Tuesday 28 June 2016

ASKARI FFU ALIYEMBAKA MWANAFUNZI AFUNGWA JELA MIAKA 30, ATOZWA FAINI MILIONI 15, KUCHAPWA VIBOKO 12



ASKARI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Raphael Mkongojo (25), amehukumiwa kwenda jela miaka 30, baada ya kukutwa na kosa la kumbaka mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya wasichana ya Korogwe.

Akisoma hukumu hiyo katika chumba cha faragha  jana, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Jasmin Abdul, alisema licha ya kufungwa miaka hiyo, mshitakiwa pia atatakiwa kulipa fidia ya shilingi milioni 15, kwa mhanga wa tukio hilo, kuchapwa viboko 12 pamoja na kupangiwa kazi ngumu kipindi chote atakachokuwa anatumikia kifungo hicho.

Rafael, alifikishwa katika mahakama hiyo Januari 19, mwaka huu,  ambapo alisomewa shitaka hilo na Mwanasheria wa Serikali, Sabina Silayo.

Mwanasheria huyo aliieleza mahakama kwamba, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 16, mwaka huu, katika eneo la kwa Mrombo, karibu na kilipo kikosi cha FFU.

Pia, aliieleza mahakama kwamba, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo la ubakaji kinyume na kifungu cha sheria namba130 na kifungu cha 131 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16.

NJE YA MAHAKAMA

Akizunguma kwa uchungu baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mama mzazi wa mtoto huyo, Hadija Ramadhani, aliipongeza mahakama kwa kutenda haki.

Alisema kitendo alichofanyiwa binti yake (jina linahifadhiwa ni cha kinyama na kwamba, kimemuathiri kisaikolojia yeye na familia yake.

Hadija ameiomba serikali kuongeza adhabu kwa wathumiwa wanaokutwa na kosa la ubakaji  kwa kufungwa kifungo cha maisha, badala ya miaka 30 ili iwe fundisho kwa wengine.

“Nitumie fursa hii kuiomba serikali kuongeza adhabu hii na kuwa kifungo cha maisha kwani mtuhumiwa atakapotoka gerezani, anaweza kufanya ukatili mwingine kama huo au kulipiza kisasi,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment