JAMBAZI sugu Salum Said, aliyekuwa akituhumiwa kuhusika na mauaji yaliyotokea msikitini mkoani Mwanza, ameuawa wakati wa majibizano ya kurushiana risasi na polisi.
Wakati Said akiuawa baada ya kuwekewa mtego na polisi huku akikutwa na bomu la kurusha kwa mkono, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imefanikiwa kumuua mtuhumiwa mwingine wa ujambazi, anayedaiwa kuhusika katika mauaji ya watu wanane yaliyotokea Tanga.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari.
Akizungumzia kuuawa kwa Said, Kamishna Sirro alisema mtuhumiwa huyo baada ya kufanya tukio hilo Mwanza, alikimbilia Dar es Salaam.
Alisema polisi wakati wa ufuatiliaji wa mtuhumiwa huyo aliyehusika na mauaji msikitini mkoani Mwanza, asubuhi ya Juni 27, mwaka huu, maeneo ya Buguruni, kikosi kazi kilimwekea mtego kwa kutumia msiri.
“Alipokaribia kwa msiri huyo, ghafla akagundua kuwa ni askari, hivyo alirusha bomu la mkono na kuanza kukimbia, hivyo polisi walitumia risasi za moto na kufanikiwa kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake na kufariki dunia,” alisema Sirro.
Kuhusu mtuhumiwa wa mauaji yaliyotokea Tanga, Kamishna Sirro alisema Juni 25, mwaka huu, polisi katika kanda yake walifanikiwa kuwakamata watu wawili walioonekana kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na mtuhumiwa Mohamed Abdallah au Abuu Seif.
Alisema mtuhumiwa Abdallah ndiye mhusika wa kutekeleza mauaji ya watu hao katika kitongoji cha Kibatini, Tanga.
Kamishna Sirro aliwataja watu waliokuwa wakifanya mawasiliano na mtuhumiwa huyo kuwa ni Saada Abdallah (27), mkazi wa Segerea na Maramba Mawili, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Udaktari Muhimbili na dereva wa malori wa Kampuni ya TITANIC, Rashid Mangwena (26), mkazi wa Kigogo Mkwajuni.
Alisema watu hao walifuatiliwa baada ya kupatikana kwa taarifa kwamba, mtuhumiwa baada ya kufanya mauaji hayo, alikimbilia Dar es Salaam kama sehemu ya maficho ili kuepuka kukamatwa.
Kamishna Sirro alisema walipohojiwa, watu hao wawili walieleza mahali anapoishi Abdallah, ambaye alikuwa akitafutwa kwa miaka mitano kwa tuhuma za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha maeneo mbalimbali nchini.
Alisema baada ya polisi kutambua mahali anakoishi mtuhumiwa, Juni 26, mwaka huu, saa mbili usiku, timu iliandaliwa kwa lengo la kuizingira nyumba ya Saada, ambaye taarifa zilisema huwa anatembea na bastola na bomu la kutupa kwa mkono.
Kamanda Sirro alisema baada ya askari kuzunguka nyumba hiyo, ghafla mtuhumiwa alitoka ndani ya nyumba na kuanza kukimbia huku akiwarushia risasi askari, kitendo kilichosababisha askari kuanza kujibu mashambulizi dhidi ya mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema baada ya kumkagua mtuhumiwa huyo, alikutwa na bastola aina ya Norinco, iliyofutwa namba, ikiwa na risasi tatu ndani ya magazini na risasi nyingine 19, zikiwa kwenye mfuko wa suruali aliyokua amevaa na bomu la kurusha kwa mkono.
Pia, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu kwa kujihusisha na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha, ikiwemo jaribio la uvamizi wa Kituo cha Polisi Korogwe, mwaka 2013, ambapo walimjeruhi askari polisi mkono.
Matukio mengine ni uvamizi wa vituo vya mafuta na uporaji katika maduka ya Tigopesa na Mpesa mkoani Tanga, mauaji ya watu watano na uporaji wa fedha Central Bakery Tanga, mauaji ya askari na uporaji wa silaha Kituo cha Polisi Stakishari, Dar es Salaam.
Pia, anadaiwa kuhusika na mauaji ya ya askari wa JWTZ katika mapango ya Amboni na mauaji ya askari polisi maeneo ya TAZARA, Dar es Salaam kisha kufanikiwa kumpora bunduki aina ya SMG.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kujihusisha na kuwaingiza vijana kwenye kundi la kihalifu kwa kuwapa mafunzo ya kijeshi vijana 150.
Kamanda Siro alisema polisi wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliotoroka kutoka mapangoni ili kukomesha wimbi la uhalifu nchini.
Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili, raia wa Uganda, wakiwa na pembe za ndovu 660 na mashine ya kukatia pembe hizo.
Watuhumiwa hao ni Juma Said (54) na Ally Sharif (26), ambao walikamatwa Juni 26, mwaka huu, maeneo ya Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam.
Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika nyumba ya kupanga waliyokuwa wanaishi na kukutwa na pembe hizo.
Kamanda huyo wa polisi aliwataka wamiliki wote wa nyumba kuhakikisha wanakuwa na picha za wapangaji wao katika mikataba.
No comments:
Post a Comment