SERIKALI imesema ni vyema vyama vya siasa kutii amri ya jeshi la
polisi ya kutofanya mikutano ya kisiasa, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa
bila kujali ni chama gani au kiongozi gani aliyehusika.
Mbali ya hilo, imesema
itaongeza vikosi vya ulinzi na usalama katika visiwa vya Pemba ili
kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi kwa usalama na mali zao.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni,
alisema hayo bungeni jana, wakati akijibu swali la Yusuph Salim Hussein (Chambani-CUF).
Alisema kauli iliyotolewa na jeshi la polisi ya kuzuia mikutano
hiyo kufanyika ni halali kwani hakuna mtu, ambaye yupo juu ya sheria.
“Polisi ndiyo chombo pekee cha kuangalia ulinzi wa watu na mali
zao, hivyo hakutakuwa na mikutano mpaka hapo itakapotoa taarifa nyingine,’’
alisema.
Alisema serikali inatambua kuwa kila inapofika wakati wa uchaguzi mkuu
katika kisiwa cha Pemba, baadhi ya watu hujichukulia sheria mikononi kwa
kuwapiga wengine na kuharibu mali zao.
Naibu waziri huyo alisema hadi sasa tayari watuhumiwa kadhaa wamekamatwa
kutokana na matukio yaliyojitokeza, ikiwemo kuchomwa moto nyumba ya Kamishna wa
Polisi Zanzibar.
Alisema kesi mbili zimeshafikishwa mahakamani na zingine zipo kwa
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na kumuomba mkurugenzi huyo kuharakisha kesi hizo
ili ziende mahakamani.
“Naomba kupitia bunge hili nitoe wito kwa wananchi wote kuacha
mihemko ya itikadi za kisiasa wakati na kabla ya uchaguzi kwani hatua kali zitachukuliwa
dhidi yao,” alisema.
Katika swali lake, Hussein alitaka kujua iwapo serikali inajua
kuwa raia hupigwa na kuharibiwa mali zao, hasa wakati wa uchaguzi kwa upande wa
Zanzibar na hatua gani zimechukuliwa.
No comments:
Post a Comment