Tuesday, 28 June 2016
WAFUNGUA KESI KUPINGA BUNGE KUTOONYESHWA 'LIVE'
OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Julai 11, mwaka huu, itawasilisha majibu yake Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wananchi 11 kupinga hatua ya Bunge kutoonyeshwa moja kwa moja ‘live’.
Shauri hilo lililofunguliwa na wananchi hao dhidi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na AG, lilitajwa jana mbele ya Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abubakar Mrisho, ambaye alikuwa akimwakilisha waziri huyo na AG, aliomba kuwasilisha majibu juu ya madai hayo Julai 11, mwaka huu.
Kwa upande wa mawakili Peter Kibatala na Omary Msemo, waliokuwa wakiwawakilisha wananchi hao, walidai iwapo watakuwa na cha kujibu kutokana na majibu ya AG, watawasilisha Julai 15, mwaka huu.
Jaji Kiongozi Profesa Wambali alisema shauri hilo lipo mbele ya jopo la majaji watatu, akiwemo yeye, Ama-Isario Munisi na Sakieti Kihiyo, ambao wapo katika vikao vya mahakama.
Alisema upande wa walalamikiwa wawasilishe majibu yao Julai 11 na upande wa waleta madai iwapo watakuwa na cha kujibu, wawasilishe Julai 15, mwaka huu na kesi itatajwa siku hiyo kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya usikilizwaji.
Walalamikaji katika shauri hilo ni Aziz Himbuka, Perfect Mwasilelwa, Rose Moshi, Penina Nkya, Moza Mushi, Andrew Mandari, Hilda Sigala, Juma Uloleulole, Kubra Manzi, Ray Kimbito na Ben-Rabiu Saanane.
Kwa kupitia hati yao ya madai, wanaiomba mahakamaitangazwe kuwa raia wana haki Kikatiba ya kupata majadiliano ya Bunge chini ya Ibara ya 18(b) na (d) na Ibara ya 29(1).
Pia, wanaitaka mahakama itamke kwamba serikali inakiuka haki ya Kikatiba ya Tanzania, kwa kuzuia bila sababu za msingi mwananchi kupata majadiliano ya bunge kwa kuzuia majadiliano hayo yasirushwe ‘live’.
Aidha, wanaiomba mahakama kuielekeza serikali kurejesha haki hiyo ya kurusha ‘live’ majadiliano ya bunge.
Wananchi hao wanadai msingi wa kufunguliwa kwa kesi hiyo unaeleza sababu wanazoziegemea, ambazo ni serikali imezuia matangazo ya redio na televisheni ‘live’ ya majadiliano na vipindi vya bunge na makatazo hayo yaliyotangazwa na Waziri anayehusika na habari Januari 27, mwaka huu, akitaja sababu kwamba ni kupunguza gharama.
Wanadai matokeo ya kuzuiliwa huko, haki ya walalamikaji kama walivyo Watanzania wengine za kufuatilia na kuwasimamia wabunge zimezuiliwa kwa vile hawawezi kufuatilia jinsi vitendo vya wale wanaowawakilisha.
Mbali na hayo, wanadai kwamba makatazo hayo yameathiri haki ya Kikatiba ya walalamikaji ya kupata taarifa kwa vile hawawezi kupata majadiliano ya vipindi vya bunge kikamilifu kwa namna mfumo wa sasa wa utawala bora, uwazi na uwakilishi.
Wanadai sababu zilizotolewa na serikali kuzuia bunge ‘live’ hazijitoshelezi, hivyo kwa msingi huo na pengine Watanzania kwa ujumla, wana haki ya Kikatiba kuwakilishwa kikamilifu bungeni, ikiwemo haki ya kuwasimamia wabunge kupitia namna wanavyofanya wakiwa bungeni.
Pia, walalamikaji na pengine Watanzania kwa ujumla wana haki ya kupata taarifa kwa masuala ambayo yanaathiri maisha yao na taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment