WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amekutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kwa lengo la kuangalia namna kila chombo kitakavyowezesha kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi.
Kikao hicho pia kimelenga kujadiliana namna vyombo hivyo vitakavyowezesha mahakama hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Viongozi hao walikutana mjini hapa jana, ikiwa ni muda mfupi baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishaji wa Mahakama ya Mafisadi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Hazina, baada ya kufungua mkutano huo, Dk. Mwakyembe alisema mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wote wa taasisi, ambazo zipo kwenye mfumo wa haki jinai, ikiwemo Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Mahakama na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
“Kikao hiki kinafanyika kipindi muafaka kwani tayari Bunge limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali, ambao unatoa mwanya wa kuanzisha mahakama ya mafisadi na makosa ya rushwa,” alisema.
Waziri huyo alibainisha kuwa vyombo hivyo ni muhimu na katika mkutano huo, watajadili na kuangalia namna gani kila chombo kitaweza kufanikisha uanzishaji wa mahakama hiyo, ikiwa ni pamoja na kujenga ushirikiano.
Akizungumza kuhusiana na mkutano huo, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Biswalo Mganga, alizitaja changamoto zinazoikabili haki jinai nchini kuwa ni uhalifu, ambao unafanywa na Watanzania wenyewe na miongoni mwao wengine ni raia kutoka nje na wanashirikiana na Watanzania.
Mganga alitanabaisha kuwa changamoto nyingine ni vyombo vya habari kuingilia upelelezi, tatizo la uelewa kwa jamii na watumishi na maadili, ambazo zinaangaliwa ili ziweze kuboreshwa.
Aliwageukia waandishi ambapo alisema wamekuwa na nia nzuri ya kutoa habari, lakini wakati mwingine wamekuwa wakivuruga mipango mizuri ya serikali katika kupambana na uhalifu au makosa kwa kusambaza taarifa mapema kwa jamii kabla upelelezi haujakamilika.
“Nawasihi na ninawaombeni tusitoe taarifa kabla ya upelelezi kukamilika na tunapoambiwa upelelezi bado haujakamilika, tuwaache watu wa taaluma zao wafanye kazi,”alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani, alisema kikao hicho ni muhimu kwa mustakabali wa nchi.
Alisema kama nchi haina amani, utulivu na usalama, haiwezi kukaliwa wala kutawalika.
No comments:
Post a Comment