Sunday, 1 November 2015
UCHAGUZI UMEKWISHA, FANYENI KAZI-MONGELLA, BALOZI KAGASHEKI ANAWA MIKONO
Na Angela Sebastian, Bukoba
SERIKALI mkoani Kagera imewataka wananchi wa mkoa huo kutambua kuwa muda wa kampeni na uchaguzi umekwisha,
kilichobaki ni kufanyakazi kwa kushirikiana bila kujali itikadi za vyama vyao ili kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella, wakati wa mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, kwa ajili ya kuwashukuru wananchi waliowapigia kura wagombea wote waliosimishwana CCM.
Mongella alisema muda wa uchaguzi umemalizika hivyo hakuna sababu ya kuendeleza malumbano ya kisiasa kufanya vitendo vya vurugu.
"Huu sasa ni muda wa kutafuta maendeleo kwa kufanya shughuli zetu za kujipatia kipato kwa amani na mshikamano bila kuwabughudhi wenzetu kwa sababu ya itikadi na tofauti za vyama vyetu,"alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, yanaonyesha kuwa, aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ameibuka mshindi na hilo halikwepeki.
“Nasikia wapo baadhi ya vijana wanavamia majengo ya CCM, jengo la mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo la Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na kuwajeruhi wananchi hasa kinamama na kuharibu mali zao.
"Kuanzia sasa nasema yeyote atakayejaribu kuwabughudhi wenzake, atakamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya nchi kwani hakuna aliye juu ya sheria,” alisema Mongella.
Alisema ameamua kuhudhuria mkutano huo ulioitishwa na CCM kwa sababu ndicho Chama kilichoshinda uchaguzi mkuu na Ilani yake ndiyo itakayotekelezwa baada ya Dk. Magufuli kuapishwa rasmi kuwa rais.
Alisema akiwa mkuu wa mkoa, anapaswa kuitekeleza Ilani hiyo kwa vile yeye ni mwajiri wa serikali inayoongozwa na CCM.
“Kwa mfano, unapokuwa muuza duka na siku mtoto wa mwenye anafunga ndoa, ni lazima uende kusherehekea, kwa hiyo mimi ni muuza duka na CCM ndiye mwenye hilo duka,"alisema.
Aliwataka wafuasi wa CCM katika Manispaa ya Bukoba kuwa wavumilivu na kujipanga upya kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020 kutokana na jimbo hilo kuchukuliwa na chama cha upinzani.
Alisema mambo ya msingi wanayopaswa kujiuliza ni wapi walikosea ili wajirekebishe na kuhakikisha wanalirejesha jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao.
Mongella alitoa mfano wa mwanamke aliyebeba mimba, lakini kwa bahati mbaya mimba hiyo ikaharibika, kwamba hawezi kumsusa mume wake, isipokuwa watajiandaa kupata mtoto mwingine.
"Nanyi msikisuse chama, mnapaswa kujipanga upya kwa ajili ya uchaguzi mwingine,"alisema.
Katika mkutano huo, wabunge wateule wa CCM katika majimbo manane ya mkoa huo, waliwashukuru wananchi kwa kuonyesha imani kubwa kwao na kuwachagua kwa kura nyingi.
Naye mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Balozi Kagasheki, ambaye alishindwa na mbunge wa upinzani katika jimbo hilo, aliwashukuru wananchi na kuwataka wawe watulivu.
"Nilipata kura nyingi, lakini hazikutosha. Msifadhaike sana kwani hamuwezi kujua mipango ya Mungu ni ipi. Nakubaliana na usemi usemao asiyekubali kushindwa si mshindani.
"Ninawaomba wenzangu wa upinzani waache kunilisha maneno yasiyofaa, kama ni mbunge wameshampata, hivyo watulie na kupanga mipango ya maendeleo na sio kutoa matusi na kufanya vitendo vya vurugu,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment