Tuesday 26 July 2016

NAMSHUKURU MUNGU NIMEIACHA NCHI IKIWA SALAMA NA YENYE AMANI KAMA NILIVYOIKUTA- KIKWETE


Na David John, Pwani

MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha Mapinduzi CCM (CCM), Dk. Jakaya Kikwete amesema anamshukuru Mungu kwa kuutua mzigo wa kuiongoza nchi salama huku akiicha ikiwa salama.

Amesema safari yake ya urais  ilianzia Bagamoyo, na baada ya hapo alikwenda Kibaha kutangaza nia ya kugombea urais, hivyo amejisikia fulaha kurudi tena Bagamoyo akiwa salama.

Amesema wakati  akielekea kutangaza nia ya kugombea urais, alikuwa ameambatana na mtoto wake Ridhiwani, ambapo yeye alikuwa anaandika hotuba na Ridhiwani anachapa kwenye komputa.

Dk. Kikwete aliyasema hayo jana, wilayani Bagamoyo, katika hafla ya kumkaribisha nyumbani baada ya kuitumikia nchi kwa miaka  mingi. Hafla hiyo iliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani.

Alisema anashukuru kwa mara nyingine kurudi mahala alipoanzia safari ya urais na kwamba amemaliza salama na ameacha nchi ikiwa salama huku ikiwa imetulia tulii kama maji kwenye mtungi. 

Alisema wakati pekee mgumu alioupata wakati wa uongozi wake, ni mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, mwaka jana, ambapo yalijitokeza mambo mengi magumu, lakini anamshukuru Mungu kwamba mchakato huo ulimalizika salama na kwa amani.

“Ilikuwa kazi kubwa, sio ndogo, lakini hatimaye tukavuka na kuingia kwenye uchaguzi ambao ulikuwa na vurumai nyingi, ” alisema Dk. Kikwete.

Alisema licha ya matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, hakukuwa na matukio yoyote yaliyohatarisha usalama na amani ya nchi, jambo lililozishangaza nchi nyingi za kiafrika.

Dk. Kikwete alisema katika kipindi cha uongozi wake, alifanya kazi kubwa ya kusukuma mbele maendeleo ya nchi katika mikoa na wilaya zote bila ubaguzi huku akikabiliana na changamoto ya kunyooshewa vidole, hasa alipojaribu kupeleka maendeleo wilayani Bagamoyo.

Aliitaja changamoto nyingine aliyokumbana nayo kuwa ni kusimamisha fedha za ujenzi wa barabara ya Bagamoyo na kuzipeleka kujenga barabara za Geita, Sengerema, Usagara na kwingineko, ambapo yalizuka maneno mengine mengi hadi kufikia wabunge kulumbana.

Hata hivyo, alisema anamshukuru Mungu amemaliza uongozi wake salama na kumkabidhi nchi Rais Dk. John Magufuli, ambaye ana ari kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo. Aliwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli kwa nguvu zote ili aweze kufanikisha azma yake hiyo.

No comments:

Post a Comment