Sunday, 1 November 2015

JUMUIA YA WASTAAFU ZANZIBAR YATOA KAULI UCHAGUZI MKUU KUFUTWA


Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazee wastaafu, Wakulima na Wafanyakazi  Zanzibar Mzee Ali Hassan Khamis akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu hali ya nchi ilivyo sasa na kuwataka wananchi kusikiliza maelekezo yatakayotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Picha na Makame/Maelezo Zanzibar.

RAMADHANI ALI /MAELEZO

Jumuia ya Wazee wastaafu, Wakulima na Wafanyakazi  Zanzibar imewashauri wananchi  kuwa watulivu wakati huu na kusikiliza maelekezo yatakayotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar  (ZEC) baada ya  Mwenyekiti wa Tume hiyo kufuta uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25.10.2015.

Akitoa tamko  juu ya hali halisi iliyojitokeza  katika uchaguzi huo mbele ya waandishi wa Habari, katika Ukumbi wa Redio Swahiba Migombani, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mzee Ali Hassan Khamis alikubali kuwa uchaguzi umevurugika  na lililobaki kwa sasa ni kusikiliza miongozo ya ZEC ili kusawazisha kasoro iliyotokea.

Mzee Ali Hassan alisema  Tume ya Uchaguzi ndio ya kulaumiwa katika kuharibika kwa uchaguzi wa Zanzibar licha ya juhudi kubwa iliyofanya ya kusimamia uchaguzi huo katika hatua za awali.

Alishauri kumalizwa  tatizo lililopo na wananchi wenyewe wa Zanzibar bila ya kushirikisha Jumuiya za Kimataifa kwani baadhi ya wakati  maamuzi yao yanakuwa katika ushabiki wa kisiasa.


Amesema Jumuiya ya Wazee  wastaafu, wakulima na wafanyakazi inaunga mkono kurejewa kwa uchaguzi wa Zanzibar  na hatua hiyo sio jambo kigeni kwa Zanzibar kwa vile imewahi kutokea katika miaka ya sitini.

Mzee Ali Hassan aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki vizuri katika uchaguzi huo kuanzia hatua ya kampeni na kupiga kura  katika misingi ya amani na utulivu.

Aidha alimpongeza Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Magufuli kwa ushindi aliopata na kuwataka wananchi wote kumuunga mkono katika juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi wote.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa kujumla kusahau tofauti  zilizojitokeza wakati wa kampeni  na  wakati wa kupiga kura  na kuelekeza mawazo yao katika kujenga Tanzania mpya.

No comments:

Post a Comment