Monday, 23 January 2017

JECHA AKATA MZIZI WA FITINA UCHAGUZI MKUU 2015


MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, amekata mzizi wa fitina kwa kuweka bayana uhuni wa kisiasa uliofanywa na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Jecha amesema matokeo ya kura alizojitangazia Maalim Seif kinyume na Katiba ya Zanzibar, akidai kushinda uchaguzi huo, zilikuwa kura za kupikwa, uongo zisizokuwa na ukweli wowote.

Amesisitiza kuwa, kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo kulisababishwa na kukithiri kwa vitendo vilivyokuwa vinakwenda kinyume cha sheria na taratibu za uchaguzi, ikiwemo kwa baadhi ya wagombea (Maalim Seif) kujitangazia ushindi.

Pia, alibainisha kuwa marudio ya uchaguzi visiwani Zanzibar, yalifanyika kwa mujibu wa sheria na katiba kutokana na idadi kubwa ya vyama vya siasa kujitokeza kushiriki, hivyo chama ambacho hakikushiriki uchaguzi huo, hakina sababu ya kulalamika.

Mwenyekiti huyo wa ZEC, alibainisha hayo jana, wakati alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Funguka, kinachorushwa hewani na kituo cha utangazaji cha Azam Tv.

Jecha alisema ripoti ya uchaguzi huo itakayokabidhiwa hivi karibuni, itabainisha vitendo vyote vilivyosababisha uchaguzi kufutwa huku akieleza kulikuwepo na utaratibu wa kiufundi wa kuharibu matokeo hayo.

“Kama alitoa matangazo kwenye TV kutoa hesabu za kura zake alizoshinda, hizo kura hazikuwa sahihi, ni uongo, zilikuwa za kubuni na kupika. Sio sahihi hata kidogo,"alisisitiza.

Alisema wakati matokeo ya Unguja yakipokelewa, hazikujitokeza hizo hitilafu, bali matatizo yalianza kujitokeza baada ya kuanza kupokelewa matokeo ya kura kutoka Pemba, kwani ilionekana dhahiri ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi.

“Utaratibu wa kiufundi ulifanyika kuharibu matokeo ya hesabu za kura. Kulitokea urekebishaji wa taarifa, ambazo hazikutakiwa kufanyika nje ya mfumo wa sheria na kanuni za uchaguzi. Polisi walifanya uchunguzi na kubaini watu waliofanya hayo na wanajulikana,” Jecha alisisitiza.

Alisema viongozi waliojitangazia ushindi walikuwa wanafahamu kuwa, wanavunja sheria, lakini tume hiyo haina mamlaka ya kuwakamata hivyo ZEC haikuwaonea kufuta uchaguzi huo.

“Vyombo vyenye mamlaka vipo na sio tume, nilisikia polisi walifanya uchunguzi kisha kufungua jalada, lakini sina uhakika. Kuhusu hatua zilizochukuliwa sifahamu,” alisema.

Pia aliongeza kuwa, hisia kali za uchaguzi Zanzibar, haziwezi kumalizika kwa sababu kuna baadhi ya viongozi wanapalilia jazba za kisiasa kwa kuwachochea wafuasi wao kufanya fujo.

Mwenyekiti huyo alisema, sheria haikuvunjwa katika kutangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi kwa sababu maridhiano yaliyokuwa yakifanyika hayakufikiwa muafaka na wakati mazungumzo hayo hajawahi kuitwa na serikali kwa majadiliano.

“Wakati hayo yanafanyika, mengi yalizungumzwa kwamba mwenyekiti atakwenda kufungwa ICC, lakini sikuwa na wasiwasi kwa sababu sikuvunja sheria wala kanuni za uchaguzi,” aliongeza.

Alisema kubadilisha sheria za uchaguzi hakuhakikishi kumalizika kwa changamoto za uchaguzi, bali kinachohitajika ni maridhiano kwa jamii husika.

Jecha, ambaye atamaliza nafasi yake ya uenyekiti wa ZEC, Aprili, mwaka 2018, alisema bado hisia za kikoloni kwenye baadhi ya vyama bado zipo, hivyo alivitaka vyama vya siasa kuacha jazba hizo kwa sababu bado wananchi wanashindwa kushirikiana kwenye huduma za jamii.

“Kule Pemba, mazao yanaharibiwa kwa sababu za kisiasa, nyumba zinachomwa moto, mifugo inauawa, vitendo hivyo sio vya kibinadamu hata kama tuna tofauti za kisiasa. Jazba za kisiasa hazifai,” alieleza.

Alisema wapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakipalilia jazba hizo kwa kuwachochea wafuasi wao, hivyo aliwataka viongozi waache kuendekeza tabia hiyo ili wananchi waishi kwa maridhiano.

No comments:

Post a Comment