Thursday 28 July 2016

NEEMA YAJA KWA WATUMISHI WA CCM


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli amesema haiwezekani kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Chama anachokiongoza kiwe chini kuliko cha watumishi wa serikali.

Rais amesema changamoto ya maslahi kwa watumishi wa umma itakuwa ni ya kwanza kuishughulikia katika utendaji wake ndani ya CCM.

Aidha, ametangaza vita kwa watendaji wa Chama waliozoea kujinufaisha kwa manufaa yao binafsi.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo mjini hapa jana. katika ukumbi wa makao makuu ya CCM (White House), wakati akijitambulisha kwa watumishi wa CCM makao makuu na kuwashukuru kwa kazi waliyofanya wakati wa uchaguzi.

“Nawahakikishia kuwa sitawaangusha, naombeni mniamini na mnipe muda, sitaki kusema mengi maana mengine tutayafanya kwa vitendo,”alisema.

Alisema CCM ni Chama kikubwa chenye mali na rasilimali nyingi, lakini inashangaza kuona wanachama wake na Chama chenyewe kinakuwa ombomba na kwamba chini ya uongozi wake, hawezi kukubali jambo hilo liendelee.

Rais alisema anatambua kima cha chini cha mshahara wanacholipwa watumishi kuwa ni kidogo na hakikidhi mahitaji yao, ndio maana wakati mwingine wamekuwa wakirubuniwa na kurubunika kwa urahisi na kuweka maslahi yao mbele huku ya Chama yakifanywa baadaye.

Alisema atahakikisha changamoto ya maslahi kwa watumishi anaitatua na kuipatia ufumbuzi wa kweli kwa kuwa uwezo upo bali kinachohitajika ni kujipanga ili kufanikisha hilo.

Dk. Magufuli alisema Chama kinamiliki viwanja zaidi ya 5,261 nchi nzima, ambapo kwa Dar es Salaam, pekee vipo viwanja zaidi ya 400.

“Mali hizo zipo kila mahali nchi nzima, viwanja vya mpira, vibanda vimepangishwa, lakini fedha hazionekani zinakwenda wapi, haiwezekani kabisa Chama kikubwa kama hiki wafanyakazi wake wakafa njaa na kuwa ombaomba.

“Sisi tuwe Chama tawala, mimi niwe Rais, halafu kima cha chini cha mshahara kwa watumishi ni kidogo kuliko serikalini, suala hili haliwezekani hata kidogo,”alisisitiza.

Aliwatahadharisha kwa mara nyingine viongozi ndani ya Chama waliozoea kujinufaisha na mali za CCM, waziteme haraka.

“Unaweza kukuta jengo limepangishwa na wapangaji wanalipa kodi, lakini anayefaidika ni mtu mmoja kwa kuwa ni kiongozi, jambo hilo halitakuwepo na wala halikubaliki katika uongozi wangu,”alisema.

Alibainisha kuwa anataka mali za CCM ziende kwenye Chama na kuwanufaisha wanachama wote bila kujali wadhifa wa mtu.

“Mimi kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM ni bahati mbaya kwa watendaji wa aina hiyo,”alisema.

Alisema lengo na nia yake ni kuhakikisha Chama kinasonga mbele na kuendelea kushika dola kwa kuwa madarakani miaka yote.

Rais. Dk. Magufuli alisema mahali popote panapoitwa makao makuu ya Chama, ndipo uongozi halali unapotoka, hivyo lazima kuwa na watendaji waadilifu.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, wanaokiharibu Chama ni wanachama wenyewe na kwamba, inawezekana kuna baadhi yao wanachukua taarifa za CCM na kuzipeleka upinzani, ambapo alionya kama wapo wenye tabia hiyo waache.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hakuna mwenyekiti aliyewahi kushinda kwa asilimia 100 tangu kuanza kupatikana kwa wenyeviti wa Taifa wa CCM kama ilivyotokea kwa Dk. Magufuli.

Alisema ushindi huo unadhihirisha kuwa wanachama wote wana imani naye kubwa na wako tayari kufanya naye kazi.

Kinana alimshukuru Dk. Magufuli kwa imani yake kwao na kuirudisha sekritarieti yote ya CCM na kumuahidi kuyafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa kwa sekretarieti hiyo, aliyokutana nayo kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Alisema chini ya uongozi wa Dk. Magufuli, ana hakika Chama kitakuwa imara kwa kutekeleza kauli mbiu ya Mwalimu Julius Nyerere inayosema, 'Mimi Nang’atuka, lakini naendelea kuamini bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba'.

Katibu Mkuu Kinana alisema moja ya kazi za CCM baada ya uchaguzi mkuu ni kusimamia serikali na kutangaza mazuri yanayotekelezwa na serikali na kwamba, kazi hiyo wataifanya kwa umakini mkubwa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Magula, alisisitiza ajenda ya kuwashughulikia wasaliti ndani ya Chama iko pale pale.

Alisema suala la wasaliti ni jambo la kikanuni, hivyo lazima watashuhulikiwa ili kujenga Chama imara.

“Hakuna kifungu chochote kilichofutwa kwenye katiba ya CCM, uamuzi uko pale pale, watashughulikiwa,”alisema.

No comments:

Post a Comment