Monday, 23 January 2017
TEMECO YADAIWA KUUZWA KINYEMELA
WANACHAMA wa Ushirika wa Mechanical Engeering Co-Operative Society (TAMECO), wamewashutumu viongozi wa ushirika huo kwa kuuza mali za ushirika kinyemela huku wakiwanyima stahili za gawio la hisa zao.
Miongoni mwa mali zilizouzwa ni pamoja na eneo la ushirika huo lililoko Keko, ambapo kwa sasa kumejengwa kituo cha mafuta cha MEKO OIL na godauni la kuhifadhi maji ya Pangani.
Mali zingine ni mashamba yaliyoko Mbande, magari na mashine mbalimbali zilizokuwa zikitumika kuzalishia bidhaa za kiwanda hicho.
Aidha,inadaiwa kuwa viongozi hao wamezuia gawio la hisa za wanachama 12, huku wakiwanyima kuwapa hati ya umiliki wa hisa hizo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka chanzo cha ndani, zimeeleza kuwa viongozi hao waliuza mali hizo mwaka 2013, bila ya kuitisha mkutano mkuu kwa ajili ya kujadili suala la kuuza mali hizo, ambapo ni kinyume na katiba ya TAMECO ibara ya 47.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa, katika mwaka 2011 hadi 2012, aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alifuta madeni yote yaliokuwa yakidaiwa kwenye vyama vya vya ushirika na ndipo mali za TAMECO zikiuzwa.
Geofrey Haule, mmoja ya wanachama hao, ambao wamenyimwa stahiki ya gawio la hisa, alidai kuwa Mwenyekiti wa TAMECO ameshikilia nyaraka za hatimiliki ya hisa zao na hadi sasa hawajapata gawio hilo.
Haule alisema viongozi hao wa TAMECO wamekiuka katiba na taratibu wa kuuza mali za ushirika, ambapo alitakiwa kuitisha mkutano mkuu wa wanachama ili kujadiliana kuziuza.
“Hadi sasa bado haijafahamika kama TAMECO iko kama ushirika ama imeshafutwa, lakini katiba yetu ibara 10, inaeleza kabisa kuwa TAMECO ilianzishwa kwa nguvu ya wanachama, hivyo hisa au mafungu yaliyoanzishwa na TAMECO ni mali ya wanachama, hivyo thamani yote ya mali ya chama hiki zitarudi kwa mwanachama,”alisema.
Alidai kuwa katiba imeeleza wazi kuwa kulingana na taratibu, kila mwanachama kulingana na fungu lake, ndio mali aliyonayo chamani pamoja na faida yake.
Haule aliendelea kudai kuwa katiba hiyo inatambua mali ambazo zimeelezwa ku ni pamoja a majengo, mashine, samani, magari, mitambo, mashamba yenye mimea na mazao ya kudumu, mifugo na mali zinazohamishika na zisizohamishika.
“Aidha katiba inaeleza kuwa mafungu yote ya chama hiki ambayo wanachama wameyalipa, yatahesabiwa kwamba ni mali za wanachama, lakini viongozi hawa wameuza bila kufuata katiba na kuwahusisha wanachama,”alisema,
Wanachama hao 12, ambao hawajalipwa stahiki zao na kuzuiliwa kupewa hatimiliki hizo za hisa, wamedai kuwa viongozi hao hawakutisha mkutano mkuu kujadili kuuzwa kwa mali hizo.
Kwa upande wake, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Sospeter Haule, alisema kuwa hana taarifa za kuuzwa kwa mali hizo na kwamba, bado serikali inatambua TAMECO kuwa iko kwenye orodha ya vyama vya ushirika.
Haule alisema viongozi wa TAMECO hawana jukumu la kuuza mali hizo bila kuitisha mkutano wa wanachama na kukubaliana kuuzwa kwa mali hizo na kwamba, kitendo hicho ni kinyume cha sheria na mwenyekiti huyo anatakiwa kupelekwa Mahakamani.
“Mimi kama Mrajis, sina taarifa kuwa TAMECO imefutwa ama imeondolewa kama chama cha ushirika, hivyo ili mali hizo ziuzwe au chama hicho kifutwe ama kuondolewa, viongozi walitakiwa kuitisha mkutano wa kukubaliana,”alifafanua
Mrajis huyo alisema mtu mwenye mamlaka ya mwisho ya kutoa kibali ni yeye, aidha ushirika huo ufutwe ama kuondolewa na hata katika kuuzwa kwa mali hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMECO, Remigius Mbawala, alipoulizwa kuhusu shutuma hizo, alikiri kuwa ni kweli mali hizo zimeuzwa tangu mwaka 2013.
Alisema TAMECO kwa sasa sio Chama cha Ushirika tena na kwamba, baadhi ya wanachama walikubali kuuza kutokana na mazingira yaliyokuwepo.
“Baadhi ya wanachama walikubali kuuza mali na kati yao wamenunua eneo Mkuranga kwa ajili ya kampuni, hivyo TAMECO sio tena ushirika bali ni kampuni,”alisema.
TAMECO ilianzishwa mwaka 1972 na kusajiliwa kama chama cha ushirika Julai 7,mwaka 1981 na kupewa hati namba DCC59, ambapo wanachama 21 ndio waliowasilisha maombi hayo ya kuwa chama cha ushirika kwa madhumuni ya kuendeleza kazi za ufundi chuma na kutengeneza bidhaa kama vile pembejeo za kilimo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment