Monday 23 January 2017

ANNE KILANGO AAHIDI MAZITO KWA RAIS MAGUFULI


MBUNGE mteule, Anne Kilango Malecela, amemshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kumteua katika nafasi hiyo na kwamba, ameahidi kuchochea mabadiliko anayoyataka.

Amesema nafasi hiyo ya ubunge aliisaka na kuipigania kupitia jimbo, lakini hakufanikiwa na sasa imekuja kwa mlango mwingine.

“Namshukuru Mungu na Rais Dk. Magufuli kwa kuniteua, taarifa hizi nimezipata saa tano usiku, nilipoamshwa na kuelezwa kuhusu uteuzi huo kwangu, ni jambo jema,”alisema.

Mbunge huyo mteule alisema amekaa miaka 15, akiwa katika nafasi hiyo, hivyo kurejea kwenye shughuli za kisiasa kwake hakuna ugumu na hahitaji kujipanga.

Alisema nafasi hiyo ya kuteuliwa ameipata kwa mara ya pili, baada ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kumteua kwa mara ya kwanza mwaka 2005.

“Sihitaji kujipanga na kwamba kinachohitajika ni kwenda bungeni kuhakikisha ninaleta chachu ya mabadiliko kulingana na kasi ya Rais Magufuli, anavyokwenda nayo,” alisema.

Juzi, Rais Dk. John Magufuli, alimteua Anne Kilango kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema mbunge huyo anatarajiwa kuapishwa katika wadhifa huo kulingana na utaratibu wa Bunge.

Kabla ya uteuzi huo, Anne aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na baadaye Rais Magufuli aliutengua uteuzi huo.

Katika serikali ya awamu ya nne, Anne Kilango alikuwa Mbunge wa Same Mashariki na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

No comments:

Post a Comment