Tuesday 28 June 2016

MAKONDA AMTUMBUA MHANDISI MKUU DAR

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul  Makonda,  amemwagiza Katibu Tawala, Theresia Mbando, kumsimamisha kazi mara moja,  Mhandisi Mkuu wa mkoa huo, Josephate Shehemba, baada ya kushindwa kutimiza majukumu yake.

Aidha, ameagiza  uchunguzi kufanyika dhidi ya wahandisi wote, ambao walipewa jukumu la kusimamia miradi ya barabara mkoani humu na kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo, hivyo kusababisha  miradi hiyo kukwama au kujengwa chini ya kiwango.

Pia, ameagiza kufanyika uchunguzi wa kina wa  kampuni za  ukandarasi zilizoshindwa kumalizia miradi ya barabara au kujenga chini ya kiwango  ili zichukuliwe hatua stahiki.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makonda alisema maagizo ya kusimamishwa kazi kwa Mhandisi Shehemba yameanza jana.

Makonda alisema mhandisi huyo anasimamishwa kazi kwa kushindwa kutimiza majukumu  yake kwa kufanya uzembe uliokithiri na unaoendelea kuupa hasara Mkoa wa Dar es Salaam, kwa ujenzi mbovu wa barabara na kupoteza mabilioni ya fedha.

Alisema mhandisi huyo alishindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo na kila alipokuwa akielekezwa, alikuwa akienda kinyume na maelekezo.

“Hatuwezi kuendelea kuwa na watendaji wa aina hii na kila kukicha tunapata madhara makubwa  yanayorudisha nyuma maendeleo, ambayo tunaamini kwamba tungeyapata,”alisema Makonda.

“Tumeaminiwa kuwa watumishi  na Rais Dk. John Magufuli ili tuwatumikie wananchi, lakini  kwa muda mrefu kuna baadhi ya watu wanaendelea kufanya kazi  kwa mazoea na  tunapoelekezana tufanye kazi, wao wanafanya kazi za kwao,”alisema Makonda.

Alisema barabara  nyingi  za Dar es Salaam ni mbovu  ingawa wasimamizi wake  hawawajibiki kwa lolote.

“Tunaye injinia ambaye kazi yake kubwa ni kutoa maelekezo na ushauri wa kitaalamu wa mara kwa mara katika ujenzi  wa barabara na mahali ambapo hatufuati utaratibu, yeye ndiye mwenye wajibu wa kumshauri mkuu wa mkoa. Huyu mhandisi hajawahi kufanya hivyo na  kila akipewa majukumu, amekuwa akifanya nje ya maelekezo,”alibainisha Makonda.

Alisema  barabara mkoani Dar es Salaam hazikustahili kujengwa chini ya kiwango kiasi  cha kufanya wananchi kulalamika kila kukicha, hivyo kufanya wakuu wa wilaya na mkuu wa mkoa kuingilia kati.

“Pia, nimeagiza uchunguzi  wa wakandarasi wote waliojenga  barabara chini ya kiwango, ambao wameshindwa kumalizia kazi walizopewa,” alisema.

Kundi lingine ambalo limekalia kuti kavu ni la wahandisi waliopewa jukumu  la kusimamia barabara hizo, ambao walitakiwa kufuatilia hatua kwa hatua hadi mradi unapokamilika, lakini walishindwa kufanya hivyo.

Pia, alionya watendaji wenye tabia za mnyama aina ya nyumbu za kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maagizo tu bila wao kubuni na kufikiri.

No comments:

Post a Comment