Sunday, 1 November 2015

CCM YAWATAKA WATENDAJI WABOVU WAJIWEKE KANDO



NA PETER KATULANDA, MWANZA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza, kimesema watendaji wabovu katika ngazi zote wanapaswa kuachia ngazi, kwa kuwa awamu inayokuja itatekeleza kwa vitendo kauli mbiu yake ya hapa kazi tu.

Aidha, CCM mkoa wa Mwanza imesema haina cha kuwalipa wananchi kwa kuonyesha imani kubwa kwa Chama zaidi ya kuwaahidi kuchapa kazi ili kuwaletea maendeleo.

Kimeonya kuwa hakitakuwa tayari kuona uchakachuaji wa miradi na huduma za kijamii, hivyo adui namba moja wa vitendo hivyo watakuwa watendaji wa serikali watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hayo yalisemwa juzi na Katibu wa CCM mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu na baadhi ya wabunge wateule wa mkoa huo, wakati wa mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Mbugani.

“Watendaji wazembe sasa washuke kwenye gari, tumepata dereva mchapa kazi zaidi, Dk. John Magufuli na mbunge mpenda maendeleo Stanslaus Mabula, tunataka kwenda kasi kuwaletea maendeleo,” alisema Mtaturu.

“Uchaguzi wa mwaka huu ulijaa vibweka, mbwembwe, fujo na kujionea wagombea mbalimbali, akiwemo aliyekuwa akipigwa jeki majukwaani, lakini wananchi wameendelea kuiamini CCM na kumchagua Dk Magufuli, wabunge na madiwani wengi wa CCM, tunawalipa kwa kuwafanyiakazi usiku na mchana,” alisisitiza.

Mtaturu aliamsha shangwe uwanjani hapo alipodai kuwa Watanzania wengi hawataki mbwembwe, wanataka kazi ndiyo maana wamemchagua rais mchapa kazi na kuwaacha wasiokuwa na uwezo na dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo, akiwemo aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Elias Mpanda alisema CCM ilikuwa ikiwasisitiza Watanzania siasa zisiwafarakanishe, lakini wapinzani mtaji wao ulikuwa kupiga na kufarakanisha watu.

"Uchaguzi sasa umeisha ni kazi tu, hatutakubali uchakachuaji wa fedha, miradi na huduma za wananchi, adui wetu namba moja ni watendaji wa serikali wasiotaka kufanya kazi kwa uadilifu, tutawang’oa,” alisema Mpanda.

Naye mbunge mteule wa Nyamagana, Mabula alisema haijazoleka sehemu nyingi kushukuru mara moja baada ya kutangazwa mshindi, lakini yeye ameamua kufanya hivyo ili aungane na wananchi wote na kuondoa tofauti za kisiasa zilizokuwepo ili atakapoapishwa washirikiane kuchapa kazi.

“Hakuna cha kuwalipa zaidi ya kuwafanyia kazi usiku na mchana, japo sijaapishwa, lakini nimeishasoma robo tatu ya kazi na wajibu wa mbunge, nitasimamia majukumu yangu na kuitekeleza kwa dhati Ilani ya CCM,” alisema Mabula.

Aliwaomba wafanyabiashara ndogondogo (machinga) na mama lishe watulie, wasibabaishwe na maneno ya wahuni na kusisitiza kwamba atawajengea mazingira rafiki ya biashara.

Aliwapa pole wananchi na wana CCM waliojeruhiwa na kunyanyaswa wakati wa uchgauzi huo.

No comments:

Post a Comment