Tuesday 26 July 2016

MAJALIWA: NITAHAMIA DODOMA SEPTEMBA MWAKA HUU



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza mawaziri wote wa serikali kuhamia Dodoma mara moja ili kutekeleza agizo la rais la makao makuu kuhamia Dodoma rasmi.

Majaliwa alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akitoa salamu kwa wananchi wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mashujaa.

Alisema anatoa kauli hiyo huku akitambua kuwa mawaziri wote wana nyumba za kuishi mkoani Dodoma, hivyo watekeleze kauli hiyo mara moja.

Waziri Mkuu Majaliwa alifafanua kuwa, yeye binafsi anatarajia kuhamia mjini Dodoma Septemba, mwaka huu.

“Nafi kiri wote tumesikia kauli ya rais ya makao makuu kuhamia Dodoma, sasa mimi naagiza mawaziri wote wahamie Dodoma mara moja,”alisema.

Majaliwa alisema kuwa juzi alimwita Katibu Mkuu na Waziri wa Nchi Ofi si wa Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana , Ajira, Kazi na Walemavu, kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa nyumba yake atakayokuja kuishi.

Alitoa wito kwa wananchi na Watanzania kuchangamkia fursa za kiuchumi, kwani watu watakuwa wengi na wanahitaji huduma, hivyo hawana budi kuongeza hoteli nyingi, ikiwemo za kitalii.

Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela, alimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kutimiza furaha yake na kuufanya moyo wake uchemke kwa kutoa kauli ya kukamilisha makao makuu ya nchi kuhamia Dodoma.

“Umeanza vizuri, endelea vizuri, ukijua kuwa sisi tupo bega kwa bega katika utendaji wako wa kuwatumikia Watanzania….katika siku mbili ambazo ni siku ya Mkutano Mkuu maalum wa CCM na jana, nimesikia maneno yenye amani ndani ya moyo wangu na yameufanya uchemke, maneno ya makao makuu kuwa Dodoma aliyotamka baba wa taifa sasa yanatimia,”alisema.

Malecela alisema wanatambua kazi anayoifanya katika maeneo yote aliyopita na kusema: “Umekuwa kama Yesu alisema neno moja tu yule mtoto mgonjwa akapona, nawe umesema neno moja tu wana Dodoma tumepona.”

Alisema hawatakuwa nyuma yake, bali  watakuwa bega kwa bega katika kuhakikisha yale yote aliyowaahidi Watanzania katika kampeni zake anayatimiza, ikiwemo suala hilo la serikali kuhamia Dodoma ambapo alimshukuru kwa niaba ya mkoa.

Naye, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema suala la kuhamia Dodoma limekawia, lakini kukawia si kufi ka, huku akipongeza hatua hiyo kubwa.

Alisema jambo hilo walikubaliana kwa pamoja, hivyo sasa linatekelezwa na kuwasihi Watanzania kufanya mambo kwa matendo ili kumwuunga mkono Rais Dk. Magufuli na si kuleta maneno.

No comments:

Post a Comment