Monday, 23 January 2017
CCM YASHINDA KWA KISHINDO, YATWAA TENA JIMBO LA DIMANI, YAZOA KATA 19 KATI YA 20
WANANCHI wa Jimbo la Dimani, Mkoa wa Magharibi, Unguja, wamejitokeza kwa wingi kupigakura katika uchaguzi mdogo wa marudio wa ubunge, huku hali ya amani na utulivu ikitawala.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa 1.00 asubuhi, wakati misururu ya wananchi ikiwa kwenye mstari kwa ajili ya kuanza kupiga kura.
Polisi wasio na silaha walionekana kusimamia utulivu katika vituo vyote vya kupigia kura.
Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juma Ali Juma, alipiga kura katika kituo cha shule ya sekondari Fuoni, saa 3.15 asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo hicho baada ya kupiga kura, Juma, alisema ana uhakika wa kuibuka mshindi.
"Nimeridhishwa na hali ya uchaguzi inavyokwenda. Amani imetawala na wananchi wamejitokeza kwa wingi. Kikubwa ninachoweza kusema ni kwamba, natarajia ushindi. CCM ipo kwa ajili ya kushinda na tutashinda,"alisema.
Waangilizi wa ndani na waandishi wa habari wenye vitambulisho maalumu, walikuwa huru kufuatilia kwa karibu kila hatua ya uchaguzi huo huku raia wakisema ni uchaguzi huru na wa haki.
“Kwanza ulinzi ni wa kawaida, ambao hautishii raia kujitokeza, hasa yule mwenye nia ya kutimiza haki yake ya kikatiba ya kupiga kura.
Lakini pia ni uchaguzi huru na wa haki kwa sababu kila chama kimeweka wakala wake. Kama kuna malalamiko kwa mawakala, basi zipo taratibu za kuchukua, ambazo wamekwishapewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),” alisema Mustafa Omari Komba.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jimbo la Dimani lina jumla ya wapiga kura 9,280 na vituo 29, vya kupigia kura.
Awali, akizungumza na vyombo vya habari mjini Unguja, kuhusu uchaguzi huo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, alisema kura zilizopigwa zitahesabiwa katika kituo cha kupigia kura baada ya upigaji kura kukamilika.
Hata hivyo, alisema matokeo hayo yatatangazwa baada ya kuwekwa kwenye fomu za matokeo Na. 21B kwa upande wa ubunge kisha fomu hizo kutiwa saini na Msimamizi au Msimamizi Msaidizi wa Kituo, Mawakala wa vyama au mgombea aliye kituoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment