambaye ni mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Ana Shahada ya Uzamili kwenye masuala ya Utafiti wa Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia, kutoka Chuo Kikuu cha Buckingham cha Uingereza.

DK. HARISSON MWAKYEMBE
Mpambanaji wa rushwa na ufisadi asiyeyumbishwa wala kutishwa. Aliwahi kuweka bayana kuwa yuko tayari kwa lolote ikiwemo kupoteza maisha yake wakati akipambana na mafisadi.
Itakumbukwa mwaka 2008, aliongoza Kamati Teule ya Bunge, ambayo ilimsomba na maji Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Rais Kikwete.
Utendaji kazi na misimamo isiyoyumba wala kuwa na chembe ya hofu, ndiyo iliyomjengea sifa kubwa Dk. Mwakyembe. Licha ya kuwa mwanasiasa anayepigwa vita kila kona na kundi la watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, lakini bado amesimama imara.
Alipata kufanyakazi na Dk. Magufuli katika Wizara ya Ujenzi, akiwa Naibu Waziri kabla ya kupanda na kuiongoza Wizara ya Uchukuzi na baadaye Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akiwa Uchukuzi, itakumbukwa fagio alilolitumia kusafisha uozo ndani ya Mamlaka ya Bandari kwa wakati huo na kurejesha heshima huku serikali ikikusanya mapato yake inavyostahili.
Usafiri wa Reli uliokuwa umedorora ulianza kurejea na uanzishwaji wa usafiri wa reli Dar es Salaam maarufu Treni ya Mwakyembe, ambayo inaendelea kutoa huduma zake mpaka sasa.
Alizaliwa Desemba 10, mwaka 1955. Licha ya kuwa na taaluma ya uandishi wa habari, lakini pia ana shahada ya uzamivu ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Hamburg.

Wasomi wamzungumzia
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Banna, alisema waziri mkuu atakayeteuliwa anapaswa kuendana na kasi ya Dk. Magufuli.
Alisema malengo ya kiongozi huyo ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, yanapaswa kushabihiana.
“Malengo ya waziri mkuu lazima yashabihiane na yale ya Dk. Magufuli, endapo wakiwa na mwelekeo tofauti inaweza kusababisha mtafaruku,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa, sifa nyingine ni uwezo wa kujenga hoja, kuwa na lugha za kibunge na uwezo wa kuwashukia watendaji muda na wakati wowote.
Profesa Banna alibainisha kuwa, uwezo wa kuifahamu serikali, kujiamini, kuheshimu Katiba na kusimamia kile anachokiamini ni muhimu kuzingatia kwa kiongozi huyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Deus Ngaruko, alisema waziri mkuu mtarajiwa lazima awe na uwezo wa kupokea mawazo mapya na ubunifu katika kutatua changamoto zilizopo.
Alisema kiongozi huyo anatakiwa kukubali kupokea maagizo, kuyatekeleza na awe na uvumilivu pamoja na lugha ya staha bungeni.
Alibainisha kuwa kutokana na idadi kubwa ya wabunge waliochaguliwa katika kipindi hiki ni vijana, anapaswa kujizuia na mihemko na lugha zisizostahili bungeni.
Profesa Ngaruko alisema waziri mkuu atakayechaguliwa, anapaswa kutokuwa na kashfa zenye kuthibitika na sio kashfa zisizoeleweka kwa kutotolewa uthibitisho.

No comments:

Post a Comment